Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Ester Michael Mmasi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pia naungana na wenzangu wote ambao wamepongeza Kamati zote hizi tatu kwa kazi zao nzuri lakini pia na kwa ripoti ambazo ziko well informed.

Mheshimiwa Spika, nitapenda kujielekeza kwenye Kamati ya Huduma za Jamii na nitajikita kama kawaida kwenye masuala mazima ya uboreshaji wa elimu ama mfumo wa elimu ambao tunao. Ni dhahiri kwamba kumekuwa na jitihada mbalimbali katika kuinua fursa za elimu kwa watoto wetu. Jitihada hizi zinaonekana pale ambapo tunaona migomo mingi imepungua au imefutika katika elimu za juu lakini pia kero nyingi ambazo walikuwa nazo wazazi mathalani masuala ya ulipaji ada kwa elimu ya awali yameondoka. Watu wengi tumetoa pongezi hizi kwa Mheshimiwa Rais hasa tukitambua mchango wa Serikali unaoongozwa na Mawaziri wake na Naibu Waziri tunawapongezeni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika nchi mbalimbali duniani kote lakini pia katika ulimwengu wa kwanza elimu inatumika kama nyenzo kuu katika kukuza uchumi na kupelekea maendeleo ya dhati kwa Taifa husika. Misingi hii ya ujenzi wa uchumi ni dhahiri kwamba katika nchi mbalimbali haifanani.

Mheshimiwa Spika, kwa nchi ya Tanzania uchumi wa sasa tunavyouangalia, tunajitahidi kuwekeza hata katika miundombinu ya elimu, tunajikita hasa kwenye ku-promote uchumi wa viwanda (Industry Economy), lakini pia katika Mataifa yaliyoendelea, wamehama katika mfumo huu wa kusukuma uchumi kupitia Industry Economy kwenda kwenye knowledge economy. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Safi sana.

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Spika, tunapoongelea knowledge economy tunaangalia nchi ya Tanzania inavyowekeza nguvu nyingi katika kuinua uchumi mathalan ujenzi wa Stiegler’s Gorge, uwekezaji wa anga na uwekezaji kwenye Bahari Kuu, uwekezaji wa utalii na masuala mengineyo, bado tunaona kuna kila sababu kwa nchi ya Tanzania kuona umuhimu wa promote au ku- embrace knowledge economy kwa maana ya kwamba elimu au mfumo wa elimu uinue zaidi masuala ya ujuzi na maarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu bila kuoanisha muktadha huu vizuri ni dhahiri kwamba hata nguvu zinazowekezwa na Serikali zitakosa mapokeo chanya kwa vijana ambao wanaandaliwa kwa mifumo ya elimu ambayo tuko nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inasikitisha sana kwamba kupitia ilani bado tuna maswali mengi ya kujibu kwenye masuala ya ajira. Ninapoongelea knowledge economy ni dhahiri kwamba vijana wetu watashiriki rasmi kwenye kuandaa ajira zao wenyewe, watatoka kwenye kusimama kwenye nafasi ya utazamaji na badala yake wataingia na kuwa key players katika kuandaa ajira zao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapoongelea uchumi unaojengwa na maarifa pamoja na ujuzi, ni kwamba vijana wetu kama nilivyosema wanaweza wakajiandalia ajira zao. Ukiangalia sasa na niliwahi kusoma kitabu cha Henry Mintzberg ambaye aliandika kitabu kimoja kizuri sana MBA’s But Not Managers inaeleza vizuri masuala haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nimetoka Kilimanjaro na dada yangu Mheshimiwa Stella Ikupa ni shahidi, tulikwenda Kilimanjaro na maelekezo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu tukitaka kuwatengenezea ajira vijana wetu; na kwa Mkoa wa Kilimanjaro tulipata fursa za kuwatengenezea ajira vijana 800 kila Wilaya. Tulikuwa tumepanga kuboresha ajira za vijana kupitia kilimo kwa watoto mia moja moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dada Stella ni shahidi, lakini pia tunaye Eng. Kahabi ambaye ndio alikabidhiwa jukumu hili. Nilipita kila Wilaya, nilisikitika, hakuna graduate hata mmoja aliyeweza ku-respond kwenye mradi huo wa Serikali ambao wameweka fedha, wameweka wataalam katika kuwafundisha vijana katika kuingia rasmi kwenye Sekta ya Kilimo. Kilimanjaro tuna fursa nzuri sana ya kimasoko, tumepakana na Kenya, lakini wanafunzi hawajaandaliwa kwenda kuingia kwenye ushindani wa kibiashara, wanafunzi hawajaandaliwa kwenda kuandaa ajira zao au kushiriki kwenye ajira zisizo rasmi.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kuongelea changamoto ambazo pia nimezisikia zimeongelewa hapa asubuhi. Tunafahamu kwamba Serikali ilifuta Vyuo 19, nia na makusudi ni kuleta tija katika mfumo wa elimu. Tunaipongeza sana Serikali na tuko pamoja na Serikali katika maamuzi haya. Katika muktadha huu wa kufuta vyuo, lakini bado kuna dosari chache ambazo zimeonekena na ninafikiri ni vizuri Serikali ikaingilia kati na kuona.

