Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. ZAWADI K. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuendelea kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitachangia kwa utaratibu kabisa ili labda Wizara kupitia Waziri mwenye dhamana pamoja na Naibu Waziri wake waweze kunisikiliza kwa umakini na kuweza kupata kile nilichonacho kuhusu viwanda na biashara katika nchi yetu hii ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanza kwa kusema kwamba kama kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa lolote lile, basi viwanda ni nguvu na kichocheo cha maendeleo ya uchumi katika Taifa lolote lile. Ili tupate mapinduzi ya viwanda pamoja na kilimo tunahitaji kuwa na teknolojia ya kisasa ili kuweza kuleta tija katika uzalishaji wa kilimo pamoja na uzalishaji wa viwandani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika nchi yetu ya Tanzania mpaka sasa tumeshindwa kufungamanisha kilimo pamoja na viwanda. Mheshimiwa Rais anayo nia njema sana anaposema anahitaji kuona Tanzania ya viwanda ili kuweza kuufikia uchumi wa kati. Sijui ni wapi tunakwama hadi tunashindwa kufikia yale malengo na azma njema ambayo viongozi wetu waliopita na waliopo sasa wamekuwa wanayo toka enzi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara, pamekuwepo na mapungufu ama changamoto ya upatikanaji wa fedha. Mimi naomba nijikite katika fedha za maendeleo. Fedha za maendeleo katika Wizara hii ya Viwanda na biashara kwa mwaka 2018/2019 imepelekwa kwa asilimia 6.48 tu. Swali tu la kujiuliza sisi kama Waheshimiwa Wabunge, kweli tunaweza tukaifikia azma ya Mheshimiwa Rais ya nchi ya viwanda na kutupeleka kwenye uchumi wa kati? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo taasisi mbalimbali katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara ambazo zingeweza kusaidia uchochezi wa kuwa na kilimo cha kisasa na tekonolojia ya kisasa katika viwanda vyetu nchini Tanzania. Tunazo Taasisi kama vile TEMDO, CAMARTEC, TIRDO pamoja na SIDO. Nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara, Kamati ilikwenda kutemebelea miradi hii ya taasisi hizi ambazo nimezitaja, cha kusikitisha sana tulivyofika katika taasisi hizi hakuna fedha hata shilingi moja ambayo ilikuwa imeenda kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Zaidi Kamati ilifika pale na kukuta kwamba yale machache ambayo yamefanyika na ambayo ni mazuri yametumia fedha kiasi kidogo tu ambacho kilipelekwa kwa mwaka wa fedha 2017/ 2018. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naomba niwapongeze watumishi wote ambao wanafanya kazi katika Taasisi za TEMDO, TIRDO pamoja na CAMARTEC. Watumishi hawa wanafanya kazi katika mazingira magumu lakini wameweza kujitoa katika kuhakikisha wanalisaidia Taifa hili na kumsaidia Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba azma ya viwanda inakwenda kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia katika ukurasa wa 72, 73, 74 na 75 Mheshimiwa Waziri amejinadi na kujieleza pale kwamba hizo taasisi za TEMDO, TIRDO na CAMARTEC ni namna gani zinaenda kutekeleza wajibu wake. Huo ndiyo mkakati ambao ametueleza katika kitabu chake lakini cha kusikitisha hajaweka mikakati, kama taasisi hizi hazipokei fedha unatarajia haya ambayo umeyaandika katika kitabu hiki Mheshimiwa Waziri yatatekelezwa vipi kama si kwamba unatutaka sisi kuziwekea lawama taasisi hizi lakini fedha hawana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua nitakuwa nimeongea kidogo kwa sauti iliyokuwa juu, lakini naamini kwamba ninaeleweka vizuri ninapoenda kuongelea suala hili. Kamati ilipotembelea katika taasisi zile tumekuta mambo ambayo kwa kweli yalitudhoofisha sana na tulijiona kuwa kama Kamati tumepelekwa pale kwenda kufanya nini kama sio tu kupoteza muda na kuchezea pesa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika Taasisi ya CAMARTEC mishahara inayolipwa ni mikubwa ukilinganisha na mapato ambayo yanapatikana. Uzalishaji uliopo ni mdogo ukilinganisha na mishahara mikubwa ambayo inalipwa katika taasisi hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwaka 2016/ 2017, ililipwa shilingi milioni 900 ya mishahara ilhali mapato ya ndani ya mwaka huo yalikuwa ni shilingi milioni 242. Hiyo, haikutosha, mwaka 2017/2018 zimelipwa pesa milioni 864 wakati mapato ya ndani yalikuwa ni shilingi milioni 253. Mwaka 2018/2019 hadi kufikia mwezi Machi wamelipa mishahara shilingi milioni 362 wakati mapato yake hadi kufikia mwezi Machi ni shilingi milioni 214. Kwa trend hii siamini kama kweli tutaweza kufikia Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri Serikali kuhakikisha kwamba wanachukua ushauri wa Kamati ambao imeutoa kuangalia taasisi hizi zinaenda kuwekwa chini ya management moja. Taasisi zinapokuwa under one management itaweza kuangalia sasa hivi pesa ipelekwe wapi na kufanya nini. Pia wale wafanyakazi ambao wameajiriwa katika zile taasisi wanakuwa na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nijielekeze katika suala la Electronic Tax Stamp. Naamini mfumo huu wa ukusanyaji kodi kielektroniki umelenga kuwabaini wale ambao sio waaminifu katika ulipaji kodi. Ni suala zuri na mimi naipongeza Serikali kwa kubuni mfumo huo. Hata hivyo, gharama zile ambazo zinatumika kwa ajili ya ku-collect ile tax kwa wafanyabiashara ni kubwa sana. Kwa mfano, kijoti kile cha juice ya Azam, pact moja inatakiwa kulipa kodi ya Sh.3 lakini katika mfumo huu wa Electronic Tax Stamp gharama ya ku-collect ile Sh.3 ni Sh.9. Hebu angalia tunatumia Sh.9 kukusanya kodi ya Sh.3, hivi kweli inaingia akilini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali watakapokuja ku-windup watusaidie kutuambia ni mfumo gani ambao ulitumika kumpata huyu mwekezaji ambaye aliuweka huu mfumo. Hata Kamati wamesema pale kwamba, huu mfumo hauna teknolojia ambayo unaweza kusema kwamba it is a rocket science. Mfumo hata wewe binafsi unaweza ukaubuni. Kwa nini TRA haikufikiria kuwekeza wao wenyewe katika mfumo huu na kuleta mwekezaji? Naishauri Serikali iweze kukaa na huyu mwekezaji ili waweze ku-review zile gharama za kukusanya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)