Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Haji Hussein Mponda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi kwanza kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba muhimu sana katika kipindi hiki cha bajeti. Naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ndiye aliyetuwezesha leo kutupa mazingira haya leo tunachangia hii bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze na pongezi za dhati kabisa, kwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli, jamani kazi inafanya. Pongezi pia kwa Waziri Mkuu na Mawaziri walioko katika Wizara yake, lakini vilevile na Manaibu Waziri, pongezi za dhati vilevile ziwafikie Wakurugenzi, Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya. Kamishna Siang’i anafanya kazi ya kujituma sana, mpaka tumefikia hali tulivyo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango yangu itakuwa mifupi sana leo, nitazungumzia hotuba hii ya Waziri Mkuu, kipengele cha 87 na 88 kinazungumzia huduma za kiuchumi. Wote tunajua humu tunapozungumzia uchumi, tunazungumzia Watanzania ambao wengi wako vijijini na wanategemea ardhi. Niipongeze Serikali hii kwa mara nyingine tena, katika Wilaya ya Malinyi, Wilaya ya Kilombero na Ulanga, tuna mradi wa urasimishaji wa ardhi ambao unatuwezesha kupima, kupanga namna gani tutatumia ardhi yetu na mwishoni kuwakabidhi wananchi hati za umiliki. Hili limesaidia kwa kiasi kikubwa sana kuondoa migogoro ya ardhi ambayo inatuweka sasa kwa msingi wa ardhi namna gani tunaweza kuwekeza kuunga mkono jitihada za Dkt. John Pombe Magufuli katika suala la uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye ardhi kwenye kipengele cha 89, Serikali imeeleza wanatekeleza agizo la Mheshimiwa Rais, tarehe 15 Januari mwaka huu Mheshimiwa Rais kama alivyo kwa tabia yake mjasiri, anathubutu ni kweli, amethubutu kusimamisha zoezi la kufuta vijiji 364 katika nchi hii. Wananchi hawa, miongoni mwa hivyo vijiji 364, vingine vipo katika Wilaya ya Malinyi, wamejikuta wao ni wahanga wa mabadiliko ya Sheria ya Wanyamapori ya 2009. Sheria ya zamani ilikuwa imenyamaza haikusema lolote hasa katika mapori tengefu na ndio matokeo yake kwamba vijiji vimesajiliwa ndani ya mapori tengefu na wananchi wameruhusiwa shughuli za kawaida za maisha yao, pamoja na kilimo, uvuvi na ufugaji, sasa 2009, tukabadilisha ile Sheria, imekataza, lakini wananchi hao tayari wako ndani ya hifadhi na wako ndani ya yale mapori tengefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Watendaji wa Serikali hasa hawa wa Wanyamapori wamekuwa too machinery, wamekuwa wanafanya kazi kimashine mno, huwezi kuangalia mazingira yale unawaambia wananchi wale watoke vile vijiji 364. Huu msiba kwa kweli ungekuwa mkubwa sana. Bado migogoro inaendelea, pamoja na Rais ametumia busara ameonyesha ujasiri wake, ameunda Tume ya Mawaziri nane, wamezunguka Mawaziri wale watachukua na michango ya wataalamu, rai yangu ya mwisho kwa suala hili, upande wa kule Malinyi lile Bonde la Kilombero, tuna dhamira ya kweli na tunataka kulilinda, wananchi wale wanachogombania ni kiasi kidogo sana, ile buffer zone, eneo lile la Pori Tengefu la Kilombero ni ina range kati ya kilomita nane mpaka kilomita 23, wananchi hao wanataka kidogo tu wapewe angalau kilomita tatu ndiyo mashamba yao yamo mle. Ndiyo maana nasisitiza nashauri tena Serikali, hili zoezi wanaloendelea nalo la kurejea mipaka wawaachie mashamba yale wananchi, hayo ndiyo maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uchumi, vilevile linaendana na suala la barabara, Serikali imeonesha dhamira yake na tumeiona barabara inayounganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Ruvuma. Hii barabara inaanzia Mikumi, Ifakara, Lupilo, Malinyi, Kilosa Mpepo, Londo, Lumecha mpaka inaingia Songea. Barabara hii sasa imetoboka toka 2017, lakini ombi langu toka itoboke ile barabara haiwezi kutumika kwa sababu bado ina maeneo korofi katika bajeti hii, sijaona dhamira ya kweli kabisa kurekebisha ile barabara ili yale maeneo korofi angalau ipitike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiikamilisha barabara hii sasa tutakuwa tumekamilisha dhana na Sera ya barabara kwamba iunganishe Mkoa kwa Mkoa, nitachangia zaidi itakapofika kwenye Wizara ya Ujenzi. Kwa hiyo hapa ninachoomba, Mheshimiwa Waziri Mkuu, hili suala la barabara ya kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Ruvuma ni muhimu sana kwa maendeleo sio tu hii Mikoa miwili, lakini kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, kama nilivyosema nitachangia ni suala la Tume ya Udhibiti UKIMWI. Ndugu yangu hapa Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya UKIMWI ameshagusia, lakini naomba nisisitize zaidi, jamani, suala la UKIMWI, takwimu zinatuonesha kwamba linapungua, lakini kihali halisi bado tatizo ni kubwa. Sasa naomba tuungane wote kwa pamoja na ule mkakati ambao unasema 90 kwa 90 kwa 90, nini maana yake 90 kwa 90 kwa 90? Ni kwamba asilimia 90 wanaokadiriwa wanaishi na Virusi vya UKIMWI wao wamepima na 90 ya pili ni kwamba wale ambao wamegundulika wanaishi na Virusi vya UKIMWI baada ya kupimwa, waingie kwenye matibabu na asilimia 90 yao wanaendelea na matibabu na 90 ya tatu wale ambao wanaendelea na matibabu ya ARV’s asilimia 90 yao wao wamefubaza Virusi vya UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mkakati ambao unaweza ukatokomeza suala la UKIMWI, nini maana yake, ile 90 ya mwisho maana yake ni kwamba kama mtu umefubaza Virusi vya UKIMWI unakuwekea mazingira wewe huwezi kumwambukiza mwenza wako unayeshea naye kama yeye hajaambukizwa na halikadhalika na yeye hawezi kuambukizwa na Virusi vya UKIMWI kama yule mwenza anatumia ARV’s. Sasa changamoto iliyopo Tanzania hatuna rekodi nzuri katika ile 90, 90, 90 na mkakati huu mwisho 2020 ni mwaka kesho. Sasa hii 90 ya kwanza ndio tuko asilimia 61, najiuliza asilimia 61 leo, 2019 mkakati unasema 2020 tuwe
tumefikia asilimia 90.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa kuna changamoto, tunaiomba Serikali, Kamati ya UKIMWI wamependekeza mara nyingi, tunaiomba Serikali labda isikie kwamba vitu ambavyo vinachangia navyo hii 90 ya kwanza ni suala la Sheria ya UKIMWI. Sheria ya UKIMWI haimruhusu mtoto chini ya miaka 18 kwenda kupima bila ridhaa ya mzazi au mlezi ambapo hawa watoto wa miaka 18 na takwimu zinaonesha waathirika wengi, survey iliyofanywa mwaka 2017 ilionyesha asilimia 40 ya waathirika wa Virusi vya UKIMWI ni vijana wenye umri kuanzia miaka 15 mpaka miaka 24, ndiyo hao tunazungumza wengi wao hawaruhusiwi kwenda kupima kwa hiari yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama mtu ataenda kupima yeye mwenyewe, kwa hiyo tukiongeza idadi ya watu kupima Virusi vya UKIMWI, tunaongeza ile 90 ya kwanza. Sasa hili suala ni la kisheria tumeiomba mara nyingi Kamati ya Masuala ya UKIMWI, Serikali wamekuwa wana-dill dull suala hili hawalileti...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)