United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
SPIKA wa Bunge,Mh. Job Ndugai amezindua Chama Cha Wabunge wa Kupambana na Rushwa (APNA-Tanzania) katika Bunge la Kumi na Moja huku akiwataka Wabunge kuhakikisha wanatekeleze majukumu yao kwa kufuata maadili.
Mh. Ndugai amesema katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano kila Mbunge ahakikishe anafanya kazi kwa maadili ya hali ya juu.
"Mnapofanya kazi ya kuishauri na kuisimamia Serikali msifanye hivyo kwa mashinikizo ya rushwa nyuma yake," amesema.
Aidha, amesema Bunge linatambua kazi inayofanywa na APNAC na kwamba linajitahidi kutoa msaada wa hali na mali kwa Chama hicho.
Amewataka wajumbe wa chama hicho pia kuhakikisha vyombo vinavyohusika na mapambano dhidi ya rushwa vinapatiwa bajeti ya kutosha.
Amesema yeye siku zote amekuwa mwanachama wa APNAC na ana imani wajumbe wa chama hicho watajifunza mambo muhimu kuhusiana na jinsi ya kupambana na rushwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mh. Angellah Kairuki amewataka Wabunge waendelee kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na sheria ya kuwalinda watoa taarifa iliyopitishwa na Bunge lililopita.
Amesema pia Serikali inatarajia kuifanyia marekebisho Sheria ya Rushwa ili adhabu zitakazotolewa ziendane na kosa.