Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Lucy Thomas Mayenga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kwa kunipatia nafasi hii walau na mimi niweze kutoa mawazo yangu kwenye mpango huu ambao umeletwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa mpango huu mzuri. Naomba kumpa moyo sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake. Haya maneno mengine ambayo yanasemwa uyazoee tu kwa sababu leo wanasema, kesho wanasifia, ndivyo walivyo baadhi ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda nimpongeze sana kwa nafasi ya kipekee Mheshimiwa Waziri wetu Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mtendaji mkuu, ni kiongozi wa shughuli za Serikali ndani ya Bunge. Anafanya kazi nzuri sana, anafanya kazi kubwa sana na mimi napenda sana style ambayo huwa inakuwa ya kimya kimya, tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa leo tunajadili mpango lakini yapo mambo ambayo mbele huko tunaona mwanga mkubwa sana na wa kijani. Hata hivyo, mafanikio haya yatakamilika endapo na sisi wenyewe kama Taifa tutakaa katika mstari na kufanya yale mambo ambayo kweli tunajua kabisa yatatufikisha kule tunapotaka kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Mipango ambayo tumekuwa tunajiwekea kuanzia 2011 - 2016 na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2020-2025, tumekuwa tunajinasibu na tunasema kwamba tunataka tuwe Taifa la uchumi wa katika by 2020-2025. Hata hivyo, mimi nikiwa mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara ninajiuliza jambo moja, hivi kweli tupo tayari? Ninajiuliza hivi kweli Serikali ipo pamoja? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu sioni inter-connection kati ya Wizara na Wizara. Kuna tatizo kubwa sana kwamba tumejinasibu sasa hivi kwamba tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda lakini ukiangalia Wizara hii inafanya jambo pekee yake na hii inafanya jambo peke yake. Kwa utaratibu huu hatuwezi kufikia malengo na matokeo yake viongozi hawa wakubwa, Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu tutakuwa tunawapa kazi kubwa sana, watakuwa kama vile ni Mawaziri wa Wizira zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano moja, kuna Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), mimi mpaka nawaonea huruma wale watendaji wa TIC kwa sababu yapo mambo ambayo yanatakiwa kufanywa na Serikali. Jamani, tunajinasibu kwamba tuwe na uchumi wa viwanda lakini tunashughulikia yale matatizo ambayo tunaona kabisa kwamba yanatukwamisha huko ambako tunataka kwenda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee to mfano, TIC iko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, kwanza naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa heshima kubwa itolewe chini ya Wizara hii. Kwenye nchi za wenzetu ambazo zimeendelea kituo hiki huwa kinakuwa chini ya Ofisi ya Rais au Ofisi Waziri Mkuu. Zamani kituo hiki kilikuwa chini ya Ofisi ya Rais, baadaye kikatolewa kikapelekewa chini ya Ofisi ya Waziri lakini baadaye kimepelekwa chini ya Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watu kazi yao ni kuratibu mamlaka zote za Serikali kwenye masuala yote yanayohusu uwekezaji. Hata hivyo, kama tunavyojua watendaji tulio nao Serikalini ni kweli wana mawazo yale ya uwekezaji? Zipo sheria kwa mfano Sheria za Uhamiaji mwekezaji akiwa ametoka nje ameingia hapa Tanzania ameleta mtaji wake mkubwa anakuja kuwekeza sheria inasema akiwa mwekezaji mkubwa kwa class A atapata kibali cha kuishi hapa kwa kipindi cha miaka 10. Akiwa kama ni mfanyakazi, labda ni mtaalam anapewea kibali cha miaka miwili, lakini kibali cha Uhamiaji kile cha ukaazi wa hapa, anatakiwa arudi kule kwao aje a-apply tena miaka miwili mingine baadaye tena arudi kwao aje apply mwaka mmoja. Hivi kweli mtu