Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia namshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini na kuniteua katika nafasi hii. Nampongeza kwa kazi kubwa anayofanya katika kuwaletea Watanzania maendeleo. Vilevile sina budi kumshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa ushauri na maelekezo yao muhimu katika utendaji kazi wangu wa kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru pia Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge ukiwemo wewe mwenyewe kwa kuliongoza Bunge hili kwa hekima, busara na weledi mkubwa. Naishukuru pia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa ushirikiano mkubwa wanaotupatia. Hii ni moja kati ya Kamati bora sana ambayo Wajumbe wake wanauelewa mpana wa sekta ya elimu na hivyo kuendelea kutoa ushauri muhimu katika kuboresha elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Prof. Joyce Lazaro Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa uongozi wake thabiti ndani ya Wizara. Pia nawashukuru Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa Wizara kila mmoja kwa nafasi yake kwa ushirikiano wanaonipatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo kwa umuhimu, naishukuru familia yangu kwa upendo na ushirikiano mkubwa wanaonipatia katika utekelezaji wa majukumu yangu. Pia nawashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Ngorongoro kwa imani yao yangu kwangu na ushirikiano ambao wananipa ambao umetusaidia Jimbo letu kupiga hatua kubwa sana ya maendeleo katika kipindi kifupi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, sasa naomba kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja ambazo zimechangiwa na Waheshimiwa Wabunge. Kwa sababu ya muda hatutaweza kujibu kila hoja zingine tutazileta kwa maandishi, lakini naomba nijielekeze katika hoja chache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamependekeza Serikali kuweka utaratibu wa ada elekezi katika shule binafsi. Ni muhimu ikafahamika kuwa shule za binafsi zinatoa huduma lakini pia zinafanya biashara. Hivyo, ni vigumu kwa Serikali kutoa ada elekezi na badala yake itaendelea kuacha nguvu ya soko iamue kama ilivyo katika sekta nyingine ikiwemo afya. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia utoaji wa elimu katika sekta ya umma na binafsi ili kuimarisha utoaji wa elimu na elimu iwe bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia juu ya umuhimu wa kuimarisha Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule. Wizara yangu inatambua umuhimu wa Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule katika kuboresha utoaji elimu bora nchini. Katika kuimarisha Idara hiyo, Wizara kwa mwaka 2018/2019, ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya ukaguzi wa shule na hadi kufikia Machi 2019, Idara ishapokea kiasi cha shilingi bilioni 1.8 sawa na asilimia 51.30. Kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4.1 kwa ajili ya ukaguzi wa shule na pia Wizara inajenga ofisi 100 za Udhibiti Ubora wa Shule katika Wilaya 100 na inakarabati ofisi 40 za Udhibiti Ubora wa Shule katika Wilaya 40. Vilevile Wizara imenunua computer 353 na printer 153 kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa Ofisi za Wilaya za Kanda ambazo hazikuwa na vitendea kazi. Aidha, Wizara ishapeleka magari 45 katika Wilaya 45 ili kuhakikisha kwamba shule nyingi zinafikiwa na kufanyiwa tathimini kwa lengo la kuboresha utoaji wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maslahi ya Wadhibiti Ubora wa Shule na kuboresha mishahara yao, Wizara imepokea michango ya Waheshimiwa Wabunge tena kwa uzito mkubwa na itafanyia kazi ili kuwapa motisha ya kazi Wadhibiti Ubora wa Shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia sana kuhusiana na masuala ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Badhi ya Waheshimiwa Wabunge wamechangia juu ya umuhimu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kushirikiana na NIDA kubaini wanafunzi wanaostahili kupewa mikopo lakini pia kurejesha baada ya kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii