Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Gimbi Dotto Masaba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nakushukuru nami kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba nianze kwa kumpongeza Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kazi anayoifanya, lakini pia nimpe pole kwa changamoto anazopitia. Sisi kama Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) bado tunaendelea kumtia moyo na tunamshukuru kwa kuijenga CHADEMA kama taasisi. Hata kipindi anachopitia changamoto taasisi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na changamoto ambayo naona nisipoisema kidogo nitapata shida sana. Nianze na Mkoa wa Simiyu kabla sijaingia kwenye mambo mengine. Mkoa wa Simiyu umekumbwa na changamoto kwenye Halmashauri zake kwenye suala la uchumi. Halmashauri za Mkoa wa Simiyu zinakabiliwa na uhaba wa fedha, hususan Wilaya ya Itilima. Wilaya ya Itilima ni Wilaya ambayo imeshindwa kujiendesha kutokana na kwamba Wilaya ile ni mpya na haina mapato yoyote ya kuendelea kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Serikali ianze kuchukua mapato kutoka kwenye Halmashauri zetu kumekuwepo na changamoto nyingi sana. Madiwani wanakopwa, hawalipwi posho zao, magari ya Halmashauri hayana service hakuna fedha, Wakurugenzi wanashindwa kusafiri kutoka sehemu nyingine kwenda sehemu nyingine kwa sababu hakuna fedha. Historia inaongea ni namna gani Serikali Kuu imeshindwa kukusanya mapato vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017/2018 tulikusanya shilingi bilioni 11.172 na katika mwaka wa fedha 2018/2019 tumekusanya shilingi bilioni 8.434, sawa na upungufu wa negative 44.5. Hapa tutaona ni namna gani ambavyo tumeshindwa kukusanya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema haya kwa masikitiko makubwa sana kwa sababu, wakati mapato yanakusanywa na Halmashauri zenyewe zilikuwa zina uwezo wa kujiendesha, lakini leo zimeshindwa kujiendesha kwa sababu kwanza wao wenyewe wameingiza hasara kwenye ukusanyaji wa napato takribani bilioni 6.8. Haya kwa nini tunayahitaji kuyaingiza kwenye Taifa letu? Nasisitiza na kuomba sana Serikali warudishe makusanyo kwenye Halmashauri zetu ili ziweze kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba nizungumzie kuhusu bajeti ya maji. Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumza kwenye kitabu chake katika ukurasa wa 55, amesema upatikanaji wa maji umefanikiwa kwa asilimia 85. Historia inaongea, kwenye bajeti ya maji, Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge naomba tuipongeze Serikali ya Awamu ya Nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Serikali ya Awamu ya Nne, nimechukua mfano mdogo tu. Bajeti ya mwaka 2012/ 2013, zilitengwa shilingi bilioni 466, zikatolewa shilingi bilioni 303, sawa na asilimia 65, hii sio mbaya ndio maana nimesema tuna kila sababu ya kuipongeza Serikali ya Awamu ya Nne. Mwaka 2013/2014 zilitengwa shilingi bilioni 553, zikapelekwa shilingi bilioni 353 sawa na asilimia 64. Mwaka 2014/2015 zilitengwa bilioni 485, zikatolewa shilingi bilioni 249 sawa na asilimia 50; akaja baba yangu, mwaka 2016/2017, zilitengwa shilingi bilioni 915.1, zikatolewa shilingi bilioni 350.99 tu sawa na asilimia 23. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kiongozi pale Mheshimiwa John Mnyika ameuliza swali lake akajibiwa kwa kejeli na Serikali ikijinasua kwamba, imetekeleza jukumu la maji kana kwamba, asilimia zote imemaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi takwimu tunazotenga zenye namba nyingi…

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. GIMBI D. MASABA: …halafu utekelezaji wake unakuwa mdogo, nataka kuuliza ni nani wanayemdanganya? Kwa faida ya nani?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gimbi kuna Taarifa.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpe Taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba, utekelezaji wa miradi ya maji si kama kilimo cha matikiti kwamba, mwezi mmoja, mwezi wa tatu unavuna. Utekelezaji unaweza ukawekwa mwaka huu, ukavuka hadi miaka miwili, lakini atambue tu katika Mfuko wa Maji tumetengewa shilingi bilioni 158, mpaka mwezi Februari tumeshapokea zaidi ya shilingi bilioni 93. Pia tuna mitadi mikubwa ambayo inatekelezwa maeneo mbalimbali zaidi ya bilioni 54, milioni 154 zimeshatoka. Kwa hiyo, atambue hilo, nampa taarifa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gimbi, Taarifa hiyo.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa siipokei. Kama ana majibu ya kwangu asubiri atanijibu wakati Mawaziri watakapokuwa wana-wind up. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeyasema haya nikisisitiza kwamba, kama Serikali ya nne ilitenga bajeti kidogo, wameona ni namna gani iliweza kutekeleza kwa asilimia ambayo inazungumzika. Hawa wanatenga kwa namba kubwa, matokeo yake utekelezaji ni hakuna, hiyo ndio hoja yangu ya msingi. Sasa nikahoji nani wanamdanganya na ni kwa faida ya nani, kwamba tukiongea namba kubwa, hii itawadanganya wananchi, sasa hali kadhalika hata sisi wenyewe humu Bungeni tunadanganywa. Nawashauri Waheshimiwa Wabunge tusomeni historia ya Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu suala la fedha za maendeleo. Hivyo hivyo historia inazungumza na kabla sijazungumza historia ya Serikali ya Awamu ya Nne nizungumze tu ni kwa mara ya kwanza bajeti ya Serikali ya Awamu ya Tano kutekelezwa kwa asilimia ishirini na… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, muda wetu ndio huo.