Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Mattar Ali Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shaurimoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ahsante kwa kunipa nafasi lakini la pili nikushukuru sana. La tatu niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Maji pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Aweso kwa kazi nzuri wanazozifanya ambazo zinaleta matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ya kuzungumza na la kwanza ni kuhusu miradi ya maji vijijini. Baadhi ya miradi ya maji wanatumia majenereta ambapo ni kuwapa mzigo mkubwa wapiga kura wetu. Niombe sana Serikali iweze kufikiria kutumia solar system kwa sababu upatikanaji wa maji unaweza kuwa rahisi zaidi kuliko kutumia majenereta. Kwa hiyo, nikuombe sana Waziri uweze kwenda mbali zaidi kwenye solar system ili kuwapunguzia mzigo wa gharama wananchi wetu. Unapotumia solar system hata Serikali inaweza ikawa imepunguza mzigo mkubwa katika matumizi ya maji na hili ndilo tunalolitaka kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, fedha za kwenda kwenye miradi ya maji bado ni tatizo kubwa na halijapatiwa ufumbuzi. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri ujue ni miradi gani ni muhimu uikamilishe kuliko kukusanya miradi mingi ambayo haimaliziki. Tunaziumiza fedha za Serikali kisha baadaye ile miradi haifanyi kazi, ina maana hakuna faida ambayo ninyi mnaipata na wananchi hawapati faida kutoka kwa Serikali yao. Kwa hiyo, nikuombe sana, Mheshimiwa Waziri unafanya kazi vizuri lakini kuwe na miradi maalum ambapo kwa fedha ambazo tunaweza tukapata basi tunaweza kuitekeleza na kuisha. Tukifanya jambo hili tunaweza tukafanya kazi nzuri na wananchi wetu wakapata mafanikio mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni shilingi 50 kuongezwa kwenye Mfuko wa Maji. Ninyi Serikali mnaweza mkatafuta chanzo chochote lakini shilingi 50 hii kwenda kwenye Mfuko wa Maji ni jambo la lazima kwa sasa ili tuwasaidie wananchi wetu. Ili tuweze kupata kile ambacho tulichokusudia ni lazima tuongeze shilingi 50, ikiwa ni kwenye mafuta, simu au mahali pengine popote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tumwambie sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha hili suala la shilingi 50 ndiyo mwarobaini wa matatizo ya maji. Ukiangalia mtiririko wote wa fedha basi fedha inayotoka na inayokwenda kwenye miradi ya maji na inayotoka kwenye Mfuko wa Maji tu peke yake, ukiangalia fedha ya Serikali iliyokwenda ni ndogo sana. Ni kwa nini Mheshimiwa Waziri msiweze kuwakubalia Wabunge hawa, ndiyo wananchi, hiki kishilingi 50 kikienda kwenye Mfuko wa Maji tukatatua matatizo ya maji, nia yetu sisi ni safi, tunakushaurini vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui ni kwa nini Mheshimiwa Waziri wa Fedha huwezi kupokea huu ushauri wa Wabunge? Sisi tunakushangaa sana na tunaona mambo ya ajabu sana. Kubaliana na ushauri wa Wabunge, ukikubaliana na ushauri wa Wabunge maana yake umekubaliana na ushauri wa wananachi wote, sisi ndiyo wenye wananchi. Nikueleze tu Mheshimiwa Waziri na Serikali suala la shilingi 50 safari hii halina mbadala. Tunawaomba sana muweze kufanya kazi vizuri. Mkipewa shilingi 50, naamini tatizo la maji tutakuwa tumeliondoa kwa asilimia kubwa kwenye nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nilizungumzie sana, Mamlaka za Maji zinadai sana, Serikali yetu inadaiwa. Ukiangalia tathmini za Mamlaka zote za Maji zinaidai Serikali yetu. Tuombe sana Serikali ikubaliane na kulipa madeni haya ili iwaachie hizi Mamlaka ziweze kujiendesha wao wenyewe, zina uwezo kujiendesha lakini bado madeni makubwa yako Serikalini. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri uweze kulipokea hili na uweze kutoa fedha kuzilipa hizi Mamlaka za Maji ziweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)