imeanza kufanyiwa kazi, ambapo Bodi ya Mikopo imekutana na NIDA Februari, 2019 kwa lengo la kuweka utaratibu wa kubadilishana taarifa za kimfumo na kuwa na mifumo ya taasisi bora zaidi ya kufanya kazi kwa ufanisi kwa kuunganisha na mifumo ya taasisi zingine zinazotoa huduma kwa wananchi. Aidha, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imeendelea kufanya mazungumzo kama hayo na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa lengo la kuwa na mifumo inayoendana kubadilishana taarifa ili kuongeza ufanisi katika upangaji na urejeshaji wa mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Wabunge pia wameshauri Bodi ya Mikopo ifanye malipo ya fedha za mikopo kupitia akaunti za benki za wanafunzi moja kwa moja ili kuondokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza. Ushauri huu ulishaanza kutekelezwa kwa majaribio ambapo katika awamu ya kwanza mwaka 2017/2018 jumla ya wanafunzi 37,184 kati ya wanafunzi 123,285 sawa na asilimia 30 wanaopata mikopo waliunganishwa katika mfumo wa kielekitroniki wa malipo unaofahamika kama Digital Disbursement Solution. Wanafunzi wengine waliobaki wataunganishwa katika awamu inayofuata, katika mwaka unaokuja wa fedha. Utaratibu huu tunaamini utaongeza ufanisi na kuondoa kero kwa wanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge pia ambao wamechangia hotuba yetu wamechangia kuhusu baadhi ya wanafunzi wasio na uwezo kukosa mikopo ya elimu ya juu. Napenda ifahamike kwamba mikopo hutolewa kwa wanafunzi wote wenye uhitaji na huongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Sura 178 inayotaja vigezo vikuu ambavyo ni pamoja na kuwa Mtanzania kwa maana mwombaji lazima awe raia, lazima awe amepata udahili, asiwe na chanzo kingine cha kugharimia masomo yake, pia awe ameomba mikopo kwa usahihi. Aidha, kipaumbele cha mikopo kuzingatia makundi maalumu yaani yatima, wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu walifadhiliwa katika masomo yao ya sekondari au stashahada ambao katika maombi yao wamethibitisha taarifa hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kumekuwa na changamoto katika uwasilishwaji wa taarifa kwa waombaji. Kwa mfano, katika mwaka 2018/2019 wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 16,797 kati ya wanafunzi 81,425 waliwasilisha maombi yenye dosari mbalimbali. Wito wetu kwa wanafunzi na kila mmoja wetu ni kuhakikisha kwamba wakati wa kuomba mikopo kila mmoja achukue muda wake vizuri ajaze zile fomu vizuri kwa sababu ukikosea kuomba inakuwa ni vigumu wewe kupata ule mkopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondoa athari za changamoto hii, katika mwaka 2018/2019 Bodi ya Mikopo imeendelea kutekeleza programu za elimu ya uombaji mikopo kwa wanafunzi wa sekondari Tanzania Bara na Zanzibar. Kati ya mwezi Februari na Aprili, 2019, Bodi imeendesha programu hizi katika shule mbalimbali za sekondari 49 na kuelimisha wanafunzi wapatao 25,000 kati ya wanafunzi 81,300 wanaotarajiwa kufanya mtihani ya kidato cha sita mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Bodi iliwafuata wanafunzi 25,000 wanaotegemea kumaliza kidato cha sita katika shule wanazosoma kutoa elimu ya namna ya kujaza fomu. Tunategemea mwaka huu hatutakuwa na changamoto kubwa ya waombaji wengi kukosea kujaza fomu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia juu ya umuhimu wa kutoa mikopo kwa asilimia 100 kwa wanafunzi wa sayansi hasa wale wanaomba kusomea udaktari na ualimu. Mikopo ya elimu ya juu hutolewa kwa kuzingatia sheria ambayo imepishwa na Bunge hili. Masomo ya sayansi, udaktari na ualimu ni sehemu tu ya vigezo vingi vya utoaji mikopo. Vigezo hivyo ni pamoja na uhitaji wa waombaji wanaotoka katika makundi yale ambayo tumesema yatima, wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu waliofadhiliwa katika masomo ya sekondari na wanaotoka katika kaya zenye vipato duni. Hivyo, waombaji wote ambao ni wahitaji na ambao wamepata udahili katika programu za kipaumbele ikiwemo masomo ya sayansi hasa udaktari kupewa kipaumbele katika