Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuongea jioni ya leo, nina mambo machache tu, la kwanza nilichojifunza kwenye hii Wizara ya Maji, kuna matatizo makubwa mawili, tatizo la kwanza ni kutopewa fedha za kutosha kulingana na bajeti yao. Tatizo la pili, hata hizo pesa kidogo wanazopewa bado hawazitumii vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa maana ipi, ukiangalia tunapotembea na Kamati kwenye halmashauri nyingi unakuta miradi mingi ya maji inasuasua, usanifu mbovu sijui pressure ya maji ndogo, DP hazitoi maji, mtu, mfano tumeenda Mkoa wa Kagera zimejengwa DP kumi na saba, lakini tisa hazitoi maji, unajiuliza?. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu si wasomi? Wamesoma wanajua kufanya usanifu kwa nini haya mambo yanatokea? Lakini nilichojifunza ni kwamba watu hawako serious katika kufanya hizi shughuli hata hicho kidogo wanachokipata basi hawakitumii vizuri achilia kwamba nayo Serikali pia haiko serious kutoa pesa za kutosha, ili kuleta maji ya kutosha katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate ufafanuzi kuhusu ile miradi ya vijiji kumi kila wilaya ambayo ilikuwa inafanyika kupitia mikopo ya Benki ya Dunia, miradi mingi haifanyi vizuri, kwa hiyo, nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie kama Tume aliunda imeona nini na inatatua vipi changamoto hii. Kwa sababu kama ni pesa za mkopo tutakuja kuzilipa kwa hiyo tulitarajii watu wafaidike na kuna tabia imezoeleka. Wakijua Kamati inapita, basi maji watayafungua, ama Kiongozi anapita, maji wanayafungua. Kiongozi akiondoka anaondoka na maji yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni tabia mbaya watu wa maji, Wizara ya Maji, hiyo ni tabia mbaya, tunatamani tuone wananchi wetu wanapata maji siku zote, hatutaki mambo ya geresha, kwamba tu kwa sababu leo Rais anakuja basi maji yanatoka. Kwa sababu leo Kamati ya Bunge inakuja basi maji yanatoka. Hilo ni tatizo tumeliona na ninao mfano dhahiri tumeenda kule Karagwe na wakatuambia kwamba haya maji, mmekuja nayo ninyi na mtaondoka nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate ufafanuzi kuhusu mradi wa maji kutoa maji Mto Ruvuma kuleta Mtwara mjini ambao ulikuwa ufaidishe vijiji 26 katika Jimbo la Mtwara Vijijini, naomba tu nipata ufafanuzi kwanza ule mradi bado upo ama haupo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nikisoma katika hiki kitabu cha kwako Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 150 umesema kwamba Serikali itagharamikia imetenga bilioni moja, lakini mwanzoni tuliambiwa ule mradi utatekelezwa kutokana na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China, which is which? Huu mradi bado upo, ama haupo? Na kama haupo ni kwa nini? Na kama upo utatekelezwa lini? Tangu nimeingia Bunge hili Kila nikisimama lazima niuongelee huu mradi lakini umekuwa unasuasua hatujui hatima yetu. Naomba tupatiwe ufafanuzi wa kutosha ili kusudi sisi watu wa Mtwara tujue huu mradi kama upo ama kama haupo mtuambie. Si oleo mnatuzungusha, Benki ya China, kesho Serikali tunataka tujue hatima yake ni nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ukurasa wa 112 kwenye Hotuba ya Waziri, Mamlaka nyingi za maji zinadai Taasisi za Serikali, deni limefika bilioni 21.84 na Mamlaka zile tunajua zinajiendesha zenyewe. Sasa nataka kujua kauli Waziri zile Taasisi za Serikali zinapewa pesa kwa ajili ya kulipia huduma zinazotumia ikiwemo na maji, kwa nini hazilipi kwenye hizi Mamlaka za Maji, na hizi Mamlaka za Maji zinajiendesha zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zina mambo mengi ya kufanya, hizi pesa zinazodaiwa ni nyingi nataka kujua Mkakati wa makusudi kabisa wa kuwaweka hadharani watu hawa ambao hawataki kulipa maji kwa sababu sisi wananchi wa kawaida kwa mfano kule Mtwara, ukishatumia maji, yakafika deni 30,000 wanakuja kukata maji. Kwa nini kwenye hizi Taasisi tunaacha mpaka madeni yanakua, kama Serikali haitoi pesa basi mtuambie, na sio kuzunguka zunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia nipate ufafanuzi ukiangalia ukurasa wa 90 katika hotuba ya Waziri, kuna ule mradi wa maji katika Miji ya Mtwara na Babati, ukisoma pale umeongea tu kwa ujumla kwamba usanifu unaendelea mradi utafanya kazi, usanifu utakapo kamilika. Nataka nijue hili suala liko siku nyingi, linaongelewa ni lini, usanifu unakamilika na lini mradi unaanza kufanya kazi huu mradi katika hii Miji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio mambo ya jumla ya kutuambia kwamba ukikamilika hamna deadline, hamna kipindi maalum umesema umemaliza hilo halikubaliki kabisa, tunaomba tupatiwe kwa sababu tunahitaji huduma hiyo ya maji. Miundombinu yetu pale Mtwara ni chakavu haitoshelezi, kulingana na watu ambao wapo kwa kipindi hiki. Miundombinu ile ni tangu enzi za Mkoloni, kwa hiyo sasa hivi tunapata shida za maji ingawa maji tunayo lakini kwa sababu miundombinu ni mibovu ni michache haiwezi kukidhi haja ya wananchi ambao wapo katika Mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo machache, ukifungua, naomba tu niulize swali moja, ukifungua kwenye hotuba yako ukurasa wa 134, kuna kampeni za maji na usafi wa mazingira chini ya mafungu mengine, lakini ukisoma pale, unakuta fedha zote ni fedha za nje. Sasa tunaenda kufanya kampeni za maji, na usafi wa mazingira, lakini fedha zote tunategemea kutoka nje, maana yake ni nini? Serikali haijatenga fedha za ndani kugharamia hii kampeni. Na tunajua mambo ya maji na usafi wa mazingira ni jambo nyeti, kwa nini Serikali inategemea zaidi pesa kutoka nje. Naomba nipatiwe majibu ya suala hilo. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kengele ya pili imelia.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. (Makofi)