Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuchangia hoja hii naomba kutoa shukrani kwa matumaini yanayoanza kuonekana kwa kwanza, kukarabatiwa kwa FDC ya Tarime. Hiki chuo kinasaidia wanafunzi toka Tarime, Rorya na hata baadhi ya kata za mpakani za Serengeti, hivyo ni bora kile chuo kingefanywa kuwa chuo cha VETA. Pia napenda kushauri baada ya ukarabati basi viweze kupatiwa vifaa vya kisasa vya kujifunzia, karakana ya kisasa na vifaa vingine. Hii itaongeza ufanisi kwenye utoaji wa mafunzo kwa wanafunzi wetu na wakufunzi kwa ujumla. Vyuo hivi vya Maendeleo ya Wananchi vikitoa mafunzo yenye tija vitasaidia sana kutoa vijana watakaosaidia katika soko la ajira na huduma kwa Taifa letu kwani wengi watajiajiri na kuajiri Watanzania wengi. Ikumbukwe huchukuliwa vijana waliokosa udahili wa form one na wale ambao wanakosa udahili wa form five. Ikizingatiwa changamoto za nafasi hizo sanjari na ufaulu wa wanafunzi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kujua status ya ukarabati wa Shule ya Sekondari ya Tarime ambayo ni ya kidato cha tano na cha sita tu na ina mikondo mingi sana. Kwa kweli, ni shule ya tangu mwaka 1970, hivyo inahitaji kukarabatiwa na kuwa na hadhi ya aina yake maana shule za hivi ni chache sana Tanzania na lazima tuweke mazingira mazuri kwa wanafunzi ya kujifunzia. Pia, shule hii haina gari la dharura, mfano, mtoto akiugua. Tulikuwa na gari aina ya Land Cruiser, lakini lilichukuliwa kwa mazingira ya kutatanisha na hadi leo halijarudishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alitembelea jimboni kwangu na kuahidi kutupatia fedha kwa ajili ya kujenga shule ya bweni kwa watoto wa kike. Tayari tuna eneo kwenye kata mbili, ningependa kujua kama mwaka huu wa fedha tumetengewa fedha za kuanza ujenzi na ni kiasi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tuna shule mbili za kata ambazo zipo tayari na miundombinu ya kuwa high school mchanganyiko. Tumeomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ambayo ni shule ya Mogabini na ile ya Nyandoto. Je, lini tutapata hizo fedha, tumeshuhudia Halmashauri nyingine zinapata na sisi Halmashauri ya Mji tunakosa, ilhali tuna mapato ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika kusimamia elimu ya msingi na sekondari lazima tuboreshe mazingira ya kujifunzia kama vile madawati, madarasa, vitabu, maabara, maktaba, motisha kwa Walimu wetu kama vile kuwapunguzia workload kwa kuajiri Walimu wa kutosha, ili waendane na uwiano pendekezwa, wapewe malipo ya ziada. Unakuta Walimu watatu shule nzima mlundikano wa wanafunzi zaidi ya wanafunzi 200 au 150. Walimu wapandishwe mshahara, walipwe posho ya nyumba kama hawana nyumba katika maeneo ya shule, maana upungufu wa nyumba za Walimu ni zaidi ya 80%, walipwe madeni yao ya likizo na wapandishwe madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni kuhusu mikopo ya elimu ya juu; wanafunzi wengi wanaachwa kwa kigezo cha kuwa, alisoma private, lakini pia kuna wengine wamesoma shule za kawaida, lakini wanakosa fursa ya kusoma, hii si sawa na inajenga matabaka kwenye jamii. Ikizingatiwa huu ni mkopo. Ni muda sasa Serikali itenge fedha za kutosha kuwapa mikopo Watanzania wote wenye sifa. Maana Rais wakati wa kampeni 2015 aliahidi akiwa Tabora kuwa, kila Mtanzania mwenye sifa ataenda chuoni.