Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami niungane na Wabunge wenzangu walioshangia kwenye hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Suala hili la elimu naona kama ni suala kubwa kuliko hata suala la Katiba. Ukiangalia juzi TRA walitangaza nafasi 70 za kazi, waliojitokeza ni wanafunzi 40,000. Suala hili ni suala ambalo Wizara ya Elimu ilitakiwa isikitike na iogope sana na vyuo vikuu vilitakiwa visikitike na vishangae sana. Wewe una watu 40,000 wakapata kazi watu 50, hawa wengine wanakwenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu yetu hii tulirithi kutoka kwa wakoloni, kwa Waingereza haina pingamizi, wakimaliza watu laki tisa wakastaafu, Uingereza kwa mfano, watakaomaliza shule au university watakuwa milioni moja. Kwa hiyo laki tisa watapata kazi, hawa laki moja Serikali inaweza kuwatunza na kuwahifadhi. Lakini kwetu sisi wanaomaliza shule wanaweza kuwa milioni moja wanaopata kazi ni 50,000 kwa hiyo tukiendelea na utaratibu huu nadhani tunatengeneza bomu kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala hili naona kila mtu anaogopa kupasema lakini ukweli ni vizuri tukubaliane na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambao wao ndio watunga sera za elimu, tukubali iundwe Kamati au Tume ambayo itachunguza suala zima la elimu kwa Tanzania. Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, amejaribu kuliongea hili suala mara mbili, mara tatu, lakini naona kama watu hawalichukulii kwa uzito. Watu 40,000 ukachukua 50,000 kama wangekuwa Uwanja wa Taifa wakasema hawatoki mule uwanjani utakuwa na kazi ngumu sana ya kuwatoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vizuri watunga sera watutengenezee Sera mpya ya Elimu ambayo itawafundisha watoto wetu kutoka shuleni, darasa la kwanza wafundishwe shughuli zao za nyumbani; iwe biashara, kilimo, ufugaji na asilimia 50 ya maksi wapate kutoka huku, asilimia 50 wapate za darasani. Itatusaidia wakati mtu anakuja kumaliza sekondari au university hata unapomwambia aende akajitegemee kweli anayo sababu ya msingi na anafahamu atajitegemea nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kumwambia mtu aende akajitegemee, wewe umechukua pesa zake milioni 10 za university ukampa unayosema wewe ni degree, lakini kiukweli umempa karatasi. Umempa karatasi kwa sababu ni sawasawa na mtu amecheza DECI; hii degree hakuna mahali inapotambuliwa kokote, hata kama unaumwa huwezi kuiweka dhamana pharmacy, huwezi kuiweka dhamana benki. Sasa inawezekana kweli; mimi nimesomesha mtoto wangu, nimeuza mifugo yangu nimelipa milioni 10, wewe umenipa degree halafu wewe unaniacha mimi nikazunguke mtaani na ile degree na sidhani ukifika kwenye mji ulioathirika kama huo mimi mwenyewe ni muathirika wa degree, ninao watoto sita wana degree, kwa kweli inahuzunisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingekuwa bora watunga sera tukubaliane kwamba vyuo vikuu kabla havijatangaza nafasi za shule vikatafute ajira pia na vyenyewe, vieleze mishahara kwamba tumepata NBC shilingi laki nane mshahara, tumepata NSSF laki tano, sasa tunaanza kusajili lete milioni tano nitakupa degree kazi hii hapa. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, linaweza kuwa suala la kuchekesha, lakini hali ni mbaya sana kule mtaani; watu wanazo degree kila kona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini muda wa kusoma vilevile watunga sera wauangalie upya. Ni kweli nani alifanya research kwamba ubongo wa binadamu unahitaji kila mwaka darasa moja, kama yupo atuambie. Wakati huu nafasi za ajira hakuna, unachukuliwa mtoto wako miaka 17 unarudishiwa ana miaka 25, unaambiwa katafuteni kazi ya kujitegemea, mnajitegemeaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama watakubali watunga sera mwaka mmoja watu wasome madarasa matatu au manne ili watu wamalize shule mapema itatusaidia sana ili mtu akimaliza shule arudi huku tuje tuendelee na maisha kijana akiwa bado mdogo. Leo wanakaa naye muda wote wanakuja kukurudishia wewe miaka 25, huwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye familia zilizoathirika kwenye suala hili la elimu ukasema elimu ni ufunguo wa maisha, watakwambia hapana, elimu ya leo ya Tanzania ni kifungo cha maisha. Maana yake ni gereza ngumu sana; umefungwa wewe, amefungwa mtoto, amefungwa mama na pesa zimekwenda na umezeeka, wote mna vyeti viko ukutani na majoho ya siku ya graduation, cha kufanya hakuna, mnatazamana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina nia ya kubeza elimu lakini wakati huu uliopo ni lazima tufanye mabadiliko makubwa sana vinginevyo tunaziona nchi nyingi sana duniani sasa hivi zina matatizo makubwa kama haya. South Africa wanalo tatizo kwa sababu wote wamefuata elimu hii hii tu ya Mwingereza ambayo ni sukuma document basi, hakuna kitu kingine. Mwisho wa yote leo tuna shida kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana sana, kwa kuwa suala hili linaonekana limemtesa kila mtu, Mheshimiwa Waziri akubali kuunda Tume kama Mheshimiwa Rais Mstaafu Benjamini Mkapa alivyosema ili ijaribu kuchukuwa maoni kuhusu suala hili. Tume hiyo ijumuishe na wananchi wa kawaida siyo lazima wawe wasomi tu wawepo na watu wengine maana sasa hivi waathirika ni wengi sana sana, kiasi ambacho hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda kijijini kwenye majimbo ukiwauliza wananchi ni mtoto yupi mwenye faida hapa kijijini. Kama siyo uongo wanakwambia mtoto ambaye hajasoma ndiye mwenye faida kijijini. Anafuata wa darasa la saba, wa form four halafu wa degree. Wanasema wenye degree wanasema ni kama viazi vilivyoshindwa kuiva. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema hivyo kwa sababu hawezi kulima au kufanya kazi yoyote, anasubiri ajira na ajira hakuna. Kama zimetangazwa nafasi 50,000 walioomba ni 40,000 na hawa ndiyo wana email na internet, je, ambao hawana email na walioghairi ni wangapi. Je, watu hawa wapo wapi sasa hivi na wanafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu alifikirie sana suala hili. Najua watu wengi wanaogopa kulipasua. Nasikia Mheshimiwa Waziri anasema aboreshe elimu lakini unaboresha elimu ipi kama watu hawajapata kazi uliyozalisha? Bidhaa inaboreshwa pale ambapo bidhaa uliyopeleka sokoni wateja wamesema tunataka bidhaa aina fulani, ukisema unataka kuboresha elimu unaboresha ipi kama watu walio bora… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)