Mheshimiwa Spika, imeelezwa kwamba wanafunzi wengi baada ya kuhamishwa kwenye vyuo hivi, unaenda mtu ana-inquire loan status anaambiwa loan not registered. Siyo hivyo tu, wapo wanafunzi kwa Mkoa wangu wa Kilimanjaro ambao walitoka St. Stephano Memorial University ambao walipelekwa Chuo cha Mweka, lakini wengine walipelekwa Masoka na wengine walipelekwa Ushirika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu anasoma let’s say BBA, lakini anapopelekwa Masoka anaenda kuingizwa kusoma HR akiwa tayari ana background ya miaka miwili amesoma Accounts au amesoma BBA. Akienda Masoka, baada ya miaka miwili kukaa kwenye Chuo kile alichofutwa, anaenda kule anaingizwa kwenye mfumo wa kusoma HR anaitwa ni graduate.

Mheshimiwa Spika, Taifa kwa lililoendelea hatuwezi kujikita kuandaa bomu kwa Taifa hili kwa maana ya kwamba tunaona kuna uwekezaji mkubwa unaofanywa na elimu ya juu kupitia Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote wa Loans Board. Kwa hiyo, nafikiri ni jambo ambalo inabidi liangaliwe vizuri sana.

SPIKA: Mheshimiwa Ester unaweza ukarudia kidogo hicho kitu? Kimefanyika cha namna hiyo?

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Spika, ndiyo. Ninao ushahidi, kuna wanafunzi ambao walitoka St. Stephano Memorial University ambao walipelekwa Mwika na Ushirika. Walikotoka walikuwa wamesajiliwa masomo mengine, walipofika kwenye vile vyuo walivyokuwa dispatched wameenda kulazimika kusoma masomo mengine ambayo walikuwa hawana foundation nayo. Nasema hapa nikiwa na ushahidi wa mwanafunzi ambaye alikuwa anasoma BBA akaenda Mwika akalazimika kusoma HR. Ni Mwika kama sikosei, Ushirika, akalazimika kusoma HR. Nafikiri hapa inabidi pengine Wizara itusaidie.

SPIKA: Subiri kidogo Mheshimiwa Ester, Profesa amesimama.

T A A R I F A

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nimpatie taarifa Mheshimiwa Ester Mmasi.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa tu nataka kumpa taarifa kwamba, utaratibu ni kwamba mwanafunzi anapohama, anahama na kozi kama alivyo. Kwa hiyo, utaratibu wa mwanafunzi kwenda kubadilisha, hicho ni kitu ambacho, kama anao ushahidi naomba anipatie ili niweze kuufanyia kazi. (Makofi)

SPIKA: Ndiyo maana na mimi nilistuka kidogo, nikamwambia hebu rudia hilo, maana yake ni jipya. Endelea Mheshimiwa Ester.

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Spika, nitafuatilia, nitampatia document Mheshimiwa Waziri ili kwa pamoja tuone ni kwa namna gani tunaweza kuboresha haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, lakini kuna changamoto ya masuala ya Bima ya Afya. Tunaona wanafunzi wanaosoma Vyuo; Private University vis-à-vis public Universities, yaani hivi vyuo vinafsi na vyuo vya Serikali, unakuta ulipaji wa bima hizi unatofautiana. Utakuta kwa mfano mwanafunzi anayesoma kwenye Chuo cha Serikali analipa Sh.50,400/=, lakini wale wanaosoma vyuo binafsi wanalipa shilingi 100,000/=.

Mheshimiwa Spika, napenda Wizara yako ifahamu, masuala haya yanaleta sintofahamu kubwa kwa sababu siyo wote wanaoenda kwenye Private University wako vizuri au wazazi wao wana uwezo wa kuwapeleka na kuhimili maelekezo yote ambayo yanaondoa masuala mazima ya uniformity kwenye muktadha huu.

Mheshimiwa Spika, naomba Waziri husika au Wizara husika itusaidie kuona hapo tunafanyaje? Kwa sababu kimsingi wanafunzi hawa wanaotoka kwenye background za wazazi wa wakulima, wafugaji na vitu kama hivyo. Kwa hiyo, kuwa kwenye Private University, haimaanishi kwamba mtoto huyo au mzazi huyo alipenda kwenda pale. Wengine tunalazimika kwa kuchangiana kwenye ukoo, kukopa, kuweka rehani vitu mtoto aende kwenye hicho chuo asibaki nyuma. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri na hilo pia atusaidie kuangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo concern ya uporaji wa mali kupitia taasisi zetu hizi za elimu. Inafahamika na nilishawahi kumwona Mheshimiwa Waziri wa Elimu, lakini pia suala hili limewahi kuletwa na Mheshimiwa Mizengo Pinda, mwaka 2006, vile vile hapa Bungeni liliwasilishwa mwaka 2016 kwamba kuna shule ambayo inaitwa Shule ya Kolila ambayo inatokana na Kijiji cha Old Moshi ambacho kinaitwa Sudan.

Mheshimiwa Mweneyekiti, Shule ya Kolila ni shule ya wazawa na ni shule ya kijiji ambapo Kijiji hicho cha Old Moshi kilikuwa na ekari zake 40. Kijiji kilijitahidi kikajenga madarasa 10, lakini cha kusikitisha katika shule hii, Shule ya Kolila imeingia kwenye mgogoro mkubwa na mvutano mkubwa na dhehebu la Kikristo ambalo sitapenda kulitaja nisije nikaleta migongano huko ya kiimani.

Mheshimiwa Spika, Shule Kolila ni Shule ya Wanakijiji, shule ile ikaja baada ya wanakijiji kukosa nguvu ya kuiendeleza ikakodishwa kwa shirika hilo la taasisi ya kidini. Kinachosikitisha, leo hii shule ile haikuwahi kuendelezwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Ester, muda hauko upande wako.

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Spika, nitaomba pia nikabidhi taarifa hizi TAMISEMI na kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)