Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Mattar Ali Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shaurimoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri na timu yake yote pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Alhaj Masauni kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ambayo nataka niyazungumze, nataka Mheshimiwa Masauni anisikilize vizuri.

MWENYEKITI: Unasemaje Mheshimiwa?

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri sana.

MWENYEKITI: Eeeh, ndiyo Waziri mwenye hoja.

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar kuna Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ambapo leo ndani ya Bunge hili ni mara ya pili kuvizungumzia kwamba havitumiki katika kupata passport na leo vilevile havitumiki kupata hata laini ya simu. Sioni sababu kwa nini Vitambulisho hivi vya Mzanzibari Mkaazi haviwezi kutumika kwa sababu ya kupata passport ya Mtanzania wakati vitambulisho hivi ni halali ambavyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa pesa za walipa kodi kuhakikisha vitambulisho hivi wanavitumia Watanzania. Tunaomba Waziri wakati wa kuhitimisha atupe majibu mazuri kuhusu Vitambulisho hivi vya Mzanzibari Mkaazi ili Wazanzibari wapate fursa ya kuvitumia kusajili laini pamoja na kupata passport. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kushangaza leo tuna NIDA hapa ni kwa nini Vitambulisho hivi vya Mzanzibari Mkaazi haviunganishwi kwenye system kwa wakati ili vikapata hadhi yake? Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, Serikali yetu imefanya kazi kubwa na tuipongeze sana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhakikisha Wazanzibar wote wanapata vitambulisho hivi. Leo tunashangaa kitambulisho hiki kina kasoro gani mpaka hakiwezi kutumika katika matumizi hata ya kusajili line? Mheshimiwa Waziri naomba tuhakikishe kitambulisho hiki kinaweza kufanya kazi kwa maslahi ya Wazanzibari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni miradi ya Wizara hii, bado ni changamoto kubwa. Wizara hii ya Mambo ya Ndani wanapoanzisha miradi hasa ya Jeshi la Polisi mfano majengo hayamalizwi kwa wakati. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha alichukue suala hili ili Wizara hii aipatie fedha za kutosha ili ikamilishe miradi yake kwa wakati. Tukifanya nusu na fedha zikipelekwa nusu inasababisha miradi hii kutokamilika na hizi fedha zinaweza kupotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha atoe fedha kwa wakati kuhakikisha miradi hii inamalizika kwa wakati. Kama haikuwezekana kutoa fedha kwa wakati, nimwombe sana Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Kangi Lugola badala ya kutekeleza miradi yote basi achague miradi muhimu ili iishe kwa wakati tusibakishe majengo tu yasiyoisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tuna majengo ya kufanyia kazi hayakaliki, hayawezi kufanyia kazi. Siku moja nilikuwa sehemu moja katika Mkoa wa Kusini Unguja, nimekwenda katika Ofisi ya RPC haifai kufanyia kazi. Jengo lile ni la zamani na plan ya kujenga jengo lingine haijawa tayari. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kulichukua suala hili, alitembelee jengo hili na kama kuna uwezekano wa kujenga jengo lingine wafanye haraka kujenga lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, wapo askari wanastaafu wakiwa na vyeo vya Sergeant lakini mafao yao wanalipwa na vyeo vya Corporal hawapati haki zao husika. Sasa Mheshimiwa Waziri ikiwa askari hawa wamefanya kazi na mmewapandisha vyeo wamefika wakati wa kustaafu kwa nini hawapati mafao yao ya cheo husika cha kustaafia?

Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri ulichukue hili na ulifanyie kazi na askari hawa waliostaafu ambao hawajapata haki zao kwa ukamilifu utoe haki kwa ukamilifu ili askari wetu waweze kulitumikia Taifa letu kwa makini zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)