Parliament of Tanzania

Ofisi ya Bunge yazindua Baraza la Wafanyakazi

Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai amewataka watumishi wa Bunge kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wafanye kazi kwa bidii.

Mhe. Spika alitoa rai hiyo kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Spika, Mhe. Dkt. Tulia Ackson alipokuwa anazindua Baraza la Wafanyazi la Ofisi ya Bunge lililofanyika katika Ofisi Ndogo za Bunge Tunguu Zanzibar.

Alisema kunahitajika mabadiliko katika utekelekezaji wa majukumu ya kila siku kwa watumishi katika kuchapa kazi ili kuleta utendaji kazi wenye tija na ufanisi.

Aidha, aliwataka wajumbe kupitia mada zitakazowasilishwa katika Mkutano huo wa Baraza kukumbuka wajibu wao katika kutelekeza majukumu waliyopewa kulingana na taaluma husika na hatimaye kufanikisha utekelezaji bora wa majukumu na madaraka ya Bunge Kikatiba.

Vilevile, alimpongeza Katibu wa Bunge, Ndugu Stephen Kagaigai kwa kufanikisha utatuzi wa changamoto ya muda mrefu ya muundo wa Ofisi ya Bunge ambayo hatimaye ufumbuzi umewezesha kuundwa kwa Baraza la Wafanyakazi.

“Naomba nitumie fursa hii kuwapongeza watumishi wote mlioteuliwa na Tume ya Utumishi wa Bunge kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi na ni matumini yangu kwamba mtatumia uwezo na karama mlizojaaliwa na Mwenyezi Mungu katika kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi hivyo kuliwezesha Bunge kufikia malengo yake,” alisema.

Aliwapongeza pia Wajumbe na Wawakilishi wa Idara na Vitengo kwa kuchaguliwa kushika nafasi hizo na kuwataka kutumia nafasi zao ili kuwa kiungo kati ya Wafanyakazi wa kada, ngazi zote, Menejimenti na Tume ya Utumishi wa Bunge.

Uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi ulihudhuriwa na Katibu Mkuu Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya, TUGHE Ndugu Hery Nkunda na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Ndugu John Mchenya ambao walinasihi Baraza kudumisha ushirikiano na kuongeza ufanisi katika ujenzi wa nchi.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Katibu wa Bunge Ndugu Stephen Kagaigai alisema Ofisi ya Bunge imeunda Baraza la Wafanyakazi baada kutokuwepo ya Baraza hilo katika kipindi kirefu kutokana na changamoto zilizokuwepo za kimuundo za Ofisi ya Bunge.

Alisema, lengo la Baraza lililopo kisheria ni kuboresha utendaji kazi wa taasisi kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na bila ya ugomvi wala mifarakano.

Kabla ya uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi, wajumbe walimchagua Ndugu Frank Mbilinyi kuwa katibu wa Baraza na Ndugu Felister Njovu kuwa Katibu Msaidizi

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's