Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuchangia Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa, nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanazozifanya. Tunawapongeza, jitihada zinaonekana wanafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na kikosi chake chote anachofanya kazi tunawapongeza; na kama Watanzania hatuna la kuwaambia zaidi ya kuwaambia waendelee kufanya kazi. Sisi tunasimama, ni wajibu wetu kuangalia maeneo gani tunaweza kuboresha ili tujenge Tanzania kwa nia moja na kwa nia ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ametumia muda wake vizuri na muda mwingi kuboresha elimu ya juu na ameitendea haki. Michango ya Waheshimiwa Wabunge itaendelea kuboresha katika malengo yake na misimamo yake ya kutaka Tanzania iwe na elimu bora na yenye malengo na yenye ufanisi. Ndiyo maana halisi ya michango inayotoka ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri achukue fursa kwa muda uliobaki. Tukiwa kama Wabunge wenzake tuungane kwa pamoja tuboreshe elimu ya msingi. Muda uliokuwepo kwa sasa, autumie kuboresha elimu ya msingi. Ametumia muda ipasavyo kuboresha elimu ya juu, sasa tunataka kuboresha elimu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa wakati huu, kati ya vitu ambayo vinapaswa kuboreshwa katika elimu ya msingi ni pamoja na kupeleka walimu wa kutosha ndani ya shule. Katika elimu ya msingi tunahitaji walimu wa kutosha. Mheshimiwa Waziri aweke mikakati, ashirikiane na Mawaziri wenzake kuona wanashusha walimu ili wawe kuwapatia elimu ya msingi ya kutosha wanafunzi wa shule za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri kwa masikitiko kabisa, nilikuta shule moja, nakumbuka Liwale; nimebahatika kutembea Liwale kijiji kwa kijiji, nilikuta shule ina Mwalimu Mkuu na Mwalimu mmoja, lakini kuna watoto vijana wa form four na form six, wakaamua kujitolea kuwasomesha wanafunzi wa kijijini kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna watu wanaamua kujitolea ndani ya vijiji vyao, maeneo wanayotoka, kufanya kazi kwa uzalendo, kwa nini tusiwape kipaumbele na fursa ya ajira?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kijana anakaa Kigoma unamshawishi kukumwondoa Kigoma kumpeleka Liwale, mazingira anayokumbana nayo huwa magumu. Ndiyo maana kelele kubwa za Wabunge kutokuwepo walimu wa shule kusomesha, hususan kwenye elimu ya msingi. Walimu wanakimbia kwa sababu ya mazingira wanayokumbana nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimchukua anayetoka kijiji kile kile, hata suala la kukaa na makaazi kwake inakuwa rahisi. Kama hakukumbana na familia yake akaishi, basi atakuwa ana mategemeo ya pale anapoishi. Namwomba Mheshimiwa Waziri kwenye suala la walimu aweke mkakati na mkakati wake kwa uwe kipindi hiki cha Bunge tulichokuwanacho, mwaka mmoja na nusu ili tuweze kumalizia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa ikiwa ni mara ya pili nikiongelea suala la Wizara ya Elimu. Kati ya kero kubwa ambayo naona inaitendea dhambi nafsi yangu, kuwepo shule na bar ikawepo karibu. Nimeshaizungumza Bungeni, kwangu kimekuwa kilio kikubwa. Haiwezekani tuwe na shule na Bar iko pembeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kama Watanzania tunategemea nini? Shule na Bar ipo pembeni; tuna mikakati gani kwa wanafunzi wetu? Tena unakuta ni shule za watoto wa primary, tunategemea nini Mheshimiwa Waziri? Hili nililiomba niliwahi kulizunguza. Hili halihitaji bajeti. Linahitaji tamko. Lazima tujue. Haiwezekani ijengewe na Bar hapo hapo. Tunawafundisha nini watoto wetu? Leo mtoto akitaka kununua soda, anakwenda Bar, akitaka maji anakwenda Bar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichonifanya nisimame kuongea, watoto wanafanya mitihani ya darasa la saba wote wanachungulia nje muziki unapigwa usiku. Hatuwatendei haki Watanzania. Ninalizungumza mara ya pili nikiwa Bungeni. Mheshimiwa Waziri toa tamko, wenye Bar waondoke kwenye shule, tunataka tuwatengeneze mikakati wananchi wa Tanzania na wananchi wa Tanzania. Anayejenga Bar kama mwenda wazimu tunamwambia aondoe Bar katika shule, hatutaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine niliokuwa nalo, natamani sana kuona tunaambukiza uzalendo wananchi wa Tanzania, tuanze kuwawekea uzalendo kwenye utoto wao. Yaani tukimplekea mtoto wa shule wa primary kumpeleea uzalendo tunatakuwa na nchi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalendo uanze kusomeshwa chini. Mtoto wa darasa la kwanza na la pili ukimwambia itifaki ya Tanzania haijui. Tumpe itifaki ya Tanzania kupita wimbo. Waliotunga nyimbo za nyingi za Tanzania na nyimbo nyingine wapo, kwa nini tusiwatumie? Mtoto tangu yupo chini, mdogo, afundishwe uzalendo wa nchi yake. Haya tunayopiga kelele humu ndani yataondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yawe ni historia ya kuiwekea mkakati, Kama somo la historia, basi liwekewe makakati wa kuanzia chini kuja juu, liwe na uzalendo ndani yake. Haya tunayopiga nayo kelele yote yataondoka. Hivi kama mtoto wa Kitanzania, tumemjengea msingi wa uzalendo wa historia yake ya Tanzania katika somo la historia ipasavyo, unavyodhani tutapata shida na ma-engeener wa nchi hii? Unavyodhani, tutapata shida na Madaktari wa nchi hii? Wote watawajibika katika misingi ya uzalendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalendo ni kila kitu. Kati ya mambo mengi tunayoyafanya, tunasahau kuwapa uzalendo. Tumwangalie Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, moja ya kitu kinachomsumbua ni uzalendo, nafsi yake imejawa na uzalendo. Uzalendo ndiyo uliokufanya kufanya mambo mazuri na yenye tija. Tuambukize uzalendo kutoka chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutoe mifano ya dini zetu zote mbili ambazo ni kuu; dini ya Kikristo na Kiislamu, inampandikiza mtoto imani akiwa mdogo. Leo mtoto wa Kiislamu anapelekwa Chuoni toka mtoto. Dini ya Kikristo wana Sunday School, watoto wadogo wanafundishwa dini. Nini maana yake? Maana yake ni kuweka misingi ya dini akiwa mtoto. Tuweke misingi ya uzalendo kwa watoto wetu wakiwa wako chini. Hatuwezi kuweka uzalendo wakiwa juu, hawatakuwa wazalendo hata siku moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya, lakini pia aliangalie suala la riba ya mikopo kwa wanafunzi. Atumie mama fursa yake, natamani nimhamasishe kama mama, lakini kuna watu watanipa mwongozo. Kama mama atumie fursa yake, ahurumie Taifa hili, ashikane na Kiongozi wetu na Rais wetu tufanye kazi ambayo yeye anataka tuifanye. Mambo madogo tu tukiyarekebisha elimu yetu itakaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nashukuru kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)