kupangiwa mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, upangaji wa mikopo hutegemea idadi ya wanafunzi wanaopata udahili na uhitaji. Kwa kuzingatia hilo, katika mwaka wa fedha 2018/2019, wanafunzi 2,118 wanaosomea programu ya sayansi ya afya walipangiwa mikopo ambayo ni asilimia 5 ya wanafunzi wote waliopangiwa mikopo. Kati yao, wasichana walikuwa 636 sawa na asilimia 30 na hao walipangiwa mikopo katika programu hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamependekeza kwamba tutoe kipaumbele cha kipekee kwa wanafunzi wanaopata madaraja ya kwanza na ya pili wakati wa kutoa mikopo. Serikali imeendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye uhitaji kwa kuzingatia vigezo vya upatikanaji wa fedha. Kulingana na vigezo vilivyowekwa, siyo wanafunzi wote wanaopata udahili wanakuwa na sifa za kupata mikopo ya elimu ya juu. Mikopo inayotolewa na Serikali huongozwa na Sheria na Sera ya Uchangiaji wa Huduma za Kijamii ikiwepo elimu. Aidha, utoaji wa elimu hiyo huongozwa na Sheria ya Mikopo, Sura ya 178 inayolenga Watanzania wahitaji na wenye udahili lakini wasio na uwezo wa kumudu gharama au sehemu ya gharama za mafunzo ya elimu juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge vilevile wamezungumzia kuhusu umuhimu wa kutoa elimu. Kama nilivyosema, tayari elimu hiyo ya namna ya kujaza fomu zile imeshatolewa mwaka huu kwa wanafunzi 25,000 ambao tunategemea wataomba mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imechangia kwa hisia kubwa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge ni suala la wanafunzi kutoruhusiwa kufanya siasa vyuoni. Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 345 ya mwaka 2005 (Toleo la 2002 la Sheria za Tanzania) pamoja na Kanuni za Sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2013, kifungu cha 51(1)(2) inakataza wanafunzi kujiingiza katika siasa za vyama wawapo vyuoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kuzuia wanafunzi kujiingiza katika vyama vya siasa ni kujenga mazingira tulivu kwa wanafunzi kujisomea na kumaliza masomo yao ndani ya muda uliopangwa. Lazima tuseme, lengo ni zuri tunataka wanafunzi wetu waweze kufanya kile ambacho walikifuata vyuoni na ni kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, haimaanishi kwamba hawaruhusiwi kufanya siasa ya aina yoyote, siasa inayokatazwa ni siasa ya vyama vya siasa ndani ya vyuo, wanaweza wakaendelea kuwa ni wanachama wa vyama vya siasa, wakaenda kufanya siasa hiyo nje lakini ndani ya vyuo wanaruhusiwa kufanya siasa za wanafunzi (student politics) na ndiyo maana wana Serikali zao, wanafanya chaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile uongozi wa vyuo ni lazima wawajibike kuhakikisha kuwa chaguzi za wanafunzi zinafanyika kwa kufuata demokrasia lakini siyo kwenda kukwaza au kuingilia chaguzi zile. Kwa hiyo, tunachosema kimsingi ni kwamba siasa wanaweza wakafanya kama students politics lakini siyo siasa za vyama ndani ya vyuo kwa sababu inaingilia masomo na inavuruga utulivu.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imezungumziwa kwa hisia kubwa sana ni suala la ni namna gani nchi yetu imejitayarisha kuelekea katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (The Fourth Industrial Revolution). Serikali inatambua uhusiano kati ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda na Tanzania ya Viwanda ambayo tunajaribu kujenga huku tukitaka kuelekea kwenye uchumi wa kati. Mapinduzi ya Viwanda ya Awamu ya Nne ni mageuzi makubwa ya nne toka mapinduzi yale maarufu kama Mapinduzi ya Kwanza ya Viwanda yaliyotokea karne ya 18 (Industrial Revolution).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapinduzi hayo yanajumuisha muunganiko wa teknolojia mbalimbali ambapo mifumo yote inaunganishwa ki-digital ikihusisha sayansi na teknolojia ya hali ya juu ambayo ni ukusanyaji, utunzaji na uchakataji wa takwimu na uimarishaji wa mifumo ya mawasiliano. Mipango ambayo tayari imeshaanza ndani ya nchi yetu kwa kweli ni mingi katika kujaribu kuelekea katika The Fourth Industrial Revolution.