Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Anna Joram Gidarya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika hii Wizara ya TAMISEMI. Kwanza kabisa naomba nichukue fursa hii kwa kuwapa pole viongozi wangu, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe na dada yangu Mheshimiwa Ester Matiko, kwa muda mrefu kuwepo mahabusu kwa ajili ya dhuluma ama kutokufuata utaratibu na miongozo ya utawala bora kwa watu wanaoshikilia hayo madaraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitangulize kwa kusema utawala bora ni matokeo ya msingi bora wa maadili mema. Misingi hii inakubalika na inatokana na mtawaliwa na yule anayemtawala mtu mwingine. Kumekuwa na vurugu nyingi kwa baadhi ya watendaji wa Serikali hususan Wakuu wa Mikoa na ma-DC. Kumekuwa na mkanganyiko kati ya Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi katika halmashauri nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, tumekutana na kesi nyingi, mwaka jana tumeshauri, lakini bado mwaka huu hizo vurugu zinaendelea, natumai Waziri akija atatuambia hizi kero za kila siku zitakwisha lini? Utawala bora ni pamoja na kulinda wale watu unaowaongoza, lakini katika nchi yetu imekuwa ni tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi yanayoudhi, kuna mambo mengi ambayo yanaleta hitilafu tunasema rais anafanya kazi nzuri nami nakubali ni kweli anafanya kazi, lakini wao wenyewe humu ndani ndiyo wanaomwangusha rais. Tusifurahishane hapa hata Rais mwenyewe anajua kwamba wao ndiyo wanaomwangusha, wanamwangusha vipi? Amepewa dhamana kubwa yeye kwenda kutawala kwa ile ngazi ambayo inampasa yeye lakini hawampelekei ripoti nzuri. Huku chini wanakuja kwa ajili ya kukamiana, kila mtu kwa nafasi yake akatekeleza wajibu wake, wanatuletea Wakurugenzi ambao hawajui hata mipaka ya kazi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakuu wa Mikoa vile vile, kila mtu kwenye hizo nafasi zao amejifanya Miungu watu, tena wengine wamewaleta wanathubutu kabisa wanakwenda kwenye shughuli za ufunguzi wa miradi, ni DED amevaa shati ya CCM. Tukisema haya mnatuombea miongozo, kuhusu utaratibu kwamba siyo kweli, kwamba ma- DED na ma-DAs ni makada wa CCM, hata hilo mnakataa? Ushahidi tunao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na shida kubwa, kuna issue ya TAKUKURU, nchi hii watu wanaogopa hata kufanya biashara. TAKUKURU wakikuweka ndani leo hii utakaa miezi miwili wanasema uchunguzi bado, lakini kesi wamezibadilisha. Hivi mtu ambaye hana hata shilingi milioni 10 benki unambadilishiaje kesi kwamba ni uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, anatakatisha makaratasi? Wasaidieni watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala ni kitu cha msimu tu, tutapita, tutarudi mitaani, tutakoseana heshima, lakini at least ungali wewe kama unajua unaishi je, watoto wako unawabakizaje huku nyuma? Tumejenga athari, mioyo ya watu inalia, wamekuwa waonevu, uchumi kama unashuka wasiende kuumiza watu kwa ajili ya kuwakamata wanatafuta pesa. Tufungiane humu ndani tutafute namna bora ya kuuinua uchumi wa nchi hii. Hivi wanavyowakamata hawa wafanyabiashara, wanafikiri kwamba hawa wafanyabiashara ndiyo wachangiaji wakuu wa mishahara. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anna subiri taarifa.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Wenyekiti, nataka kumpa taarifa dada yangu anayezungumza kwamba, waliokuwa makada wa CCM kuwa ma-DC na Wakuu wa Mikoa wala siyo shida, kwa sababu hata yeye alikuwa kada wa CCM lakini leo hii ni Mbunge wa CHADEMA, anaamini katika kazi yake mpya.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anna.

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona alikuwa anataka nimwone tu, kwa sababu mdogo wangu nataka tu nimwambie katika hizo ngazi, mimi nilikuwa CCM na najua utaratibu unaoendelea ndani ya CCM. Kwa hiyo ninachokizungumza siyo kwamba nabuni, nina jua.(Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye tume ya haki za binadamu, kumekuwa na mazuio ya mikutano ya hadhara. Hivi leo hii kama Mbunge wa Upinzani wa Jimbo ananyimwa asifanye mikutano kigezo kikuu nchi nzima kumekuwa na sababu wanasema, intelejensia, hivi intelejensia iko kwa Wabunge wa CHADEMA tu, halafu mnawatuma polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu ulindwe. Naomba niendelee asinipotezee muda.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J.NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, subiri taarifa hiyo.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hakuna Mbunge wa Jimbo anayezuiwa kufanya mikutano kwenye maeneo yake. (Makofi)

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anna umeisikia hiyo taarifa? Hakuna Mbunge anayekatazwa kufanya mkutano kwenye Jimbo lake.

