Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Dua William Nkurua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi ya kutoa mchango wangu katika eneo hili la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kutoa ushauri au mchango wowote, nitumie fursa hii kuwashukuru sana viongozi wa nchi, hii hasa Jemedari wetu Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi hasa Waziri wa Maji, Naibu na watendaji wote wa Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kuizungumzia Nanyumbu kwa sababu tuna shida kubwa sana ya maji kwenye Wilaya yetu ya Nanyumbu. Nanyumbu tunaposema hatuna maji tafsiri yake ni kwamba hata maji ya kuokota ni shida. Kuna watu kijiografia tumekaa sehemu mbaya hata maji ya kuokota hayapatikani. Katika vijiji vya Nanyumbu tunapofika mwezi Juni maji yanakuwa ya shida sio ya bomba wala siyo hayo mnayosema maji bora sisi ya kuokota yanakuwa shida, tunapata sana shida ya maji hata ya kuokota, hata oga yetu inakuwa ya shida. Waziri ninapomwambia Nanyumbu kuna shida ajue kwamba hata maji ya kuoga ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali kwa mkakati wake wa kuondoa shida ya maji katika mji wetu wa Mangaka ambapo ndipo Makao Makuu ya Wilaya ya Nanyumbu. Pale Mangaka tuliiomba Serikali itupatie maji kutoka chanzo kikubwa cha maji cha Mto Ruvuma, nashukuru Serikali ilifanya upembuzi yakinifu lakini baada kukamilisha ripoti Serikali ikabaini kwamba gharama ya kutoa maji kutoka Mto Ruvuma mpaka Mangaka ambapo ndiyo Makao Makuu ya Wilaya ni kubwa sana na ikaja na utaratibu wa kuyatoa maji kutoka Mbwinji kuleta Mangaka. Mimi kama Mbunge naishukuru sana Serikali kwa wazo hili zuri na naona jitihada ya Waziri namna ambavyo anakamilisha mchakato huu ili maji yaweze kupatikana pale Mangaka Makao Makuu ya Wilaya ya Nanyumbu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina shida na hilo lakini ombi langu la kwanza. Naomba Mchakato huu uende kwa spidi nzuri Mheshimiwa Waziri, muda hautusubiri, 2020 ni kesho na mimi wananchi wangu walitaka maji. Natamani sana wakati wa kipindi changu maji hayo yaanze kufanyiwa kazi. Mheshimiwa Prof. Mbarawa nakuamini na nina mategemeo makubwa kwamba suala hili utalikamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili kutoka Mbwinji kuja Nanyumbu sheria inasema kilomita 12 kutoka kwenye bomba kuu vijiji vyake vitapata maji. Naomba suala hili lizingatiwe katika kulishughulikia tatizo la maji pale Mangaka kwa sababu tuna vijiji vingi sana kutoka kule mpakani mwa Masasi na Nanyumbu mpaka kufika Mangaka. Kwa hiyo kama sheria itazingatiwa vijiji vingi vya Mangaka, vya Wilaya ya Nanyumbu vitakuwa vimepata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kushukuru hilo ambalo nina matumaini makubwa muda si mrefu mradi utaanza, nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba kuna baadhi ya maeneo, ingawa tuna shida kubwa sana ya maji lakini tumetofautiana kutokana na eneo na eneo. Kuna Kata za Mnanje na Maratani, kata hizi zina shida kubwa sana ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Juni Mheshimiwa Waziri ukija Maratani hutaoga kwa sababu kuna shida kubwa sana ya maji, vyanzo vyote vya maji vinakauka. Pia ukija kwenye Kijiji cha Michiga ni kikubwa sana na kina watu wengi sana lakini hakina maji hasa inapofika mwezi Juni na kuendelea. Kwa hiyo, naomba sana katika mipango ya baadaye na mimi nitakaa na Waziri nitatoa mapendekezo ya maeneo ambayo tunatakiwa tupeleke miradi kwa haraka kabla ya vijiji vingine kutokana umuhimu na shida ya eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji haya yakifika Mangaka tulikuwa na matumaini makubwa sana ya kutoka Mangaka mpaka Masuguru ambako kulikuwa na chanzo cha Mto Ruvuma wangepata maji yale ya kwanza. Kwa mabadiliko haya vijiji hivi ni kama wamekumbwa na butwaa. Nitakaa na wewe tupendekeze namna ya kuweza kushughulika na vijiji hivi ili tuondoe tatizo kubwa la maji katika vijiji hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo la kwanza twendeni tukachimbe mabwawa, tunayaacha maji yanakwenda mtoni na baharini. Bahati nzuri bado maji ya mvua yanapatikana lakini tunashindwa kuyadhibiti ili wananchi wetu waweze kupata haya maji. Kwa