Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na uzima na kuweza kuchangia katika Wizara hii kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri mama yangu Mheshimiwa Prof. Ndalichako kwa jitihada ambazo amekuwa akizifanya katika kuboresha suala la elimu Tanzania. Pamoja na jitihada zinazofanywa na Wizara bado kuna changamoto nyingi katika suala la elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Asilimia 90 ya wanaoomba mkopo wazazi wao hawana uwezo lakini pamoja na Serikali kuboresha huduma hii, bado kuna changamoto kwani wapo wanafunzi ambao wana vigezo kabisa vya kupata mkopo lakini hawajapata. Naomba sana Wizara ihakikishe wanafunzi wote wanapata mkopo na kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasema inasaidia wanafunzi wasio na uwezo kupata mkopo, sawa tunashukuru sana kwa jambo hili jema linalofanya na Serikali yetu lakini kwa nini Serikali iwasaidie wanafunzi hawa kwa riba? Leo Serikali inampa mwanafunzi mkopo Sh.7,000,000, lakini anakuja kulipa Sh.12,000,000. Sasa huu ni msaada kweli ukizingatia anamaliza chuo anaanza kazi mshahara ni mdogo na hata kupata hiyo kazi ni shida. Kwa nini mwanafunzi asilipe kile ambacho Serikali imempa? Kama digrii amesoma miaka mitatu kwa Sh.8,000,000 basi akianza kulipa alipe hiyo hiyo na siyo Sh.13,000,000 au Sh.14,000,000. Hii sidhani kama ni sawa na kiukweli inaumiza sana. Naomba mtu alipe alichokopeshwa na siyo na riba tena kubwa inakuwa kama umekopa benki, hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala upungufu wa walimu hasa masomo ya sayansi. Shule zetu nyingi hazina walimu wa kutosha wa sayansi. Sasa kama kweli tunaenda katika nchi ya viwanda ni lazima tuwekeze katika suala la sayansi katika shule zetu. Niombe sana zijengwe maabara za kutosha ili wanafunzi wetu waweze kufanya mafunzo kwa vitendo, hii itawasaidia sana kwani sayansi ni vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu kwenye shule zetu kiukweli kuna changamoto kubwa kwani maeneo mengi hakuna madarasa ya kutosha. Katika Mkoa wangu wa Kigoma hakuna madarasa ya kutosha kwani kuna shule wanafunzi wanakaa chini. Vilevile shule nyingi hakuna vyoo bora yaani hali ni mbaya sana, watoto wana mazingira magumu sana. Unakuta watoto wanajisaidia hovyo na kupelekea mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu. Pia kuna watu wenye ulemavu wanaotambaa chini sasa angalia hali ya choo ilivyo chafu na hakuna maji hawa wanafunzi wanakuwa katika hali gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba bora kwa walimu. Walimu ni muhimu sana, tuwe wakweli wote tumefika hapa kwa msaada wa walimu. Walimu wanafanya kazi kubwa sana lakini wanaishi katika mazingira magumu sana. Wengi hawana nyumba za kuishi na hata zilizopo zina hali mbaya sana kwani hakuna maji wala vyoo bora. Naomba Serikali iwaangalie walimu Tanzania nzima kwa jicho la pili wapatie nyumba bora za kuishi. Hii itasaidia kuongeza morale ya utendaji kazi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la kupanda madaraja kwa walimu na stahiki zao za likizo na matibabu. Bado kuna changamoto kwani walimu wanapanda madaraja lakini mshahara haupandi, anapanda daraja toka A kwenda B, lakini anaendelea kulipwa mshahara wa daraja A. Hali hii imepelekea mpaka leo kuna wastaafu wamestaafu lakini wamepunjwa mafao yao kwa kufanyiwa kikokotoo kwa mshahara wa daraja A wakati alipanda daraja miaka mingi na amestaafia daraja jipya. Jambo hili si haki kabisa, huyu mtu ametumikia Serikali kwa moyo wote kwa nini anyimwe haki yake? Ahsante.