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa.

MHE. MCH.PETER S. MSIGWA: Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Haya Kuhusu Utaratibu.

MHE. MCH.PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 64(1)(a) Mbunge hapaswi kutoa taarifa za uongo.

Mheshimiwa mwenyekiti, Mbunge aliyesimama sasa hivi hapa anasema Wabunge hawazuiwi kufanya mikutano kwenye maeneo yao. Mimi nimekuwa mhanga na nimelalamika mara nyingi nakataliwa, Wabunge wengi tunakataliwa kufanya mikutano kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa anasimama hapa anasema uongo, kwa nini Mbunge unasema uongo na Wabunge wenzako tupo? Tunaomba afute uongo huo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Peter Msigwa hata na mimi naelewa kwamba Mbunge hakatazwi kufanya mkutano kwenye eneo lake.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Tuendelee Mheshimiwa Anna.

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu ulindwe. Mimi sijazoea kujibizana na watu wenye umri wa baba zangu. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tu, twendeni tukajenge nchi kwa maslahi mapana ya vizazi vyetu vya baadaye, tutasifiana humu lakini ukweli wanaujua mioyoni mwao na Biblia inasema, ole wako mnafiki. Sasa tusinafikiane humu ndani, mikutano ni kweli wanazuia lakini kwa nini wanakimbia vivuli? Hilo wanalijua kwa nini wasituruhusu tukafanya mikutano, tukutane jukwaani kwa hoja, wasitufungie kwenye chupa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie mambo machache tu kwa ajili ya Taifa hili. Huku ndani watu tunaenda na interest za vyama lakini hao hao wanaopiga kelele humu ndani kwenye maeneo yao hakuna kitu. Kuna halmashauri nyingi hazifanyi vizuri katika mapato ya ndani, tuache vyama twendeni kwenye halmashauri zetu, wananchi wanataka nini. Maendeleo yanaletwa sisi tumetumwa huku kwa ajili ya kutetea wananchi, tumekuja hapa tunapongezana, ni interest tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni halmashauri kama sita hazikufanya vizuri na wamo humu wanaotetea. Mfano mzuri ni Mkoa wa Mtwara, Halmashauri ya Masasi imefanya kwa asilimia 10.95, Nanyumbu asilimia 10.44, Tandahimba asilimia 13.22, wastani ule wa mkusanyo ni 11.53. Leo tunasifiana huku wanasema wamefanya kazi nzuri, kwa nini hawakushauri huko kwenye halmashauri zenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nsimbo ni halmashauri mojawapo imetuangusha 23.5, Mlele 26.3, Tunduru 27, sasa leo hii hapa tukisema tuambizane kwa nini tunahangaika humu kupeana taarifa kusifiana tu, haiwezekani, tusemane humu ili tukajenge kule kwa wananchi. Tumekosa umoja humu kwa ajili ya hili Taifa kwa sababu kuna watu wanajipendekeza huko. Halafu wanaojipendekeza huko kwa taarifa yao jamaa mwenyewe anapiga mzigo, sasa wafanye kazi na wao wasimfurahishe furahishe humu. Bahati nzuri yeye huwa haendi na upepo anafanya kazi, haya twendeni. (Makofi)

MWENYEKITI: Haya malizia dakika moja.

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni ni halmashauri mojawapo pia yenye madeni makubwa. Halmashauri inadaiwa milioni 112 na CRDB benki, asilimia 20 ile ya vijiji haipelekwi, leo hii hapa tunasema kila kitu kimefanyika, kimefanyikaje? Halmashauri inadaiwa, makusanyo ya ndani yanaenda kulipa madeni ya mikopo ya Madiwani, mtapata wapi maendeleo. Halafu huku mnaogopana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie issue moja ya mwisho tu dakika zangu hizo zilizobaki. Kuna issue ya Mfuko wa Jimbo, Wakurugenzi wamekuwa wamiliki wa Mifuko ya Jimbo, Mkurugenzi ana uwezo wa ku-host pesa za Mfuko wa Jimbo na kule kuna akinamama wanakufa kwa ajili ya kukosa dawa. Hawataki hizi pesa zifanye maendeleo na kazi ya Mfuko wa Jimbo siyo kwenda kumaliza miradi ni kwenda kuchochea maendeleo. Sasa kwanini Wakurugenzi hawa wasichukuliwe hatua? Au basi kama hawajui waambiwe utaratibu na mipaka yao ya kazi, Wakurugenzi wanasigana mno na ma-DC na Wabunge.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anna, ahsante sana.

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)