Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye mjadala huu wa bajeti ya Wizara hii muhimu sana ambayo inachukua sehemu kubwa ya keki ya bajeti ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea, naomba muungane nami kumpa pole Secretary wangu ambaye alfajiri hii amepotea mume wake, Mama Dionisia Mkoma, ndiyo maana sijakaa vizuri hata mimi mwenyewe.

MBUNGE FULANI: Pole sana.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Ahsante.

Mheshimiwa Spika, pia naomba nitoe pongezi mahsusi kwa Mheshimiwa Rais ambaye ameendelea kutoa kipaumbele cha juu kwenye ukarabati na ujenzi wa miundombinu msingi, yaani basic infrastructure na hii amefanya kwa umahiri mkubwa tangu alipokuwa Waziri wa Ujenzi; na kwa kweli alitambua mapema sana kwamba miundombinu ni kichocheo na mhimili mkuu wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana Mhandisi Kamwelwe na Naibu Mawaziri Mhandisi Elias Kwandikwa, Mhandisi Atashasta Nditiye. Kwa kweli wanatekeleza majukumu yao vizuri pamoja na watendaji wao ambao wamekaa kule nyuma ya kioo wakiongozwa na Makatibu Wakuu husika. Niseme mapema kabisa kwamba naunga mkono hoja ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema, ninaunga mkono kwa sababu kwa kweli uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa inachochea uchumi na maendeleo ya nchi na watu wake kwa namna nyingi ambazo Waheshimiwa Wabunge wanazifahamu. Ujenzi wa miundombinu unatengeneza fursa nyingi sana za ajira, lakini pia kipato kwa wananchi wetu. Ujenzi na ukarabati wa miundombinu unatumia nguvu kazi yenye ujuzi na ndiyo maana bench pale tunaona ni Wahandisi watupu au waliowatangulia ni wanasayansi na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, pia miundombinu bora inapunguza sana gharama za uwekezaji na uzalishaji na inaongeza uwezo wa kusafirisha watu, malighafi, bidhaa na kadhalika na kufanya biashara iende kwa haraka zaidi. Kwa kweli moja ya tofauti kubwa ya nchi zetu masikini na nchi zilizoendelea ni ubora wa miundombinu. Kila unaposafiri ukaenda nchi yoyote iliyoendelea, kitu cha kwanza unachoona ni tofauti ya miundombinu. Ndiyo maana katika mwaka ujao wa fedha kwa makusudi kabisa Serikali imeitengea Wizara hii shilingi bilioni 606 zaidi ya bajeti ya mwaka huu wa fedha tuliyonayo ambayo ni takribani asilimia 12.8 ya ongezeko.

Mheshimiwa Spika, mgawanyiko wa fedha kwenye Wizara hii, umezingatia maoni ya wadau mbalimbali na Waheshimiwa Wabunge na hasa kwamba tujielekeze kama Serikali kwenye ujenzi wa reli mpya ya kisasa ili barabara zetu nazo ziweze kudumu lakini pia ili tuweze kupata manufaa makubwa ya kuwa na hiyo miundombinu ya kisasa.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba nichangie baadhi ya hoja ambazo zilijitokeza. Kwanza tulishauriwa kwamba Serikali katika ujenzi wa reli ya kati iufanye kwa kuzingatia faida za kiuchumi. Napenda nilihakikishie Bunge lako Mheshimiwa Spika na Watanzania kwa ujumla kwamba kazi hii ya kujenga reli imezingatia fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii ambazo zinapatikana katika ukanda mzima wa reli, fursa za kilimo, madini, mifugo na uvuvi pamoja na biashara miongoni mwa mikoa yetu, lakini pia katika nchi jirani.