hiyo, nashauri sana Serikali iwekeze kwenye uchimbaji wa mabwawa aidha ya umwagiliaji lakini pia ya upatikanaji wa maji ya kunywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Maliasili kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne, Mheshimiwa Maige yupo hapa aliahidi kusaidia maji kwenye Kijiji cha Masuguru na Kijiji cha Chinika aliahidi kutoa shilingi milioni 6. Mpaka leo nashindwa kukaa vizuri hapa Bungeni, wananchi wananikumbusha pesa ile, pesa ile ilitolewa ahadi na Serikali ya Awamu ya Nne. Mimi nataka iende pesa cash, Halmashauri itaongezea tutachimba visima, ahadi hii ni ya Serikali inatutia aibu sana. Serikali ya Awamu ya Nne aliahidi Mheshimiwa Ezekiel Maige na bahati nzuri nilikuwepo pale wakati ahadi inatolewa. Naomba sana unisaidie Mheshimiwa Waziri wa Maji kuikumbusha Wizara ya Maliasili wasisahau deni hilo wananchi wanakumbuka. Kama ninyi mmesahau lakini wananchi hawajasahau. Naomba sana ulitilie mkazo suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa ushauri, kutoka Mto Ruvuma mpaka walau Makao Makuu ya Tarafa ya Nanyumbu, Tarafa yenyewe ya Nanyumbu si mbali sana. Makao Makuu ya Wilaya ya Mangaka tunategemea maji kutoka Mbwinji lakini tuna uwezo pia wa kuanzisha mradi mdogo kutoka Mto Ruvuma mpaka kwenye Kijiji cha Nanyumbu ambako ni Tarafani pia tukaweza kusaidia kutoa maji kusaidia vijiji ambavyo vimezunguka ile Tarafa ya Nanyumbu. Tukifanya hivyo, nina hakika sana Wilaya ya Nanyumbu itakuwa imepata maji ya kutosha na hatimaye kero ya maji itakuwa haipo. Vijiji vingine sisi kama Wilaya tumejipanga namna ya kuweza kusaidia kwa sababu Halmashauri ina mtambo wa kuchimba visima virefu, basi tunaendelea kupunguza baadhi ya vijiji ambavyo vina shida ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, sisi Nanyumbu tuna pesa ya kuchimba mabwawa mawili, moja kwenye Kijiji cha Maratani na lingine kwenye Kijiji cha Namasogo. Taratibu zote kama Nanyumbu tumekamilisha ni ngazi ya Wizara inatuchelewesha na mvua zimeanza kuisha na ni vizuri mabwawa yakachimbwa kipindi ambacho mvua hainyeshi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa hebu nipe matumaini na wananchi wasikie, hizi pesa utazipeleka lini maana mkandarasi ameshapatikana, tunataka tu utoe go-ahead kazi ianze ili wananchi wa Kata ya Maratani na Namasogo wapate maji kama ambavyo Serikali ilikuwa imeahidi kushughulikia tatizo lao la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye ushauri sasa kwa sababu nimeweza kuyapunguza machache yanahusu Nanyumbu. Watu wengi sana wanaongelea hapa kuongeza nguvu ya Mfuko wa Maji. Mheshimiwa Waziri hayo unayokwama nayo hufanyi makusudi, huna fedha, lakini chanzo kikuu ambacho tumekiona hapa ni ile shilingi 50 ya kwanza, Wabunge wanapendekeza tuongeze, kuna ugumu gani Serikali kutusikiliza sisi Wabunge? Sisi tumechaguliwa msituone hivi, tumeaminika. Kama kuna hofu tutawaambia wananchi wetu kwamba hakuna kitu cha bure duniani ni lazima tufunge mikanda. Mimi naomba sana Serikali kubalini mawazo ya Wabunge, twendeni tuongeze shilingi 50 kwenye mafuta ili Mfuko wa Maji utune. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii bajeti iliyopita ya 2018/ 2019 mpaka leo una asilimia 51 tu ya pesa, tunajifunza nini hapo? Ni kwamba uwezo wetu wa kupambana na hii kitu bado ni mdogo lazima tuongeze nguvu. Nitashangaa sana ukija hapa Mheshimiwa Waziri usikubaliane na mawazo yetu, nitakushangaa kweli. Una muda, kaa na wenzako ambao mnakaa nao huko na ambao wana hofu, Wabunge ambao ni wawakilishi tumekubali tutakwenda kuwaeleza wananchi, sisi ndiyo tunakaa nao wale ninyi hofu ya nini? Serikali, sikieni hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vyanzo vingi mbali ya mafuta kuna simu. Mtu mmoja alisema hapa, hivi mtu akiona kwamba umenunua vocha ya Sh.1,000 akaona Sh.20 imeenda kwenye maji wananchi watakasirika, vingapi tunachangia wananchi wasikasirike? Maji ni shida kubwa kwa wananchi wetu tena wanyonge hawa ndiyo zaidi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa, muda wako umeisha. (Makofi)

MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri mawazo yangu yamesikika vizuri, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)