Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama ili niweze kuchangia kwenye Wizara hizi ambazo ziko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nichukue nafasi hii kukishukuru chama changu, Chama cha Mapinduzi, kikiongozwa na jemedari wake Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo inafanyika katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, naomba nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Waziri wetu wa TAMISEMI kwa kazi kubwa na nzuri ambazo anazifanya, lakini sambamba na hilo kwa uwasilishaji wake ambao ni mahiri sana, pamoja na kwamba muda kwake ulikuwa ni mfupi, lakini nimpongeze kwa uwasilishaji wake na kazi nzuri ambazo anazifanya kila kona ya nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais mara alipochaguliwa au kabla ya kuchaguliwa aliwaahidi Watanzania kufanya kazi kwa umahiri na weledi mkubwa sana. Hii inaonesha kwamba Mheshimiwa Rais anawatumikia Watanzania. Ukiangalia kwenye kipindi ambacho kinasema tunatekeleza na kishindo cha Awamu ya Tano unaona jinsi kazi ambavyo zinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ukiangalia tunatekeleza, unaona kila kona ya mkoa wa nchi yetu, kila wilaya, kila eneo na Mawaziri wote kwa pamoja wameshikamana kufanya hizo kazi ambazo zinaonekana katika nchi yetu; ama kweli Tanzania ya viwanda inaonekana na tunaamini itakapofika mwaka 2025 kwa kweli uchumi wa kati utafikiwa kabla ya huo mwaka ambao tunausema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa machache tu naomba niyaseme yafuatayo ambayo Mheshimiwa Rais na Serikali yetu imetekeleza; ujenzi wa Stiegler’s ambao utatusaidia kupata umeme wa bei nafuu na sisi tunaelekea kwenye nchi ya viwanda, ni lazima tuwe na umeme wa bei nafuu. Sambamba na hilo, kuna standard gauge, itarahisisha usafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine, vilevile, itapunguza matatizo ya barabara kwa sababu mizigo mingi inaposafirishwa kupitia barabarani maana yake ni kwamba barabara inaharibika na kila baada ya muda mfupi inabidi tutengeneze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo, sisi tunahitaji watalii. Amenunua ndege ambazo sio kwamba watatumia watalii pekee bali hata sisi wenyewe ndani ya nchi tutazitumia. Na tunashuhudia, Jumatatu asubuhi watu wengi, kila mtu anahitaji ile ndege na watu wengine wanakosa, na hizo ndege watu wote tunazipanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ameanzisha Mahakama ya Mafisadi. Hili nataka nilisemee; Mahakama ya Mafisadi ilikuwa na umuhimu kwa sababu ni agenda ambayo ilikuwa imezungumzwa kwa kasi sana lakini Rais wetu na chama chetu ni sikivu, chama chetu kimetengeneza ilani ya kuvishughulikia hivi vitu na kweli Rais wetu kwa sababu ni msikivu vyote amevifanya, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna suala la elimu bure, elimu hii imeleta chachu ya watoto wengi wa Kitanzania kuingia shuleni. Kila kwenye mafanikio hakukosi upungufu na upungufu ndiyo chachu ya maendeleo. Kwa hiyo sasa tunachotakiwa ni kujipanga juu ya watoto wengi waliopo madarasani kwetu ambao wanakosa huduma muhimu za msingi. Na zote hizi zimeelezwa na jinsi ya kutekelezwa vilevile zimeelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuhusiana na elimu bure naomba nijikite kwenye suala hilohilo, tunaanzia elimu ya awali. Kwenye elimu ya awali ilani inasema kila kwenye shule ya msingi kuwe na darasa la awali na hii imetekelezeka kwa kiasi kikubwa. Jambo ambalo nataka nishauri, kwenye elimu ya awali ni lazima kuwe na Walimu ambao wana weledi wa kuwafundisha wale watoto wa darasa la awali kwa sababu kabla ya hapo tulikuwa hatuna hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake watoto walikuwa wanakwenda kwenye zile private schools wakitoka pale wakiingia darasa la kwanza matokeo yake wale wanaonekana kwamba wana maarifa zaidi kuliko hao kwa sababu hawakupitia elimu ya awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utafiti wanasema hakuna mtu ambaye uwezo wa akili ni mdogo isipokuwa wanatofautiana katika kuelewa, mwingine anaelewa kwa kiwango cha chini, mwingine cha kati na mwingine kwa kiwango cha juu. Kwa hiyo hii elimu ya awali imesaidia sana, hapa ni lazima wawepo walimu wenye weledi sio Walimu wapo basi anachukuliwa huyu nenda kafundishe elimu ya awali, hii sio sawa na haileti afya kwa suala zima la elimu na tukiamini kwamba elimu ndiyo msingi wa kila jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nizungumzie suala la elimu ya msingi; kwenye elimu ya msingi hapa ni lazima tuwaandae watoto wetu tangu mwanzo kuona kwamba hawa watoto wetu je, wanafaa kuwa akina nani, tuwaandae watoto kuwa Walimu kwa sababu kila kitu kinatengenezwa. Sasa kitu ambacho tunakiona unakuta kwamba, kwa sababu watoto hawaandaliwi kuwa Walimu ukienda ukauliza nani anataka kuwa malimu kila mtu ameshusha mkono chini, hataki kuwa Mwalimu kulingana na kutowaandaa na kulingana na mazingira yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hilohilo la Walimu, wamesema kuna Walimu wengi, ajira zimetoka; je, kati ya hizi ajira zilizotoka ni Walimu wangapi? Pamoja na kwamba wanasema wengine wamepelekwa kwenye eneo la wenye ulemavu, je, kwenye ulemavu mmeangalia watoto wenye usonji? Kwa sababu watoto wenye usonji ni wenye mazingira magumu, mtoto mwenye usonji unaanza kumtambua akiwa na umri wa miaka mitatu na ni watoto ambao kukaa nao ni mtihani, naomba tufanye utaratibu tuwaandae.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali haina shule hata moja yenye watoto wenye usonji. Al Muntazir wameanzisha hili darasa la watoto wenye usonji, hakuna ubaya Serikali ikashirikiana na Al Muntazir kuwasaidia watoto wenye usonji kwa sababu kila mtoto anayo haki ya kupata elimu kwa wakati muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Walimu wa sayansi. Tatizo hili ni kubwa sana hapa nchini. Ni lazima tutengeneze mkakati wa kuwaandaa Walimu wa sayansi tangu ngazi za awali, hasa kwenye shule za msingi, tuwaandae watoto tujue huyu atakuwa Mwalimu wa sayansi. Kwa hiyo tuanze maandalizi haya mapema, hatimaye tutaondoa tatizo la Walimu wa sayansi. Pamoja na kwamba wameajiriwa Walimu zaidi ya 1,900, kati ya Walimu hawa je, Walimu wangapi ni Walimu wa sayansi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kama alivyosema pale mwanzo, maandalizi ya Walimu yaanze mapema baada tuwe na mkakati kwamba ndani ya miaka ama mitano au kumi tuwe na kazi ya kuwaandaa Walimu hawa ili tuwe na Walimu bora kuanzia elimu ya awali, elimu ya msingi mpaka elimu ya sekondari, hapa tutakuwa na matokeo mazuri na kama tunataka hayo maboresho. Tunaamini Serikali yetu ni sikivu haya yanawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna suala zima la ukaguzi; nimepitia sikuona kabisa eneo la ukaguzi, au labda pengine nime-overlook, sikuona. Suala la ukaguzi ni muhimu, ni lazima kuwepo na Wakaguzi ili waweze kufuatilia kazi za Walimu, hatimaye ndiyo tutaona mafanikio ya elimu yetu. Hili kwa kuwa halipo ni lazima liwekwe kwa ajili ya ubora wa elimu ya watoto wa nchi yetu, bila ukaguzi hakuna kitu, nazungumza hayo kwa uzoefu wa kazi yangu ya ualimu niliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, hongereni sana. Mheshimiwa Dkt. Magufuli endelea kufanya kazi, tuko nyuma yako. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)