Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, na mimi nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nichangie machache kwenye kamati hizi tatu. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu Subhanahu-wataala kwa kutupa afya njema.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, niipongeze sana Serikali kwenye ujenzi wa vituo vya afya vinavyosimamiwa na TAMISEMI na Wizara ya Afya, wamefanya kazi kubwa sana. Mheshimiwa Rais kwa hili hata uchaguzi ujao kama ni 2020 au 2022 anatereza tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri iliyofanywa ya ujenzi wa vituo vya afya, zipo kasoro ndogondogo kwenye maeneo yetu, zinaweza kurekebishwa. Rai yangu na ushauri wangu kwa Serikali ni kuandaa watumishi wa kutosha watakaofanya kazi kwenye vituo hivi vya afya. Leo tutajisifu tumetengeneza vituo vya afya vizuri, vifaa vitakavyowekwa kwenye vituo hivi ni vifaa vya kisasa, je, tumejiandaa vya kutosha kuwa na programu ya kupeleka watumishi huku? Hili ni jambo ambalo nadhani kwamba ipo haja sasa Wizara ya Afya, TAMISEMI na Utumishi kuanza kuchukua hatua za haraka kwa sababu MSD tayari wameshaanza maandalizi ya kununua vifaa, nani atakwenda kuvipokea kule na hao wataalam watakaopokea wana ujuzi huo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, nije kwenye elimu. Kwa mtazamo wangu mimi nafikiri tumepoteza plot somewhere. Elimu yetu ya sasa imekuwa ni ya biashara zaidi. Vyuo vikuu karibu vyote vinaandaa extension officers na tunawafundisha vijana kwa kuwafahamisha kabisa kwamba tunawaandaa kwa ajili ya ajira, ajira zenyewe hazipo.

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri, leo pale Chemba wanafanya mahojiano ya kupata Watendaji wa Vijiji nafasi sita lakini walioomba ni 870, walioitwa 220. Juzi Chamwino hapa, walikuwa na nafasi nne za Watendaji wa Vijiji lakini walioomba walikuwa 1,500. Jeshini nimeona siku moja wameenda kwenye uwanja wa mpira wanagombea nafasi nane. Kwa hiyo, elimu yetu inawajenga watu kwa ajili ya ajira badala ya kujiajiri. Nadhani tuangalie namna gani tunaweza kufanya kama Taifa.

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye utawala bora, lakini naomba nizungumzie mwisho kwa sababu lina changamoto yake. Kwenye walimu, siamini kama kweli tuna matatizo makubwa ya walimu ila tuna tatizo la reallocation ya walimu. Mfano ni hapa Dodoma Mjini, kuna excess ya walimu 371 lakini shule za pembezoni huko Chemba, Kongwa, Mpwapwa zina matatizo ya walimu. Kwa hiyo, TAMISEMI wakae chini waangalie, hivi tatizo ni nini? Nadhani tatizo liko hapohapo TAMISEMI, wakae chini waangalie namna gani reallocation ya walimu ilivyo, walimu wanapelekwa lakini hawakai, wanarudi kwenye shule za mjini.

Mheshimiwa Spika, lingine ninalotaka kushauri ni kwenye michezo. Niombe sana Serikali lazima tuwe na programu ya walimu wa michezo. Kwenye mpira wa mguu Taifa hili ni kubwa sana, ni aibu sana kuwa na walimu wa mpira wa mguu qualified kutoka Burundi wanakuja kufundisha mpira wa miguu Tanzania. Ni aibu kwa sababu hatuna programu ya kuwa-train wachezaji wetu wanaostaafu mpira na wenye uelewa ili waje wafundishe vilabu vyetu, kutwa kucha timu zetu za Taifa hazitafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, angalia hata ligi ya wanawake leo inachezwa nyumbani na ugenini. Timu imetoka Njombe inakwenda kucheza Mwanza hawana mahali hata pa kulala halafu mnasema waende home and away akina dada wale. Leo asubuhi Timu ya Majimaji ya Songea imekwama Dar es Salaam inashindwa kwenda Tanga, kocha wao anasema vijana wamekula jana, usiku hawajala tunategemea msaada ili tuweze kwenda Tanga, hatuwezi kuendesha mpira hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kakoso ananiambia Yanga imetoka Tanga ika-draw ikaja Singida ika-draw, ndiyo matatizo hayo.

