Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie hoja hizi za Wenyeviti watatu. Kwanza kabisa, nianze kuwapongeza Wenyeviti wote wa Kamati tatu ambazo wamewasilisha taarifa zao hapa Bungeni. Pia nitoe pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais wetu John Pombe Magufuli na kwa Mawaziri wote ambao Wizara zao ziko kwenye hizi Kamati kwa kazi nzuri sana ambazo wamekuwa wakizifanya na kwa kweli wanaitendea haki nchi yetu na Chama chetu cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile naomba niipongeze Serikali kwa utoaji wa pesa kwa ajili ya Hospitali za Wilaya 67. Kwa kweli pesa hizi hata katika Mkoa wetu tumepata Iringa DC, Kilolo na Mufindi lakini naomba nitoe ombi maalum. Katika Mkoa wetu wa Iringa tunayo hospitali ambayo ipo katika Manispaa yetu, Hospitali ya Frelimo, Iringa Mjini ambayo iliazishwa mwaka 2013, naomba Serikali yetu iwapatie pesa kwa sababu kabla ya hizi pesa hazijaenda kujenga hospitali za wilaya hizi nilizozitaja wagonjwa wanatibiwa katika hospitali hii. Kwa hiyo, naomba Serikali ingeangalia kama kuna uwezekano wa kuhakikisha kwamba hizi hospitali ambazo zinafanya kazi basi zipewe kipaumbele. Hii hospitali ingejengewa wodi za akina mama, akina baba na watoto ingeweza kusaidia hata kupunguza msongamano mkubwa ambao upo katika hospitali yetu ya mkoa. Vilevile ingeweza kujengewa hata jengo la vipimo ambalo kwa kweli imekuwa ni tatizo. Kwa hiyo, niombe ombi maalum kwamba sasa hivi tumalizie hizi hospitali ambazo zipo na tayari zimeanza kusaidia maana hospitali hii imesaidia kupunguza vifo vya akina mama na watoto katika Mkoa wetu wa Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna changamoto kubwa sana katika Hospitali ya Mkoa, kuna mwingiliano katika Hospitali ya Mkoa na katika Gereza la Mkoa. Mwingiliano huo kwa kweli ni mkubwa sana kwa sababu kuna wakati ambapo barabara zinafungwa, wagonjwa wanashindwa kupelekwa hospitali wakati wanapeleka wafungwa kwenye gereza. Kwa hiyo, naomba kipaumbele kitolewe kwa sababu bale wanashindwa hata kuongeza majengo kwa ajili ya Hospitali yetu ya Mkoa ambayo Serikali yetu sasa hivi imesema hizi hospitali za Mikoa zitakuwa za rufaa na zingeweza kusaidia sana katika Mkoa wetu wa Iringa na Nyanda za Juu kwa suala zima la matibabu. Katika Hospitali ya Mkoa hakuna nyumba za Madaktari Bigwa, kwa hiyo, wananchi wanapata shida sana, hili ni ombi maalum.

Mheshimiwa Spika, nimwombe tu kaka yetu Mheshimiwa Sugu kwenye Wizara ya Afya kazi kubwa imefanyika. Kuna vingine ambavyo Wapinzani mnatakiwa muunge mkono. Nishukuru safari hii mengi mnayaunga mkono na iwe hivyo kwa sababu ni kwa nia nzuri kabisa Serikali yetu inafanya kazi hizo. Nimpongeze Mheshimiwa Tulia anafanya kazi nzuri sana, amewatendea haki sana wananchi wa Mbeya, kwa kweli hongera zako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda ukurasa wa 37 na 38 wa Kamati ya Huduma za Jamii, naomba niunge mkono kabisa ushauri wa Kamati hii wa kuiwezesha Idara ya Maendeleo ya Jamii. Idara hii mara nyingi imekuwa haipatiwi pesa za kutosha na ndiyo ambayo inasaidia jamii na sasa hivi tuna tatizo kubwa sana la watoto kubakwa na vifo vya watoto.

