Parliament of Tanzania

Ofisi ya Bunge yawapatia Wabunge tablets ili kusaidia kuondoa matumizi ya karatasi Bungeni

Ofisi ya Bunge imewapatia Waheshimiwa Wabunge tablets ambazo watazitumia katika shughuli za Bunge. Zoezi hilo limefanyika siku moja kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Kumi na Saba wa Bunge katika Ukumbi wa Pius Msweka Jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Katibu wa Bunge, Ndg. Stephen Kagaigai amesema kuwa hatua hiyo ya utoaji wa tablets itasaidia kuondoa matumizi ya karatasi katika shughuli za Bunge, kwa kuwa sasa Waheshimiwa Wabunge watakuwa wanapata nyaraka mbalimbali kwa njia ya mtandao kupitia tablets zao.

Aliongeza kuwa matumizi ya mtandao katika kuongoza Bunge yatasaidia kuokoa ghrama kubwa ambayo imekuwa ikutumika katika matumizi ya nyaraka za karatasi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bunge Mhe. Andrew Chenge alipongeza hatua ya Ofisi ya Bunge kutoa tablets kwa Waheshimiwa Wabunge akisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuleta ufanisi katika uendeshaji wa Bunge.

“Kwa hatua hii tunapaswa tuipongeze Ofisi ya Bunge kwa kuweze kukidhi haja ya Wabunge na kutimiza ahadi ya kuwapatia tablets na sasa dhana ya Bunge mtandao imetimia,” alisema Mhe. Chenge.

Nao baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walipongeza hatua ya Ofisi ya bunge kuwapatia tablets wakisema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji kwa vitendo matumizi ya mtandao katika uendeshaji wa shughuli za Bunge.

Waheshimiwa Wabunge wanatarajiwa kuanza kutumia kwa mara ya kwanza tablets walizopewa katika Mkutano wa Kumi na Saba wa Bunge utakaofanyika tarehe 5 hadi 15 Novemba, 2019 ambapo zitawasaidia kupata nyaraka mbalimbali ikiwemo; Orodha ya Shughuli za kila siku za Bunge, Ratiba ya vikao vya Bunge, Hotuba, Kauli za Mawaziri pamoja na nyaraka mbalimbali zitakazowasilishwa Bungeni.

Hatua ya kuwapatia Wabunge tablets ni muendelezo wa utekelezaji wa dhana ya Bunge Mtandao ambayo Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai aliasisi katika Mkutano wa Kumi na Sita alipotangaza usitishaji wa utoaji wa Orodha ya Shughuli za Bunge kwa njia ya makaratasi na badala yake akatangaza matumizi ya mtandao katika utoaji wa orodha hiyo.

Sambasamba na hilo, wakati wa Mkutano wa Kumi na Sita wa Bunge Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Bunge App na kusema kuwa safari ya uendeshaji Bunge kidigitali imeanzia hapo na itaendelea mbele katika kuhakikisha kuwa wanaachana na matumizi ya karatasi katika shughuli za Bunge.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's