Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Nampongeza sana rafiki yangu Mheshimwa Khatib kwa maneno mazuri sana leo aliyozungumza lakini hata vitabu vya dini vinasema umpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Kwa hiyo, maneno matamu aliyoongea na mazuri yenye usia mzuri kama Mtanzania halisi angeanza kwanza kushauriana na majirani wakimsikiliza kwamba ushauri wake ni mzuri sisi wa mbali tutapokea bila wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie upande wa biashara ya madini. Sisi tunatoka kwenye maeneo ya madini, nilitaka nimpe ushauri kaka yangu Mheshimiwa Mpango, biashara ya madini ni ngumu sana na kodi iliyowekwa kwa mchimbaji wa kawaida ni asilimia saba, maana yake loyalty asilimia sita na export levy ni asilimia moja na wachimbaji wameitikia wito wa kulipa hiyo kodi, hawana tatizo. Wanapomaliza kulipa hizi kodi unawarudishia tena dhahabu wakauze wao wenyewe, haijalishi ina ukubwa wa kiasi gani. Sasa hawana uwezo wa kupeleka Kenya, pengine hawana passport, hawana nini wanaenda kuuza kwa watu wa kawaida, lakini baada ya mwaka unakuja tena kuwakamata unataka wakupe document ya ku-export ile dhahabu, biashara ya dhahabu ya dola moja faida yake ni shilingi 15,000 au 20,000 mtu hawezi ku-afford kwenda kuuza dhahabu Kenya au wapi, anauza humu ndani kwa watu wa kawaida anaendelea na biashara yake. Baada ya mwaka unakuja kumwambia tunaomba document za export levy na kama hauna utulipe 18% ya VAT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu hiki sio sahihi na ninyi Serikali mimi nawashangaa kwa sababu unawezaje kuchukua dhahabu ukaitoza kodi halafu ukamrudishia mwenyewe akauze huku mnahangaika na kangomba, mnahangaika na kahawa, kwa nini msinunue hii dhahabu mkaiweka stock kuliko kuhangaika na mbaazi na kangomba hawa wanaotusumbua. Mnachukua hii kodi mnaenda kuhangaika na kangomba Mtwara. Nakuomba sana kama kuna uwezekano sisi tumeitikia kulipa kodi vizuri muichukue hii dhahabu, muiweke stock kwa sababu dhahabu haishuki bei kama hizi kangomba tunazohangaika nazo humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nilikuwa nazungumzia suala la upanuzi wa viwanja vya ndege. Mheshimiwa Waziri ninakuomba sana katika viwanja hivi ambavyo kiukweli vinaisaidia shirika letu kama Mwanza na Mbeya, tengeni pesa ya kutengeneza hivi viwanja tuache maneno ya kusema kila siku kitu ambacho hakitekelezeki.

Mimi nataka niwape mfano Waheshimiwa Wabunge wanaotumia uwanja wa Mwanza, ukienda ndege ya jioni inapoenda Dreamliner inaenda na watu zaidi ya 200, Wasukuma wameitikia kuchangia nchi yao. Inaenda FastJet na watu 100, inaenda Precision Air ina watu 70, mnapoteremka kwa wakati mmoja ni aibu, Mheshimiwa Waziri usipite VIP hebu pita huku wanapopita watu wa kawaida, ni msongamano ambao kile kichumba kinaweza kupokea wageni 30, kinapokea watu zaidi ya 400 na kama hatuna hela basi mruhusu tuweke hata maturubai maana kuna mvua na kuna vitu vingine, lakini nikuombe ujaribu kuangalia uwezekano wa kuwahisha ujenzi wa nyumba ya kupokelea wageni pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine Mheshimiwa Waziri, tunakubali kabisa kwamba tunahitaji nchi yetu tulipe kodi na tuchangie kwa kutumia EFD machine. Mimi najiuliza hizi hesabu wanazopiga pengine Wakuu wa Mikoa na Serikali inaruhusu, ukikaa hapa Dodoma ikifika saa 5.00 usiku karandinga inazunguka, kalaleni. Wageni wakija hapa, sasahivi nchi imehamia Dodoma unaweza ukaja kumuona Waziri, huna kazi nyingine hamjui mtu, ukaambiwa utamuona Waziri kesho kutwa, inabidi ukae kusubiri, kwa hiyo, mchana wote unaambiwa ukakale baa hazifanyi kazi, vitu vingi vimefungwa, kuna tatizo gani? Kwani mnaambiwa na nani kwamba, mkiwalaza watu saa 5.00 usiku wanaenda kulala?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine watu wanaingia vyumbani wanajifungia, lakini mngeruhusu watu wakanywa bia watachangia pesa. Watu wakiingia kwenye ma-guest watapewa risiti. Tuache huu ukiritimba wa kuwalaza watu saa 5.00 usiku tujifunze kwenye nchi zinazoendelea. Sio kwamba, mkiwalaza watu saa 5.00 usiku ndio itakuja hela, tunapoteza pesa kwa vitu ambavyo tunataka kujiuliza tuna wasiwasi gani kwamba, ma-group ya majambazi yana nguvu kuliko polisi wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye usafiri mnataka magari yasisafiri mwisho saa 5.00 usiku. Mtu anataka afanye kazi Mwanza aende akanunue vitu Dar es Salaam, polisi ni wengi wafanye doria na magari yaruhusiwe pia kutembea usiku na mchana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la viwanda. Suala la kufungua viwanda Tanzania kiukweli mnahamasisha vizuri na Rais wetu anafanya kazi nzuri, lakini sijui kama mnajua hizo adha zilizoko kwenye ufunguzi wa viwanda; unafuata procedure zote TIC, ukienda TIC pale OSHA yupo, migration yupo, taasisi zote zipo, lakini hazina mandate ya kuruhusu. Ukimaliza kujadili pale tena wanabeba makaratasi kumtafuta Waziri aweke muhuri, hiyo ni miezi sita.