Mheshimiwa Spika, vilevile, napenda kujua Benki yetu ya Wanawake imefikia wa wapi, kwa sababu najua idara hii ipo chini yake. Kuna wakati kulikuwa na sintofahamu kwamba na yenyewe imetangazwa na Benki Kuu hata akina mama sasa wameingia wasiwasi kwamba hii benki sasa inawasaidiaje wanawake? Benki hii tulikuwa tunajua ndiyo suluhisho la akina mama kwamba hatupati zile shida za benki nyingine ambazo zimekuwa zikituzalilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nielezee pia kuhusu bima ya afya. Niombe katika bima ya afya kuna ile package ya Sh.1,500,000 ambapo huduma anapata baba, mama na watoto wanne lakini utakuta kina mama wengi au familia sasa hivi ile package hawasaidii kwa sababu watoto wakiwa juu ya miaka 18 hawatibiwi. Nashauri ingekuwa vizuri ikawepo na package ya mtu mmoja pengine iwe Sh.500,000 ili kama watoto wangu wameshafikisha miaka 18 niweze kumkatia bima yake ama kama nina mzazi wangu basi niweze kumkatia bima yake au mama mwingine ni mjane, wababa wengine ni wagane inakuwa haina maana kuchukua package nzima. Kwa hiyo, naomba suala hili lingeangaliwa ili kuweza kusaidia wananchi ambao wanahitaji bima kwa ile package ya juu kwa maana ya grade one. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuchangia kuhusu ukarabati wa shule zetu za msingi. Kwa kweli hili ni tatizo kubwa sana. Katika Mkoa wetu wa Iringa shule nyingi sana za msingi ni za siku nyingi sana. Kwanza nipongeze Serikali kwa ukarabati shule kongwe za sekondari, Ifunda imetuhusu, shule nyingi kweli zimekarabatiwa, kwa kweli nipongeze.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe hizi shule za msingi kwa sababu katika halmashauri zetu bado hakuna uwezo wa kuzikarabati. Mara nyingi tumekuwa tukianza kujenga madarasa kwa ajili ya hii elimu bure, kwanza nimpongeze Rais kwa elimu bure katika Mkoa wa Iringa, lakini kuna tatizo ambalo limejitokeza kutokana na ukongwe wa hizi shule za msingi basi vyoo ndiyo haviingiliki kabisa. Watoto wetu sasa wamepata hata tatizo la kubakwa sababu mojawapo ni kwamba wanakwenda kuomba kujisaidia kwenye vyoo vya jirani na shule hazina uzio. Kwa hiyo, naomba Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi iangalie kabisa hizi shule za msing kwa sababu ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee kuhusu capitation fund. Wanapotoa hii fund wanaangalia idadi ya watoto lakini hawaagalii matatizo yaliyopo. Kwa mfano, sasa hivi shule nyingi sana wanashindwa kulipia maji, umeme na zile gharama ndogo ndogo. Kwa hiyo, kuna zile shule ambazo idadi ya watoto siyo wengi lakini wanatakiwa kugharamia huduma hizo nilizosisema, nashauri labda wangeangalia jinsi ya kuwa na mfumo mwingine.

Mheshimiwa Spika, utakuta shule zetu hizi za msingi wamekatiwa maji hivyo watoto wanapata shida sana. Kwa sababu sasa hivi ni elimu bure pengine tungewaacha watoto wasikatiwe maji kwani wamekuwa wakipata matatizo sana mfano kunapokuwa na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu. Kwa kweli shule nyingi za msingi hata za sekondari hazina maji labda tungeangalia mfumo mwingine mzuri wa kusaidia shule hizo ili wasikatiwe maji bali shule iendelee kudaiwa au Serikali iangalie njia nzuri zaidi ya kusaidia hizi shule zetu za msingi ili kuondokana na changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nielezee kuhusiana na timu zetu ambazo zinazocheza daraja la kwanza hasa za wanawake. Kwa mfano, pale Iringa kuna timu ya Panama inashiriki hili kombe kwenye mazingira magumu sana. Nafikiri nilishamwambia hata Waziri tuone tunawasaidiaje hawa watoto wa kike na pale kuna vipaji vikubwa sana lakini utakuta wanashindwa kwenda kushiriki sehemu nyingine au wanakwenda kwa shida au wanatembeza mabakuli kiasi kwamba hawa watoto wakike wanaweza kupata masharti mengine. Naomba Wizara ya Michezo ingalie njia nzuri ya kusaidia hizi timu za wanawake ambao wanashiriki ligi kuu ya daraja la kwanza kwa sababu najua pale ndiyo tutapata vipaji vya kuunda timu ya Taifa kutoka kwenye mikoa mingine. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)