Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu bila kumsahau Mkurugenzi wa TEA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vya VETA ni mkombozi wa vijana wetu hususan wale waliomaliza darasa la saba na kidato cha nne ambao hawakubahatika kuendelea na masomo. Nchi yetu ina Halmashauri 185, ni muhimu Halmashauri zote nchini ziwe na vyuo hivi ili basi vijana wetu wapate elimu itakayowasaidia kujiajiri na kupunguza vijana wetu kujiingiza kwenye vishawishi vya kuingia kwenye wizi na vitendo visivyokuwa na maadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, nashauri Wizara iweke mpango mkakati wa kuanzisha vyuo katika Halmashauri zote nchini. Kwa kuanzia naomba Wizara itoe kipaumbele kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, kwani tunayo misitu mingi inayoweza kuwasaidia vijana kuvuna mbao na kutengeneza samani mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri Serikali kuangalia namna ya kusaidia Halmashauri mpya kupata vyombo vya usafiri. Halmashauri ya Uvinza haina gari na tunazo shule 122 za msingi, 119 zimesajiliwa na shule tatu (3) ziko kwenye hatua za kusajiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kutokuwa na gari kunasababisha wakaguzi kushindwa kutimiza majukumu yao ya ukaguzi wa shule na ukaguzi wa ubora wa elimu inayotolewa. Niendelee kumuomba Mheshimiwa Waziri, dada yangu mpendwa Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako kutupatia gari angalau tatu; moja ya Ukaguzi na gari mbili, DEO Msingi na DEO Sekondari. Jiografia ya Jimbo la Uvinza ni ngumu sana tena sana na hivyo kusababisha watumishi wa idara hizi kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya watu wazima, ukurasa wa 15. Naishauri Serikali kuanzisha vituo hivi kwenye kila Kata ikiwezekana huku baadaye kila kijiji ili elimu hii ya watu wazima iwe mkombozi kwa wote wale wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya sekondari, kwanza nitoe shukrani zangu kwa Mheshimiwa Waziri kwa namna alivyosikia kilio cha wananchi wa kata zangu mbili, Kata za Basanza na Mwakizega. Shule hizi zilizojengwa kwa nguvu ya wananchi na Mfuko wa Jimbo sasa zimesajiliwa, nasema ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, ninazo shule mbili za Kata ya Sigunga, Ukanda wa Ziwa Tanganyika na Shule Kata ya Nguruka. Shule hizi mbili zimeshajengwa madarasa sita, vyoo na darasa moja kama jengo la utawala kwa kuanzia. Namuomba Mheshimiwa Waziri aone namna ya kutusaidia kuzisajili shule hizi kwani hadi leo hii tunao wanafunzi 250 Kata ya Nguruka hawajapata nafasi na wengine 780 wameachwa kwenye shule mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Wilaya yangu ya Uvinza. Nimuombe Mheshimiwa Waziri atusaidie fedha kwa ajili ya kusaidia shule hizi mbili za Nguruka Sekondari na Sekondari ya Sigunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kidato cha sita, tunayo Shule ya Lugufu Boys na Girls. Shule hizi zilianzishwa kwenye majengo ya wakimbizi. Miundombinu yake ni chakavu sana na ina mazingira ambayo siyo rafiki, hakuna maji wala umeme. Tuiombe Wizara kuona namna ya kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo sambamba na kuwapatia visima ili wapate maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo shule ya walemavu Kata ya Uvinza. Shule hii ni ya msingi, mazingira yake siyo rafiki kabisa, tunaomba msaada kwa ajili ya watoto hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maslahi ya walimu. Hali ya makazi ya nyumba za walimu ni tete, shule nyingi za msingi, sekondari hakuna nyumba na zile ambazo zina nyumba basi ni chakavu hata vyoo hakuna. Tuiombe Serikali kutuletea fedha za ujenzi wa nyumba za walimu pamoja na matundu ya vyoo kwenye shule za msingi na sekondari kwa wanafunzi na walimu, hali ni tete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwa kuzungumzia maslahi ya walimu wa shule za msingi na sekondari. Walimu wangu wengi wanayo madai mengi wanadai na hawalipwi. Niombe Wizara ya Elimu pamoja na Wizara ya TAMISEMI ione namna ya kuwalipa walimu wanaodai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto ya walimu wapya kucheleweshewa kulipwa posho zao za kujikimu kwa mujibu wa sheria pamoja na kuwekwa hadi miezi sita bila kupata posho wala mishahara. Tutoe rai kwa Serikali kujipanga kwani wanatambua fika ni lini watawaajiri walimu. Kwa nini pindi wakitoa tangazo la ajira wasipange na fedha zao kwenye Halmashauri zote nchini ili ajira zinapotoka na fedha ziwe tayari kwenye Halmashauri za Wilaya ili kupunguza usumbufu wanaopata walimu wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira za walimu. Hivi karibuni tumeona tangazo la ajira za walimu na tumesikia walioomba ni zaidi ya 80,000. Ombi langu katika hili, Wizara itupe Halmashauri ambazo zina upungufu mkubwa wa walimu kama vile Halmashauri yangu ya Uvinza. Sambamba na hayo, niombe pia Waziri aje kutembelea Jimboni ili apate muda wa kusikiliza matatizo ya walimu wangu wa Jimbo la Kigoma Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo ya elimu ya juu. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aangalie Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kwani wanafunzi wengi wanayo malalamiko makubwa ya kukoswa mikopo hasa watoto wa watu maskini. Nimuombe Waziri atupie macho Bodi hii waache kuwaonea watoto wa maskini hasa wanaotoka vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia hayo, niendelee kumpongeza Waziri na timu yake yote kwa namna wanamsaidia Mheshimiwa Rais kutelekeza Ilani ya CCM kutoa elimu bure sambamba na kuiendeleza elimu Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba kuunga mkono hoja.