Ukiruhusiwa kufungua kiwanda tena anakuja mtu wa mazingira anafunga, mtatuua na madeni tutauzwa na benki, jaribuni kutengeneza utaratibu mwingine. Jaribuni kuangalia hivi vitu vyote viishie TIC pale kuna kila kitu kiko pale, kwa nini tunawasumbua wawekezaji wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mimi juzi wakati imetangazwa kwamba kutakuwa na mdahalo wa wanachuo kikuu pale wanaojadili uchumi, sikutoka nje na niliweka mpaka tv huko jimboni kwangu watu waone Serikali ilivyofanya kazi, lakini haya mambo huwa ninazungumza kila siku wasomi wetu ndio tatizo mnapotufikisha. Mimi nilidhani mtachambua na kuwaeleza watu kwamba, uchumi wetu kutoka miaka mitatu alipoingia Rais Magufuli tumefanya hiki kwenye kitengo fulani, tumefanya hivi kwenye dhahabu, tumefanya hivi kwenye nini, badala yake tena wasomi wetu mmeenda kuchambua tu hotuba za Rais ndio mmetuwekea kwenye tv. Maana yake Rais wetu anafanya kazi nzuri, wasomi wakubwa mmeshindwa kuwaelimisha watu wakajua tulikotoka na tulipo kelele hizi zikaisha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaenda kuchambua maprofesa wazima mnachambua hotuba za Rais zilezile ambazo Mheshimiwa Rais Magufuli anatueleza na tunampenda kwa sababu hiyo hiyo. Nilikuwa naomba sana maprofesa mliomo humu, ikitokea tena mnafanya huo mjadala mtukumbuke na darasa la saba tuna akili za kushauri kuliko za kwenu za makaratasi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka kuchangia kuhusiana na biashara ya sukari. Nimesikia kuna wafanyabiashara kule Kahama na wapi wamekamatwa. Mimi najiuliza hebu mfanye utafiti, issue hapa sio kukamata wafanyabiashara, watu wanarudishwa maisha yale ya kawaida na ninasikia Wabunge wengi kila mtu anasimama anasema hali ni mbaya hali ni mbaya, ningekuwa nategemea kila Mbunge aseme Rais alegeze wapi, pesa zilizopotea ni zile za wizi na kanjanja, haya maisha sisi tumeyazoea vijijini siku zote wala hatuna tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pesa zilizopotea sio kwamba labda ziko kwenye biashara ya sukari, mimi nikiuliza leo ukisema sukari sijui inaletwa kutoka nje, kama biashara ya sukari inaletwa kutoka nje wanafanya re-bag wanaweka kwenye mifuko ya Tanzania tumuite na mtu wa biashara ya majani ya chai tumuulize naye kama anauza na yeye biashara ni mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi niombe tu haya mambo bya mabadiliko ya tabia ambayo sasa hivi Watanzania tunaishinayo tutapata taabu sana kuyaelewa kama tutakuwa hatufanyi research za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine nilikuwa nataka kuzungumza kuhusiana na suala, niliwahi kuzungumza humu watu wengi wakanicheka na sioni ajabu kuzungumza, suala la bangi. Mnaona na bahati nzuri mimi natumia simu ya tochi, ninyi wote humu wengi mna simu za whatsapp, za mitandao hizi na nini, ukiangalia Canada juzi wameruhusu, foleni iliyokuwepo haijawahi kutokea utafikiri wanachagua Rais wa nchi, kwenda kununua bangi iliruhusiwa hadharani, ukienda Lesotho, ukienda Zambia, ukienda South Africa hivi vitu vimeruhusiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niwambie wataalam mnaofanya research mnasema bangi ina matatizo, mimi sio mvutaji, ina matatizo, mnaokula diclopa, mnakunywa coca cola, red bull, hizi zote ni bangi ni ganzi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)