Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweke mawazo yangu machache katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu anayetupa nafasi hii ya kusema kwa sababu siyo kwa nguvu zetu wenyewe lakini ni kwa neema zake. Pia tunapochangia, tunachangia yale ambayo tunayaona kwa macho yetu ambayo yamekuwa yakifanyika kwa nia njema tu ya kusaidia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nilivyokuwa Ukanda wa Gaza nilisema yafuatayo: “Ni nchi gani hii isiyokuwa hata na ndege ya kuazima, isiyokuwa na nia njema ya kuona kwamba Tanzania tunahitaji kuwa na uchukuzi wetu wenyewe lakini pia tukawa na ndege zetu wenyewe”, bajeti iliyopita nilikuwa mkali sana. Miaka mitano iliyopita nilivyokuwa Mbunge wa Viti Maalum na nilivyokuwa Mbunge wa Jimbo miaka kadhaa nyuma, nimekuwa nikichangia sana suala zima la Tanzania sisi wenyewe kuwa na ndege zetu. Leo nitazungumza tofauti na ile kauli niliyokuwa nikiongea wakati niko Ukanda wa Gaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia kwa kunukuu, nukuu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo alimnukuu Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli. Ukurasa wa saba katika hotuba yake, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameandika haya yafuatayo akimnukuu Mheshimiwa Rais, amesema: “Tumekuwa wakimya na hatuelezi kwa kina masuala tunayofanya. Niwaombe basi viongozi wenzangu wa Serikali, kila tunapopata nafasi tuseme mambo tunayofanya…tusipofanya hivyo yanayosemwa yataonekana kuwa ya kweli”. Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli hii na nukuu hii inatukumbusha kwamba lazima tuseme mambo ambayo yamekuwa yakifanyika katika nchi yetu ambayo hayajawahi kufanyika. Ni dhahiri kuna mahali tulikuwa tumekwama kama nchi, haiwezekani nchi kubwa tumejaliwa kila kitu lakini hatuna uchukuzi, hatuna ndege zetu na vitu kama hivyo. Kazi kubwa inayofanywa na Serikali hii, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu, wasiposema wengine, tutasema sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze sana hili la Serikali yetu, Mheshimiwa Rais kuhakikisha nchi yetu tunapata ndege zetu wenyewe, imetujengea heshima kubwa sana kama Taifa. Watu hawasemi lakini kipato kinaongezeka na watalii wanaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili niliseme kwa sababu nilisema sana nikiwa upande ule, nikiishangaa nchi hii, ni lini tutakuwa na ndege zetu wenyewe? Leo wametekeleza, hatutaki kupongeza. Naomba nipongeze na hizi jitihada ziendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili, uzalendo huu wa Mheshimiwa Rais Magufuli hata ajuzi tumeona anabadilisha ndege iliyokuwa inatumika kwa ajili ya kubeba viongozi, anaipeleka ibebe Watanzania. Inabadilishwa rangi ili iendelee kuongeza nguvu katika uchukuzi huu. Haya lazima tuyaseme. Naomba tusonge mbele, Mheshimiwa Rais asikate tamaa, amefanya mambo ambayo yalikuwa hayafanyiki na aendelee kuyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuwe wakweli tu, suala la barabara katika nchi zetu, hakuna mahali barabara na madaraja hayajajengwa. Nimekuwa nikiongea kwamba tuna barabara za lami kila mkoa umeunganishwa na mkoa mwingine, nimekuwa nikisifia ya Dodoma - Babati lakini juzi tumefika Kilombero tumekutana na daraja la Magufuli kule, wakati siku zote wale watu walikuwa wanahangaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuache Kilombero, twende Arusha; Mji mzima barabara zinajengwa kwa fedha hizi ambazo leo tunapitisha bajeti. Vile vile twendeni Dar es Salaam, Wabunge wa Dar es Salaam wanafahamu; mimi nimefika Dar es Salaam juzi, nimeshangaa sana; njia nne kwenda, njia nne kurudi, haijwahi kutokea. Haya mambo tusipoyasema tunamkosea hata Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kwenye Bunge lililopita jamani eeh, hebu tusimsifie sana Mheshimiwa Rais, tuangalie, tukosoe kwa