Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu kwanza naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kunipa afya njema. Lakini pia napenda nimpongeze Waziri pamoja na Naibu Waziri niwapongeze pia watendaji wote wa Wizara ya Maji. Pia nipende kuipongeza Serikali kwa kututengea pesa katika bajeti hii nimeona ukurasa 123 tumeweza kutengewa karibu 900,066,000.8. Lakini pia nipende kuishukuru Serikali kwa kuwalipa wakandarasi wetu zaidi ya bilioni 1.7 na sasa hivi tayari wapo kazini naishukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukurani hizo cha ajabu ni kwamba Serikali ilitutengea mradi huu mkubwa wa kutoka Nyamtukuza kwenda Bukwimba mradi huu ulitengewa zaidi ya bilioni 15. Mpaka sasa hivi zimeshatoka takribani bilioni nane lakini cha ajabu kazi inavyoenda mpaka sasa hivi ninavyoongea hakuna hata tone moja ambalo linatoka la maji na mradi huu unagusa vijiji vinane, vijiji hivi ikiwa ni kutoka kule Nyamtukuza kwenye chanzo cha maji, panaitwa Nyamtukuza kupita Kakola, Kitongo, Ikangala, Kalumwa, Izunya, Kayenze na Bukwimba lakini mpaka leo hii hata tone moja la maji halijatoka,.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali pamoja na kutoa fedha zaidi ya bilioni nane ebu jaribuni kufuatilia mkaangalie huu mradi, huu mradi tangu mwaka 2010 naupigia kelele tangu 2010 mpaka leo hii mradi huu haujatoa hata maji kidogo. Bahati nzuri hata Mheshimiwa Mbalawa kipindi kile alikuwa Waziri wa Maji nimeenda naye mpaka kwenye chanzo cha maji. Waziri Mkuu amefika kule kwenye chanzo cha maji, eeh! Ndiyo kipindi kile alichokuwa waziri maji tumeshawahi kwenda naye, Mheshimiwa Eng. Kamwele tumekwenda naye mpaka kule na baadhi ya viongozi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha ajabu kuna mdudu gani ambaye anasababisha maji yasitoke nakuomba Mheshimiwa Waziri kwenye Bunge hili kabla ya kuhisha twende pamoja ukaone tatizo ni nini kwa sababu wananchi wa Nyangwale wanashida kubwa sana ya maji, mradi huu bilioni nane hata tone la maji halijatoa kwanini. Kwa hiyo, naungana kabisa na Wabunge wenzangu kwamba ufuatiliaji unakuwa ni mdogo, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba utakapokuja hapa uniambie ni lini mimi na wewe tuondoke twende tukaangalie huu mradi tatizo ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia niipongeze Serikali kwa mradi wa pamoja na Bulyang’ulu Acacia mradi huu ambao umegharimu takribani bilioni 13 naishukuru sana Serikali kwamba tayari imeshatenga fedha na wakandarasi wapo kazini mradi huu unatoka kwenye bomba kuu linalokwenda Kahama kwenda Irugi. Nimepata takribani vijiji saba ambavyo vitapitiwa na mradi huo kwa kweli naipongeza Serikali mradi huo utakapokamilika basi baadhi ya vijiji hivyo saba ambavyo nimevitaja vinaweza kupata maji, ambavyo ni vijiji vya Iyugwa, Tarumwa, Mwamakiriga, Izunya, Kavita pamoja na Lushimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia hili suala kwa uchungu sana ni kwanini kwa sababu kila ninaposimama miaka yote nazungumzia huu mradi wa Nyamtukuza, leo nazungumza taratibu sana mnielewe, sitaki kuzungumza kwa kasi na kwa haraka nizungumze taratibu mnisikilize vizuri, naomba Waziri twende pamoja tukaangalie mradi huu nini ambacho kinakwamisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nimeona kwenye kitabu chako Serikali kwamba Serikali ya Oman na Serikali ya Tanzania wamekubaliana kuchimba visima mia moja, katika visima hivi ambavyo vitachimbwa kwenye shule za msingi na sekondari na Wilaya ya Nyang’hwale naomba basi niangaliwe angalau sekondari nne ambazo zinashida sana maji kama vile Nyang’hwale sekondari, Msalala Sekondari, Bukwimba Sekondari, Mwingiro Sekondari naomba angalau nipate visima vinne hivi ambavyo tunachangiwa na Serikali ya Oman. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna bwawa moja kubwa sana ambalo lipokule Kata ya Shabaka kijiji cha Nyamgongwa, bwawa lile lilikuwa kubwa sana na lilikuwa linanufaisha zaidi ya kata tano bwawa limeshaaribika takribani miaka thelathini na tano miundombinu yake imearibika lakini manufaa makubwa yalikuwa yanapatikana kwenye lile bwawa. Wananchi wengi walikuwa wakilima bustani walikuwa wakivua samaki, walikuwa wakilima kwa kumwagilia na manufaa mengine mbalimbali yalikuwa yanapatikana kwenye hilo bwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa ninaomba basi itengwe pesa kwa ajili ya kwenda kulitengenezea miundombinu bwawa lile liweze kuwasaidia wananchi, wananchi waweze kupata maji na kujipatia mapato, lakini pia mifugo kuweza kupata maji. Kwa hiyo, naomba katika bajeti hii angalau itengwe hiyo pesa kwa ajili ya hilo bwawa la Shabaka kijiji kimoja kinaitwa Nyamgongwa ambako amezaliwa ndugu yetu nimemsikia yuko hapa anaitwa Luhemeja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia baada ya kuyasema haya kuna kisima kirefu ambacho kimechimbwa katika Kata ya Nyangwale, Kijiji cha Nyang’hwale kisima kina miaka kumi na moja, miundombinu pale ilishakamilika Jengo lipo pump ipo, lakini cha ajabu maji mpaka sasa hivi hajaanza kusukumwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejaribu sana kufuatilia halmashauri wanasema wao hawana fedha kuna upungufu kidogo. Nilikuwa naiomba Serikali ikaiuangalie huo mradi ukamilishwe ili huo mradi uweze kusaidi kupunguza tatizo la maji katika Kata ya Nyang’hwale lakini pia vijiji vingine ambavyo vipo pale jirani kwa sababu ni kisima kirefu na kinamaji mengi sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri mchango wangu ni huo hauna maneno mengi kikubwa nakuomba tu ukautembelee mradi wangu wa Nyang’hwale ili uweze ku- pump hiyo hela na kuangalia tatizo nini ili sasa na mimi wananchi wangu waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)