anakuja kuwekeza pesa zake nyingi, hii haipo sawasawa hata kidogo. Mimi nimekuja kuleta pesa zangu halafu ninyi mnaanza kuniambia eti kibali kikiisha inabidi uondoke, mbona ni vitu vidogo vidogo! Hawa watu ambao wapo kwenye Serikali kwa nini hawashughulikii vitu kama hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingine ni Sheria ya Kazi. Wote tunajua kwamba kama wewe ni mwekezaji umekuja hapa Tanzania maana yake ni kwamba unataka kuleta wataalam. Hata kama mimi Lucy Mayenga nataka kufungua ofisi, nataka nitafute mtaalam toka nje, nikimtafuta yule mtu kuja kumleta hapa, kwanza lazima tukubaliane kwa mfanyabiashara au kwa mwekezaji yeyote suala la kumleta mtaalam kutoka nje si kwamba wanapenda sana wakati mwingine ni kutokana na mazingira. Ndiyo maana nimefurahi sana kwamba michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge wanasema tuongeze uwekezaji na tuongeze usimamizi mkuu kwenye mafunzo ya ufundi. Hawa watu wakati mwingine wanaleta mtu si kwa maana pengine labda hapa anaweza kukosa mtu lakini sisi tunajali sana masuala ya vyeti na elimu za makaratasi, wenzetu wakati mwingine wanajali pia uzoefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unakuta Sheria ya Kazi mtu amekuja hapa kama mwekezaji lakini wakati huo huo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha ujaribu kuliangalia hili na uzuri Mheshimiwa Prof. Ndalichako, Waziri ambaye namwamini sana, naomba ulifanyie kazi jambo hili, vibali vya walimu wa international schools ambao wanatoka nje naomba Serikali ianze kuangalia sasa hivi havipo katika utaratibu ambao unaeleweka. Sasa mwekezaji amekuja mnamwambia karibu lakini hajui ampeleke mtoto wake shule ipi? Wenzetu hawa wanajali sana familia, hicho tu peke yake kinaweza kikamfanya akasema siwezi kukaa hapa kwa sababu elimu ya watoto wangu haipo sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria za Ardhi huko ndiyo kabisa! Mtu anakuja kama mwekezaji kutafuta eneo kwa ajili ya kuwekeza inamchukua takribani mwezi mzima wanazunguka tu kwa kuwa hatuna data base ya ardhi kwa ajili ya uwekazaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingine ni Sheria za Kodi. Ni lazima kama Taifa tuwe predictable. Haiwezekani kila mwaka tukikaa hapa tunakuwa na Public Finance Act, leo tunabadilisha hili, kesho linakaa hivi. Mwekezaji na mfanyabiashara yoyote anataka kuwa na uhakika na kodi anayolipa kwamba leo nalipa kodi hii, kesho nalipa hii, kesho kutwa nalipa hii siyo kwamba leo analipa hii lakini hajui kesho atalipa nini, ni vitu vigumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba kama Taifa na sisi kama Wabunge tukubaliane jambo moja, kuwa Mzungu au mtu anayetoka nje aidha ni Balozi au ni Mzungu mtaalam wa jambo lolote umekuja hapa tuheshimiane, hii ni nchi huru. Naiomba sana Serikali, mtu yeyote ambaye atakuja hapa akienda kinyume na utaratibu wa Taifa letu aondolewe saa 24. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ya kusema kwamba eti kwa sababu ni Mzungu, eti kwa sababu ni hivi, tunataka wale ambao watakuja wawe na malengo mema na sisi. Wawe na malengo mema kwamba mtu anakuja anasaidia, ni mdau kweli wa maendeleo. Siyo mtu anakuja anapiga blabla, mara anakwenda chini kwa chini anafanya mambo mengine, wengine wanajiingiza kwenye mambo ya siasa, tutakufukuza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho kabisa, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wangu, ni Rais ambaye kwa nafasi ya kipekee na naomba kwenye hili baadhi ya Mawaziri tuweze kukaa na kutega masikio yetu vizuri kuhusu utendaji wa Mheshimiwa Rais wetu. Wizara jamani acheni mambo ya kupeleka matatizo ya ndani ya Wizara zenu kwa Mheshimiwa Rais yashughulikieni ninyi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ahsante sana, naunga mkono hoja.