upendo. Nilikuwa nasema nikiwa najikaza tu, lakini ukweli unajulikana. Leo niseme kwamba hivi vitu vinaonekana, sisi ni Watanzania, tuache siasa, tuweke ukweli mbele, vitu vinavyofanyika Dar es Salaam kumaliza ile foleni, kumaliza msongamano wa magari barabarani njia nne hizo, upande mmoja mwingine nne, haijawahi kutokea na magari yako site na watu wanafanya kazi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema ya Jimboni kwangu naweza nikawa najipendelea, lakini kwa sababu ni bajeti ya nchi nzima, ni bora Watanzania tukaongea kazi anayofanya Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tunabeza; wengi wanabeza, lakini sijawahi kuona ni Mbunge wa awamu ya pili sasa zinatolewa fedha nchi hii kwenda kukamilisha maboma ya sekondari ili watoto wetu wasome vizuri. Ndani ya miaka mitatu hii ya Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kazi ya maendeleo aliyoifanya haielezeki. Hospitali zaidi ya 67 za Wilaya zimejengwa. Kwenye elimu hawaishii hapo, sasa hivi wanamalizia sekondari, ujenzi unaendelea, wanawaza kwenda kukamilisha maboma ya Shule za Msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo Watanzania wanajua. Hata kama kuna watu watasimama watayapinga kwenye Majimbo yao, wanafahamu mioyoni mwao kwamba maendeleo yanafanyika, isipokuwa tu hawawezi kutamka hadharani kama ambavyo mimi nilikuwa siwezi kutamka hadharani nilivyokuwa ukanda wa gaza. (Kicheko/ Vigelegele/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo maendeleo yanafanyika, hawaangalii, hawabagui, fedha za maendeleo zinatoka. Nenda SGR, zaidi ya shilingi trilioni 7.1 fedha za ndani. Collections zetu kwa mwaka siyo zaidi ya shilingi trilioni 14, lakini Mheshimiwa Rais huyu ambaye wengi wanasimama wanambeza, wanaibeza Serikali ana-commit zaidi ya shilingi trilioni 7.1 kwa ajili ya SGR tu. Hajasema mengine ambayo yanafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisimama le niseme, ingekuwa ni maamuzi yangu tu ningesema hatuna sababu ya kupoteza muda, tuwapitishie bajeti yao Serikali waendelee kufanya kazi, maendeleo yanaonekana. Kuna mtu hapa juzi alisimama akawa anazungumza hoja moja, mioyo ya Watanzania kwa maendeleo haya ambayo yanaendelea, tunatamani Mheshimiwa Rais huyu aendelee kuongoza nchi hii tupate maendeleo. Ninafahamu siyo kauli ya wote inaweza ikawa inakwaza kila mmoja, lakini kwa maendeleo haya yanayofanyika, kila mmoja anaweza akawa ana feelings zake moyoni kwamba hivi tunahangaika na uchaguzi kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifika Dar es Salaam nikasema, kwa kazi hii, barabara hizi, kazi zinafanyika site, tunakwenda kwenye uchaguzi kumchagua Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli awe Rais, kwa kitu gani tunachotafuta tena? Ni kumwambia endelea, chapa kazi ili Watanzania tupate maendeleo. Tunachotaka ni maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ungeniuliza leo mimi Pauline fedha za uchaguzi kwa nini tunakwenda; labda tuchague huko kwenye Serikali za Mitaa na maeneo mengine. Kwa Mheshimiwa Rais tunaenda kuchagua kitu gani? Sawa ni Katiba, tunaenda kuchagua kitu gani? Kwa sababu ambayo yamefanyika hayajawahi kufanyika na yanaendelea kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilirusha kwenye mitandao, Mji wetu wa Babati. Siyo fedha tu za barabara tunawekewa, jana nimerusha mpaka taa za barabarani tunawekewa sasa, Mji umewaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie hotuba hii kwa kusema Serikali yetu chapeni kazi, Waheshimiwa Mawaziri chapeni kazi, Mheshimiwa Waziri Mkuu chapa kazi, Mheshimiwa Rais usiwasikilize, kwa sababu hata wanaokutukana, kwenye Majimbo yao hawajatekeleza ahadi zao. Wewe umetekeleza nyingi. Chapa kazi, fedha ni hizi sisi tunakupitishia hizi fedha, wananchi wanataka maendeleo, hawataki maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi/ vigelegele)