United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
Naibu Spika wa Bunge, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb), amefungua kwa niaba ya Spika wa Bunge Mkutano wa vikao vya Jukwaa la Kibunge la Nchi za Maziwa Makuu (Forum of Parliaments of the Great Lakes Region- FP-ICGLR) katika Ofisi Ndogo za Bunge Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano
huo, Mhe. Zungu ametoa wito kwa
wakuu wa nchi za ukanda wa maziwa makuu, kudumisha umoja na amani kwa kuwa kwani
njia ndio njia kuu itakayosaidia katika kuwalinda raia na pia kukuza uchumi wa ukanda huo.
Alisema migogoro katika baadhi ya nchi za ukanda wa Maziwa Makuu una athari kubwa si tu kwa nchi husika lakini
pia kwa nchi jirani.
Aliongeza kuwa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia,
inaamini kuwa amani ndio msingi pekee
wa maendeleo.
“Wazo letu la msingi ni kwamba amani, usalama
na maendeleo haviwezi kutenganishwa, watu wetu wanaweza kufanikiwa iwapo nchi
itakuwa na amani,” alisema.
Alisema ustawi wa kiuchumi, kijamii na kimazingira
unahitaji kiasi kikubwa cha ushirikiano na uaminifu ndani ya jamii na bila amani na usalama hakuwezi kuwa na maendeleo
endelevu.
“Eneo letu hili la maziwa makuu tuna watu takribani
milioni 312 na tuna GDP ya bilioni 325 ni uchumi mkubwa sana. Tukiamua kuwa na
amani tutasaidia wananchi wetu, tukiamua kupigana watanufaika wanaoleta ugomvi,
wengi tuliobaki tutaumia,” alisema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jukwaa hilo, Balozi Onyango
Kakoba alisema ni wakati muafaka sasa kwa Viongozi wote wa kanda hiyo kufanya
kazi ya kusaidia kuleta amani Mashariki mwa Congo na Sudan kwani hali hiyo
inaleta athari kubwa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Jukwaa hilo lina nchi
wanachama 12 ambazo ni Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda, Angola,
Tanzania, DRC, Jamhuru ya Kongo, Jamhuri ya Kati, Zambia na Sudan.
Kamati za Jukwaa hilo zinazotarajiwa
kufanya vikao kwa nyakati tofauti ni Kamati ya Ulinzi na Usalama na Kamati ya
Demokrasia na Utawala Bora.