United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
MWONGOZO WA SPIKA KUHUSU SUALA LILILOOMBEWA MWONGOZO NA MHE. JOHN WEGESA HECHE KUHUSU USAHIHI WA MAJIBU YALIYOTOLEWA NA MHE. SELEMAN SAID JAFFO, NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS (TAMISEMI) WAKATI ALIPOKUWA AKIJIBU SWALI NAMBA 64 LILILOULIZWA NA MHE. ABDALLAH DADI CHIKOTA (MB.)
MWONGOZO WA SPIKA
Waheshimiwa Wabunge, Katika kikao cha Nane, Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mnamo tarehe 29 Aprili, 2016 Mheshimiwa John Wagesa Heche (Mb) alisimama na kuomba mwongozo kwa kutumia Kanuni ya 68(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 inayosomeka ifuatavyo:-
“68(7) Hali kadhalika, Mbunge anaweza kusimama wakati wowote ambapo hakuna Mbunge mwingine anayesema na kuomba “Mwongozo wa Spika” kuhusu jambo ambalo limetokea Bungeni mapema, ili Spika atoe ufafanuzi kama jambo hilo linaruhusiwa au haliruhusiwi kwa mujibu wa Kanuni na taratibu za Bunge na majibu ya Spika yatatolewa papo hapo au baadaye, kadri atakavyoona inafaa.”
Mwongozo Mhe. John Heche (Mb) ulieleza kuwa, wakati NaibuWaziri Ofisi ya Rais TAMISEMI anajibu swali la Mhe. Abdallah Dadi Chikota (Mb) kuhusiana na posho za wenyeviti wa vijiji na mitaa alijibu kiujumla bila kueleweka katika mambo ya msingi na bila kuangalia utofauti vipato vya Halmashauri.
Mhe. Chikota (Mb) katika swali la msingi namba 64 aliuliza kuwa, “Wenyeviti wa vijiji na mitaa wana majukumu mengi ikiwemo kuhakikisha kuwa ulinzi na usalama katika maeneo yao,Je! Lini Serikali itaanza kuwalipa posho ya mwezi wenyeviti hawa ili kutoa motisha ya kazi zao”
Swali hilo la msingi lilijibiwa na Mhe. Seleman Jafo (Mb), Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI. Kwa ufupi alieleza kuwa kila Halmashauri inatakiwa kurejesha katika vijiji na mitaa asilimia 20 ya mapato ya ndani. Sehemu ya fedha hizo inatakiwa kuwalipa wenyeviti wa vijiji na mitaa.
Baada ya majibu ya swali la msingi, Mhe. Abdalah Dadi Chikota (Mb) aliuza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza aliuliza kama ifuatavyo:-
“Asilimia 20 ni fedha ndogo inayopelekwa kijijini ikiwa vijiji vitaamua kuwalipa malipo wenyeviti wa vijiji na mitaa havitafanya kitu kingine, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kubeba jukumu hili la kuwalipa wenyeviti na mitaa?”
Mhe. Seleman Jafo Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Rais TAMISEMI alijibu swali hilo kama ifuatavyo;
”Kwanza ni kweli asilimia 20 ni ndogo na kama Halmashauri itawalipa wenyeviti wa vijiji na mitaa haitatosheleza kufanya kazi nyingine, ndiyo maana Serikali imeweka Specification katika bajeti ya mwaka huu, kwamba kila Halmashauri wakati ikipitia mchakato wa bajeti kuona inakidhi na jinsi gani itahakikisha mapato yake ya ndani kupitia vyanzo vya ndani mbalimbali ili mradi mwisho wa siku ziweze kupeleka fedha na ionyeshe ni jinsi gani itakusanya pesa za kutosha, lengo ni kwamba wenyeviti wa vijiji waweze kupata posho na pesa nyingine ziweze kufanya maendeleo ya kijiji”.
Swali linalotakiwa kujibiwa katika hoja ya Mhe. John Heche (Mb) ni kama Mhe. Seleman Said Jafo (Mb) Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –(TAMISEMI) alitoa majibu ambayo hayakueleweka au hayaridhishi wakati alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mhe. Abdallah Dadi Chikota (Mb).
Maswali ya Wabunge yanatakiwa kujibiwa kwa ukamilifu. Kanuni ya 46 fasili ndogo ya (1) inamtaka Waziri aliyeulizwa swali kujibu swali hilo kikamilifu. Kanuni tajwa inaeleza kama ifuatavyo:-
“46(1) Waziri anayeulizwa swali atakuwa na wajibu wa kulijibu swali hilo kwa ukamilifu kama lilivyoulizwa, isipokuwa kwamba, kama jibu linalohusika ni refu au lina takwimu ngingi, Waziri atampa Mbunge muuliza swali nakala ya jibu mapema baada ya kikao kuanza, kabla ya muda wa kujibu swali hilo haujafikiwa.”
Aidha Kanuni ya 45 fasili ndogo ya (3) imempa mamlaka Mhe. Spika ya kutathmini swali lililoulizwa kama limejibiwa kikamilifu na kama atajiridhisha kuwa swali hilo halikujibiwa kikamilifu ataagiza lijibiwe kwa ufasaha zaidi katika kikao kingine cha Bunge. Nanukuu:-
“45(3) Iwapo Spika ataridhika kuwa swali la msingi au la nyongeza halijapata majibu ya kuridhisha, ataagiza lijibiwe kwa ufasaha zaidi katika kikao kingine cha Bunge”.
Kwa mujibu wa Kanuni hiyo, ni dhahiri kuwa Spika atapima kama majibu yaliyotolewa na Waziri yanaridhisha au hapana.
Kwa mamlaka hayo, baada ya kupitia Taarifa Rasmi za Bunge kama nilivyozirejea mwanzoni mwa mwongozo huu, nimejiridhisha kuwa majibu yaliyotolewa kwa maswali yote, la msingi na nyongeza yanaridhisha na maswali hayo yalijibiwa kwa ufasaha kama yalivyoulizwa. Hivyo Kiti hakioni sababu ya kuchukua hatua yoyote.
Huu ndio Mwongozo wangu.
Umesomwa leo Tarehe……………………………Mwezi Mei, 2016
Dkt. Tulia Ackson (Mb)
NAIBU SPIKA