Mheshimiwa Spika, lilisemwa sana lile la kipande cha Tabora – Kigoma ambacho inajulikana, nami ni mmoja wa wadau wakubwa, nisisitize tu kwamba hili ni muhimu, halina mjadala, lakini kikubwa ni kwamba tunajenga reli hii awamu kwa awamu na changamoto kubwa tuliyonayo ni upatikanaji wa fedha na tunaangalia options zote ikiwemo na kiasi ambacho kinaweza kugharamiwa na Serikali peke yake au kwa kushirikiana na wabia wengine na pia upande wa mikopo. Punde tutakapomaliza upande huu wa financing hakuna mashaka kabisa. Napenda tujenge hata vipande vyote kwa mara moja. Kwa hiyo, hili tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, tuliambiwa pia tuangalie uwezekano wa kupata mkopo wenye gharama nafuu kuharakisha ujenzi wa reli nchini. Niseme tu kama nilivyotangulia kusema kwamba hili tunalifanya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Shirika letu la Reli, wameanza upembuzi yakinifu kwa miradi ya reli ambayo itatekelezwa kwa utaratibu wa PPP na hususan ile ya Mtwara, Mbamba Bay kupitia Mchuchuma na Liganga na pia ile reli yetu ya Tanga - Arusha – Musoma.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa reli ya kati, naomba niliarifu Bunge lako kwamba Serikali iko katika mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Afrika ili watusaidie ku-leverage private sector investment na PPP na nilipokuwa Abidjan nilikuwa na mazungumzo na Dkt. Adesina kwa ajili ya hii na siyo kwa kipande tu cha kuelekea Kigali, lakini kwa vipande vingine vyote ambavyo bado tunatafuta fedha.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na swali kuhusu deni la TAZARA ambalo uhakiki wake umekamilika na kwamba Serikali ilipe hilo deni lililopo upande wa nchi yetu. Tulipokea madai ya TAZARA bilioni 59.6 kwa ajili ya kulipa madeni ya mishahara na michango kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Kama inavyojulikana madeni hayana yanatokana na changamoto mbalimbali ambazo zilikabili TAZARA kuanzia miaka ya 1990 ikiwemo na kushindwa kabisa kujendesha, lakini pia malimbikizo ya wastaafu. Sasa tumefanya nini kama Serikali, kuanzia 2015 tulianza kusaidia ulipaji wa mishahara ya watumishi wa TAZARA na tunalipa takribani shilingi bilioni
1.25 kwa mwezi na tumefanya hivyo hadi Aprili, 2019 na tumekwishalipa jumla ya bilioni 67.44.

Mheshimiwa Spika, lakini mwaka uliopita 2017/2018, tuliongeza pia mtaji wa TAZARA tukalipa bilioni 10 kwa ajili ya kukarabati vichwa na engine za treni za TAZARA. Kuhusu madai ya TAZARA ambayo yamepokelewa karibuni, tunayafanyia uchambuzi wa kina ili tuweze kupata namna bora ya kuyalipa na kuwezesha shirika kujiendesha kwa lengo kudhibiti uzalishaji wa madeni mapya.

Mheshimiwa Spika, tuliambiwa pia hapa kwamba Serikali iharakishe kulipa madeni ya pension kwa wafanyakazi waliokuwa Posta chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kulipunguzia mzigo shirika. Serikali ilikwishafanya malipo kwa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na zoezi maalum la kuwalipa wastaafu lilishafungwa na tulishawaandika hivyo toka Disemba, 2016.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tunashughulikia hoja zinazowasilishwa na wastaafu kwa kulingana na maombi au malalamiko yanayohusika na malalamiko hayo huwa yanawasilishwa kupitia taasisi ambazo walizifanyia kazi hao wastaafu.

Mheshimiwa Spika, kwa wafanyakazi wa Posta wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, maombi ya madai yenye jumla ya shilingi bilioni sita yalikwishapokelewa na tumekwishalipa bilioni 2.7 kufikia Februari, 2017 na kiasi kilichosalia ambapo nyaraka zilikuwa zina utata kiliwasilishwa kwenye Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mwezi Februari, 2019 kwa ajili ya uhakiki malipo yaweze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kwamba mradi wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana bahati mbaya muda umekwisha.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)