Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana awali ya yote nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia leo kuweza kusimama hapa na kUweza kutoa mchango katika hoja iliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuanza kuchangia naanza na utangulizi ambao ni muhimu kwa ninavyoona. Katika siku za karibuni kwenye nchi yetu umezuka mjadala mpana kuhusiana na juu ya ndoa za jinsia moja. Tumesikia sauti/kauli za baadhi ya Mawaziri akiwemo Mheshimiwa Kangi Lugola na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje. Katika kauli zao inaonekana kuna kamtego wa juu ya kuonekana kwamba kukubaliana na jambo hili na kukinzana na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwaambie Waheshimiwa iwe ni mtego au ni bahati mbaya, lakini sisi Watanzania hatutoingia katika mtego wa ushoga, Watanzania hatutaki ushoga hiyo ni mtego. Narudia kama alivyosema Mheshimiwa Kabudi iwe mmetumwa au ni bahati mbaya Watanzania hatutoingia kwenye mtego wa kukubali ndoa za jinsia moja na nawaambia m-take note please, u- take note Mheshimiwa Lugola, Tanzania ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni muungano wa nchi mbili Zanzibar na Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar asilimia 99 ni waislamu na waislamu kwa vyovyote suala la ushoga hawalikubali, tunawaambia nyoosheni maneno sawa, nchi yetu haikubali ushoga na huo ndio msimamo wa Tanzania nadhani mmenielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naumia sana moyoni mwangu kuona nchi iliyostaharabika, nchi yenye utamaduni wetu wa asili, leo kuna baadhi ya watu wanasingizia misaada iwe ni ajenda ya kututoa sisi kutupeleka kwenye ubaradhuli, haiwezekani, hili jambo ni baya na Watanzania hawataki kusikia kabisa. Nawaomba viongozi wetu kama hili jambo likae kimya kama hamuwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa tumezungumza kuna mawe yale ya chuma kule Liganga, hivi kwa nini tusitumie akili zetu kwa rasilimali alizotupa Mwenyezi Mungu mpaka tunafikiria kulainisha maneno ooh, hatutawanyanyasa, hatutawafanya hivi. Watanyanyaswa kwa sababu sheria ya nchi yetu haikubali ushoga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kuchangia sasa, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Rais aliyepita Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliwahi kusema…

T A A R I F A . . .

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taarifa bora zilizowahi kutolewa kwenye Bunge hili, hii itakuwa inaongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea majibu ya kiuanaume kama hilo lililotolewa na Mheshimiwa Kangi. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu matamu kwa wote. Nilitumia dakika moja sasa naanza upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipoazimia na akaweka nia ndani ya moyo wake kwamba Tanzania ipate Katiba Mpya alikuwa na maono mapana juu ya kuipeleka nchi hii katika mema tunayoyatarajia. Nataka ninukuu baadhi ya maneno machache aliyoyasema Mheshimiwa Rais Mstaafu wakati wa maazimio ya kutunga Katiba Mpya. Mheshimiwa Rais Mstaafu Kikwete alisema, nanukuu;

(i) “Tutatunga Katiba Mpya itakayoainisha Muungano wetu kwa kuondoa changamoto zilizopo sasa.

(ii) Tutatunga Katiba mpya itakayoipa nchi yetu mfumo bora wa kuongoza na kuendesha mambo yetu.

(iii) Katiba itakayoimarisha upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania licha ya tofauti zao za asili kwa upande wa Muungano na maeneo wanakotoka na tofauti za jinsia, rangi, kabila, dini, ufuasi wa vyama vya siasa.

(iv) Katiba itakayodumisha amani na usalama wa nchi yetu.

(v) Katiba itakayostawisha zaidi demokrasia, kuheshimu haki za binadamu, utawala wa sheria, utawala bora na kudhibiti maovu.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli hii na maneno haya hakuna yeyote ambaye anaweza kuyapinga kwamba ni kauli iliyo hai na ni kauli ambayo haitakufa milele na milele na milele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais John Pombe Magufuli wakati wa kulifungua Bunge hili aliwahi kutamka uzuri wa juu ya kazi aliyorahisishwa na Rais aliyepita wa kuandaa Katiba Mpya na akawaeleza Watanzania kwamba yeye ataendeleza pale palipobakia. Hiyo ni ahadi aliitoa ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumemsikia tena Mheshimiwa Mtukufu Rais akisema kwamba hayuko tayari kutoa pesa watu waje wale bure kwa ajili ya Katiba Mpya. Mimi nataka kutoa ujumbe kwa Watanzania, Mheshimiwa Rais alipozungumza na akasema kwamba ataiendeleza Katiba ile alisema akiwa ndani ya Bunge hili, Bunge la wananchi na hii ndiyo nchi ya Tanzania. Yeye Mheshimiwa Rais ni sehemu ya Bunge na Bunge hili aliliaminisha hivyo, kwa hiyo nawaomba Watanzania bado waichukue kauli ya Rais kwamba ile iliyotoka kweney Bunge ndiyo kauli official ya umuhimu wa kuendeleza Katiba Mpya mpaka pale itakapopatikana.

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi mpango uliopita Mheshimiwa Mpango hapa nilishauri nikamwambia hivi, kodi zetu si rafiki kwa wafanyabiashara na nilikutolea mfano wa kontena moja la vitenge katika tariff zenu ninyi TRA hapa Tanzania mnai- charge karibu milioni 80; lakini kontena hilo hilo likifika Zambia wana-charge kama milioni 20. Matokeo yake mzigo unapita kwenye Bandari ya Dar es Salaam, unaenda kupelekwa Zambia na wafanyabiashara wetu wanalipia Zambia mzigo ule unakuja kidogo kidogo unauzwa katika soko la nchi yetu. Hilo nililishauri nikakwambia angalieni kodi rafiki, wafanyabiashara waweze kulipa, hamkulizingatia. Sasa ndiyo maana tukaona hata tukishauri hamfanyi kitu, turudi huku kwenye Katiba Mpya ndiyo itakayotuongoza ili tufikie mafanikio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii mipango tumekuwa tukishauri mambo mengi sana. Wewe unaelewa Mheshimiwa Mpango kama biashara Tanzania imeanguka, wafanyabiashara wanakimbia nchi, tumeshauri njia. Mheshimiwa Zungu jana alisema gharama za Bandari ya Mombasa na Dar es Salaam ni tofauti kama ardhi na mbingu. Yanashauriwa hayo hamna mnachokifanya, turudi kwenye Katiba, Katiba ikituongoza tukipata uongozi bora, yote haya yataondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapolilia Katiba iwe bora, tunapolilia uongozi bora matokeo yake ziko nchi walizoweka miundombinu yao ya reli iwe na kila kitu. Ziko nchi ambazo zilifanikiwa katika mambo yote, walichokosa, ni uongozi bora dakika tano iligharimu mazuri yote yaliyotokana na waliotekeleza, Syria iko wapi leo, Libya iko wapi, Misri iko wapi leo? Ilikuwa hawana shida ya pesa wala miundombinu. Walichokosa ni uongozi mzuri, ushirikisho wa wananchi katika nchi zao ilisababisha kila kitu. Hii leo tunajenga hizo reil, Stieglers Gorge na vitu vingi tunafanya, tutakapokosa ushirikiano, amani, uongozi bora, siasa safi matokeo yake itakuwa tunafanya kitu cha hovyo. Dakika tano nyingi inaweza kuja kutokea watu wabaya wakamaliza jitihada zote kubwa mnazozifanya zikaonekana hazikuwa na msingi wala maana yoyote.