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya mipango hiyo ni upatikanaji wa computer kubwa zenye uwezo wa kuchakata kwa kasi taarifa za maendeleo ya jamii (supercomputing) katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salam vilevile Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela. Pia upatikanaji wa mitaala ya kufundishia masuala ya TEHAMA, big data katika Vyuo vya DIT na Nelson Mandela. Upatikanaji wa maabara za mashine za kisasa za viwandani yaani mechatronics labs kwa ajili ya kuendeleza wataalam wa viwandani na kuboresha mafunzo ya ufundi kwa wanafunzi katika Taasisi za DIT na MUST. Pia taasisi mbalimbali za sayansi na teknolojia kupitia utaratibu wa COSTECH zimeanza kujikita katika kufanya tafiti zinazojibu mahitaji ya Mapinduzi ya Viwanda Awamu ya Nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vyetu vingi vimeshaandaa mitaala mbalimbali inayojibu mahitaji ya sayansi na tekonolojia. Mfano, Chuo Kikuu cha Nelson Mandela tayari wamerekebisha mitaala ili waanzishe Digrii ya Umahiri katika Mifumo Bebwa na Jongevu (Master of Science in Embedded and Mobile Systems). Pia wanaanza kufundisha Digrii ya Umahiri katika Mifumo ya Habari na Usalama Mtandaoni (Masters in Information System and Network Security. Vilevile Digrii ya Umahiri katika Mawasiliano ya Pasiwaya na Jongevu (Masters in Wireless and Mobile Communication).

Mheshimiwa Mwenyekiti, DIT wao wanajitayarisha kufundisha Digrii ya Umahiri ya Uhandisi wa Sayansi ya Komputa (Masters of Computer Science Engineering). Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo wao wamejitayarisha kufundisha Masters of Science in Health Molecular Biology yaani Digrii ya Umahiri ya Sayansi katika Biolojia ya Molekiuli ya Afya Jumuishi. Pia Digrii ya Umahiri ya Sayansi katika Uzazi wa Wanyama na Bioteknolojia. Vilevile Digrii ya Awali ya Bioteknolojia ya Sayansi ya Maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo Kikuu cha Teknojia Mbeya wao wamejiimarisha na wataanza kutoa Digrii ya Awali ya Sayansi katika Uhandisi wa Akili Bandia. Pia Digrii ya Awali ya Sayansi katika Sayansi Data lakini vilevile Digrii ya Awali ya Uhandisi Baitiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo Kikuu Cha UDOM wao wamejitayarisha kufundisha Digrii ya Awali ya Sayansi katika Uhandisi wa Akili Bandia. Pia Digrii ya Awali ya Sayansi katika Uhandisi wa Sayansi Data. Vilevile Digrii ya Awali ya Sayansi katika Uhandisi wa Internet Vifaa na Digrii ya Awali ya Sayansi katika Uhandisi na Usalama Mtandaoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana haifahamiki sana huko nje kwa sababu haizunguzwi lakini nchi yetu na vyuo vyetu vimejikitika katika kuanza kuingia katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ili iweze na sisi kutusukuma na tuweze kuingia katika ushindani katika dunia ambayo tunaishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vikuu pia hufanya utafiti katika maeneo mbalimbali ambayo ni muhimu kwa ajili ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda. Kwa mfano, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam imeingia mkataba na kushirikiana na kampuni ya Belfrics ya nchi Malaysia ili kuwajengea uwezo wataalam wa Kitanzania katika eneo la blockchain technology ambayo ni teknolijia ya uhifadhi wa taarifa na takwimu za ki-digital kwenye sayansi ya computer ambayo huongeza ufanisi katika TEHAMA. Kwa ujumla vyuo vitaendelea kubuni mitaala mipya na kupitia iliyopo ili kukudhi mahitaji ya sasa ya sayansi na teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kupitia Mradi wa Kukuza Ujuzi, Tume ya Vyuo Vikuu imeshatoa mafunzo kwa Makamu Wakuu wa Vyuo 40 kuhusu jinsi ya kusimamia mafunzo na uanzishaji mitaala inayoendana na mahitaji ya kuanzisha mashirikiano kwenye masuala ya viwanda. Kupitia mradi huu, TCU imeshafanya mafunzo ya jinsi ya kutengeneza mitaala inayoendana na soko na tunategemea wanataaluma angalau 132 wataendelea kunufaika na mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, naomba kuunga mkono hoja.