Parliament of Tanzania

Spika Ndugai azindua Kanuni za Kudumu za Bunge la Kenya kwa Lugha ya Kiswahili

Spika wa Bunge la Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai (Mb), amezindua Kanuni za Kudumu za Bunge la Kenya kwa Lugha ya Kiswahili katika halfa iliyofayika Jijini Nairobi, Kenya.


Hafla hiyo ambayo Spika Ndugai alikuwa Mgeni rasmi ilihudhuriwa pia na Spika wa Bunge la Kitaifa la Kenya, Mheshimiwa Justin Muturi; aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa, Mheshimiwa Francis Ole Kaparo, Viongozi wa walio wengi na walio wachache katika Bunge la Kenya; Waheshimiwa Aden Duale na John Mbadi, Makamu wa Spika, Mheshimiwa Moses Cheboi, Maspika wa Mabunge ya Kaunti za nchini Kenya na Wenyeviti wa Kamati za Bunge la Kenya.


Spika Ndugai aliwapongeza Wabunge wa Kenya kwa hatua hiyo, na kutoa wito kwa nchi nyingine za Bara la Afrika kuiga mfano huo wa kutumia lugha za Kiafrika katika kuendesha shughuli za Kibunge.


"Nawapongeza sana kwa hatua hii, na ningeomba Mabunge mengine yaweze kuiga mfano huu wa kutumia lugha zetu za Kiafrika," alisema Mhe. Ndugai.


Bunge la Kenya ndilo Bunge la pili duniani ( baada ya la Tanzania) kutumia lugha ya Kiswahili katika shughuli rasmi za Bunge.


Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Kenya, Mheshimiwa Justin Muturi alimshukuru Spika Ndugai kwa juhudi za Bunge la Tanzania katika kusaidia kutafsiri kanuni hizo kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili.


Uzinduzi wa Kanuni hizo kwa lugha ya kiswahili unatarajiwa kuboresha utendaji kazi wa Shughuli za Bunge la Kenya na pia kuwatia moyo wananchi kushiriki katika shughuli za kutunga sheria, kama ilivyo idhinishwa na sheria katika kifungu namba 118 cha Katiba ya Kenya.


Mbali na kuzindua kanuni hizo katika hafla hiyo Mhe. Ndugai pia alizindua mwongozo wa kazi za Kamati pamoja na taarifa za Kamati za Bunge la Kenya.


Katika hafla hiyo Mhe. Ndugai aliambatana pia na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Tanzania ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Naghenjwa Kaboyoka (Mb).

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's