Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu pamoja na wakuu wote wanaoongoza taasisi kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu mimi nianze na barabara ya Gairo – Iyogwe ambayo inakwenda mpaka Mkoa wa Tanga kwenye Wilaya ya Kilindi pale kwa ndugu yangu Mheshimiwa Kigua. Nafikiri hii barabara Mheshimiwa Waziri amefika muda si mrefu kama miezi miwili iliyopita na Mheshimiwa Naibu Waziri naye amefika kwenye barabara hii kama miezi mitatu iliyopita na kwa bahati nzuri wakati unafika Mheshimiwa Waziri ulishuhudia pale magari yakiwa yamekwama watu hata kwa miguu wanashindwa kupita, ulijionea kwa macho. Kwa bahati nzuri ukaongea na Eng. Mfugale ukaahidi kwamba patakuwa na madaraja ya temporary angalau barabara hii ipitike lakini katika kitabu changu cha bajeti hapa sijaona matengenezo ya barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ikumbukwe kwamba iko katika ahadi ya Rais ya kuwekwa lami kwa sababu inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Tanga kupitia Wilaya ya Gairo na Wilaya ya Kilindi na ni barabara muhimu sana na wote mnaifahamu. Hata katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi pale Gairo tarehe 26 Juni, 2014 aliitaja sana barabara hii, mpaka leo iko Youtube humu bado sijajua ni kwa nini haipo lakini nafikiri ataangalia namna ya kufanya ili iweze kupitika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ile barabara ya Gairo Mjini ambayo toka mwaka jana ilipewa shilingi bilioni 1.5, mwaka jana ilitolewa shilingi milioni 500 mkandarasi amejenga madaraja lakini mwaka huu mmetoa hela chache kabisa shilingi milioni 120. Kwa hiyo, nina wasiwasi kama kuna mkandarasi atakayekubali kuanza kutengeneza barabara ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea ile barabara pale Gairo Mjini haipitiki tena ya kutoka pale njiapanda ya hospitali mpaka Magoeka kwa sababu TARURA tena hawamo na TANROADS nao hawaishughulikii, sasa haipitiki. Kwa hiyo, naomba hii barabara ya Gairo Mjini iweze kupangiwa pesa ya kutosha ili iweze kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ile barabara ya Gairo – Nongwe. Ukiangalia katika bajeti ya mwaka huu imepangiwa vihela hela vingi vingi sana vidogo vidogo. Kweli lazima nishukuru, mara nyingi imekuwa inapangiwa pesa lakini hakuna hata mara moja imeshawahi kuwekewa changarawe. Kila mwaka tunaitengeneza na mvua za mwanzo tu imeharibika. Pesa zinazopangwa hata nikiangalia hapa ni nyingi zinatosha hata changarawe lakini haijawahi kuwekewa changarawe hata mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri mliangalie hili la barabara ya Gairo – Nongwe kwa sababu pesa mnazozipangia ni nyingi lakini hakuna sehemu iliyowekewa changarawe. Kwa hiyo, hata manyunyu kidogo haipitiki na ile barabara imekaa kama ya Lushoto, unavyoona milima ya Lushoto au zaidi ya milima ya Lushoto ndiyo inakopita barabara hii ya Gairo – Nongwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia minara ya simu, nilikuwa nataka ndugu zangu Mheshimiwa Waziri na Naibu wako Mheshimiwa Nditiye muangalie sana. Minara ya kijiji cha Masenege na Idibo ipo siku nyingi na ni ahadi ya siku nyingi na hata katika vitabu vyenu kila siku ipo. Mnara katika Kata hii ya Idibo, Makao Makuu ya Kata mpaka leo hauna hata dalili ya kujengwa. Tukiweka minara hii ya Gairo pale Idibo, Masenge na Chogoa katika Kata ya Chogoa tutakuwa tumemaliza kabisa shida katika wilaya ya Gairo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka nikizungumzie ni habari ya bandari. Lazima niseme ukweli au nikiri Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa hivi inafanya vizuri sana, wizi wote uliokuwa pale katika Bandari ya Dar es Salaam sasa hivi haupo. Mmoja ambaye alikuwa hatumii Bandari ya Dar es Salaam ni mimi hapa lakini sasa hivi nina mwaka wa tatu natumia Bandari ya Dar es Salaam na huwa naweka mpaka mitego, naweka vitu loose nione kama vitaibiwa lakini iko vizuri sana. Haina wizi na ina speed ya hali ya juu sana na ndiyo maana mnaona sasa hivi inaleta changamoto ya malori. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uzuri wa bandari hii sasa hivi kumekuwa na malori ambayo yamepita kiasi kwenye barabara zetu. Tulizungumza sana na mimi bahati nzuri ni mjumbe wa Kamati kwa muda mrefu katika hii Kamati ya Miundombinu kwamba tuanzishe dry port ya pale Vigwaza ili haya malori yote yawe yanaishia pale. Ukifika pale mzigo wote wa bandari uwe unachukuliwa na ile reli ambayo sasa hivi hata haifanyi kazi ya kwenda Tanga na Arusha, mizigo iletwe mpaka pale Vigwaza, malori yote yaishie pale Vigwaza yasiende mjini. Tumelizungumza sana suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba muangalie malori yamezidi, sasa hivi foleni ya Dar es Salaam sio ya kawaida. Pamoja na kuwa tunatengeneza reli ya standard gauge kuja Dodoma lakini suala hili hata tukitengeneza dry port hapa Ihumwa itasaidia tu mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na Burundi, Rwanda na Uganda. Hata hivyo, bado ile bandari kavu (dry port) ya pale Vigwaza itasaidia sehemu zote za Malawi, Congo, Zambia na sehemu nyingine na cha zaidi ni kuondoa msongamano ambao upo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa TPA walishatoa mpaka pesa zaidi ya USD 2,000,000 kwa ajili ya kutengeneza kichwa cha treni na tulikiona pale Morogoro kwa ajili ya kufanya kazi kama hizi. Je, kile kichwa cha treni kiko wapi? Kwa sababu ukiangalia dry port za Dar es Salaam zinavyochaji usafiri ule tu wa kutoka pale bandarini kwenda kwenye dry port pale Mandela Road au sehemu nyingine ni pesa nyingi kuliko hata kukodisha hiyo treni kutoka mjini mpaka pale Vigwaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana mjitahidi kuhakikisha kwamba ile dry port inaisha. Sisi tulienda kuikagua na ilishaanza kujengwa, tunaomba haraka sana ifanye kazi na malori yote yaishie Vigwaza ili kuondokana na foleni. Maana sasa yanasababisha vifo, mara utasikia kontena limeangukia hiace na limeua watu, mara limefanya nini, tunaombeni sana mtusaidie kwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, mimi si Mbunge wa Wilaya ya Mpwapwa, lakini kwa usafiri nafanya biashara na ndiyo nilikoanzia kwenda katika biashara yangu ya mabasi, kwenda Mpwapwa, Dar es Salaam, jamani huyu mzee Mheshimiwa Lubeleje mtamuua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka na miaka analalamikia habari ya barabara ya Mpwapwa kuja Kongwa, kipande kile kidogo cha lami, kila siku mzee mpaka sasa hivi mzee meno yameng’oka bado anaongea lakini hamtaki kumsikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naombeni sana, kwa uwezo wako Mheshimiwa Mfugale, barabara ya Mpwapwa ni barabara muhimu sana, kulinganisha na barabara zingine za wilaya zingine. Tunaomba jamani kwenye bajeti hii nimeangalia na mzee wangu, lakini hatujaiona hii, na imo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020. Lakini haina dalili yoyote mpaka leo. Tunaomba sana hii barabara ya Mpwapwa, nayo iwemo kwenye mpango huo na ninajua Mheshimiwa Waziri ni Engineer na bahati nzuri na wewe Mpwapwa huwa unakwenda mara nyingi, kwa hiyo, nayo mtaishughulikia, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Naunga mkono hoja, asilimia 100. (Makofi)