SPIKA: Mheshimiwa Nkamia, siyo timu za akina dada peke yake zinazotembeza bakuli, zipo na timu zingine mnatembeza mabakuli tu. (Makofi/Kicheko)

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli. Sikutaka kuitaja timu hiyo kwa sababu rafiki yangu Mheshimiwa Mwigulu yeye ni mfadhili wa timu zote mbili. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la utawala bora. Utawala bora siyo uchaguzi na hili naomba niliseme kwa dhati sana na wewe juzi ulitania hapa. Naomba niiseme kwa dhati sana utawala bora siyo uchaguzi kwamba tukifanya uchaguzi kila baada ya miaka miwili, mitatu ndiyo utawala bora, siamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sina elimu ya kutisha sana lakini ni philosopher na sifanyi mambo bila kufanya utafiti. Nchi zote zilizoendelea duniani hazikuendelea kwa sababu ya kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitatu. Wajerumani wale leo ndiyo the leading country katika uchumi Ulaya, Angela Merkel yule mama pale amekaa miaka 16. Rwanda tunayoipigia mfano hapa ndani, tunasema inafanya vizuri sana kwenye uchumi, Kagame amekaa miaka mingapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo Lionel Messi huwezi kumuweka nje eti kwa sababu amecheza mechi kumi. Tupo kwenye siasa za ushindani, ukiwa na mchezaji mzuri acha aende. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa sisi kama Taifa lazima tufanye maamuzi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Nkamia, nakuongeza dakika tatu uhitimishe vizuri. (Makofi)

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hata hao Wazungu tunaokimbilia kwao, tunakwenda kulalamika unajua hivi na hivi na wao pia wameendelea nchi zao kwa kufanya utafiti. Ukiniruhusu nipo tayari kuleta hoja yangu hapa ndani ya Bunge. (Makofi)

MWONGOZO WA SPIKA

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, mmoja kati ya watu ninaowaheshimu sana ni Mheshimiwa Mchungaji na mmoja kati ya watu wanaonisumbua sana nilete ile hoja ya miaka saba ndani ya Bunge ni pamoja na yeye. Katika kudhihirisha hilo, hata yeye mwenyewe amekosea amesema nchi yetu inaongozwa kwa vipindi vitatu wakati siyo kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba unilindie muda wangu, nilichokuwa nataka kusema ni kwamba sisi kama Taifa hata tukifanya amendment ya Katiba si tunakwenda kwa wananchi. Leo Baba Mtakatifu yuko Uarabuni, anafanya study Uarabuni kwamba hii hali ya dunia inavyokwenda sasa ikoje? Wakatoliki wengi wanahama sasa kwenda kwenye Ulokole, lazima tutafute njia nyingine ya kujua kwa nini wanahama.

Mheshimiwa Spika, mimi hoja yangu haina maana kwamba Rais Dkt. Magufuli aendelee miaka saba, hoja yangu ilikuwa na maana ukomo wa Bunge ambaye Rais ni sehemu ya Bunge. Kwa hiyo, hata waandishi wengi na ninyi wengine mliokuwa mnalalamika hapa ndani baadhi yenu, hakuna mahali nilikotaja Rais Dkt. Magufuli akae miaka saba ila ukomo wa Bunge uwe miaka saba.

MBUNGE FULANI: Rais ni sehemu ya Bunge.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mchungaji Msigwa hiyo ndiyo anaipenda sana. Nikuhakikishie hoja hii ukiiruhusu ikaja hapa ndani ya Bunge…

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Zipigwe kura za siri (anonymous)…

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Hata dakika mbili hapa kila mmoja ataomba karatasi. Naomba mniruhusu nilete.

Mheshimiwa Spika, naomba niishie hapa kwa leo, nimalizie kwa kusema nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Na Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Mawaziri chapeni kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)