United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
MWONGOZO WA SPIKA ULIOOMBWA NA MHESHIMIWA ALLY SALEH ALLY, MBUNGE WA JIMBO LA MALINDI KUHUSU SWALI KUTOJIBIWA KIKAMILIFU KATIKA MAJIBU YA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA KWA SWALI LILILOULIZWA NA
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM, MBUNGE WA JIMBO LA MTAMBILE
MWONGOZO WA SPIKA
Waheshimiwa Wabunge, tarehe 27 Aprili, 2016 katika Kikao cha Sita cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Ally Saleh Ally (Mb) aliomba Mwongozo wa Spika kupitia Kanuni ya 68(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 kwamba, Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria wakati akijibu swali namba 59 la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Jimbo la Mtambile kuhusu uvunjaji wa Haki za Binadamu za Mashehe wa Zanzibar walio katika gereza la mahabusu la Segerea. Mhe. Ally Saleh Ally alieleza kuwa Mhe. Waziri wa Katiba na Sheria hakujibu swali hilo kikamilifu kwa mujibu wa Kanuni ya 46 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 hivyo kukiomba Kiti kueleza kama jambo hilo linaruhusiwa au haliruhusiwi Kikanuni.
Hoja ya msingi katika Mwongozo wa Spika ulioombwa ni kama kweli swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim (Mb) halikujibiwa kikamilifu? Na kama halikujibiwa kikamilifu, je jambo hilo linaruhusiwa?
Kanuni ya 46 fasili ndogo ya kwanza (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 inaeleza kuwa Mhe. Waziri anayetoa majibu anapaswa kujibu swali lililoulizwa kwa ukamilifu. Kanuni hiyo inaeleza:-
“46(1) Waziri anayeulizwa swali atakuwa na wajibu wa kulijibu swali hilo kwa ukamilifu kama lilivyoulizwa, isipokuwa kwamba, kama jibu linalohusika nirefu au linatakwimu nyingi, Waziri atampa Mbunge muuliza swali nakala ya jibu mapema baada ya kikao kuanza, kabla ya muda wa kujibu swali hilo haujafikiwa.”
Katika majibu ya Kiti kwa Mhe. Ally Saleh Ally baada ya kuomba Mwongozo, iliamuliwa kwamba, Kiti kitafanya rejea ya majibu ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria katika Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard) na baada ya hapo Mwongozo utatolewa.
Baada ya kupitia Hansard, nimeridhika kwamba majibu yaliyotolewa yalijitosheleza. Mheshimiwa Waziri alieleza kuwa, kazi ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na kwamba kama yapo malalamikohayo ya udhalilishaji na ukiukwaji wa haki za binadamu,vitendo ambavyo vinaelezwa kuwa Mashehe wanalalamika kuvipata, tayari yamepokelewa kwenye Tume. Mhe. Waziri aliendelea kueleza kuwa Tume itayashughulikia malalamiko hayo na itatoa taarifa ya Tume ambayo itawasilishwa bungeni kwa mujibu wa Ibara ya 131, Ibara ndogo ya (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya Mwaka 1977.
Ibara tajwa inaeleza bayana kuwa:
“131(3) Kila mwaka wa fedha Tume itatayarisha na kuwailisha kwa
Waziri anayesimamia haki za binadamu taarifa kuhusu:-
(a) …
(b) hali ya utekelezaji wa hifadhi ya haki za binadamu katika Jamhuri ya Muungano, na Waziri atawasilisha mbele ya Bunge kila taarifa iliyowasilishwa kwake na Tume mapema iwezekanavyo baada ya kuipokea.”
Kutokana na majibu hayo ya Mhe. Waziri na kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya Katiba niliyoinukuu, nimeridhika kuwa, swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim (Mb) lilijibiwakikamilifu kwa mujibu wa Kanuni ya 46 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016. Kama yapomalalamiko yoyote ya uvunjaji waHaki za Binadamu yaliyofanyika dhidi ya Mashehe waliopo gerezani yatashughulikiwa na Tume kama ilivyoelezwa.Ni vema ikasubiriwa taarifa itakayowasilishwa mbele ya Bunge kwa mujibu wa Katiba na hapo ndipo itajulikana hatua za kuchukua.
Huo ndio Mwongozo wangu.
Umetolewa Leo Tarehe………………………………………………..Mwezi Aprili, 2016
Dkt. Tulia Ackson (Mb)
NAIBU SPIKA