Parliament of Tanzania

Mkutano wa Kumi na Saba wa Bunge waanza Jijini Dodoma

Mkutano wa Kumi na Saba wa Bunge la Kumi na Moja, ambao ni mahsusi kwa ajili Bunge kukaa kama Kamati ya Mipango, umeanza siku ya Jumanne tarehe 05 Novemba 2019 na unatarajiwa kumalizika tarehe 15 Novemba 2019 Jijini Dodoma.


Mkutano huu umeanza huku kukiwa na mabadiliko makubwa ya matumizi ya Mtandao katika kuendesha shughuli za Bunge hii ikiwa ni baada ya Waheshimiwa Wabunge kupewa tablets kwa ajili hiyo.

Shughuli zitakazofanyika katika Mkutano huu ni kama ifuatavyo:-

1.0 KAMATI YA MIPANGO


Kwa mujibu wa Kanuni ya 94, katika mkutano wa Kumi na Saba Bunge litakaa kama Kamati ya Mipango kwa siku zisizopungua Tano(5) ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 63 (3) (c) ya Katiba inayolitaka Bunge likae kama Kamati ya Mipango ili kujadili na kuishauri Serikali kuhusu mapendekezo ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali wa Mwaka 2020/2021.


Kanuni ya 94 (4) inaelekeza kwamba, kabla ya mapendekezo ya Mpango husika kuwasilishwa Bungeni yatajadiliwa kwanza na Kamati ya Bajeti, jambo ambalo tayari limeshafanyika.


2.0 MASWALI

Katika Mkutano huu wa Kumi na Saba, wastani wa maswali 125 ya Kawaida yanatarajiwa kuulizwa na Wabunge. Aidha, wastani wa Maswali 16 ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu yanatarajiwa kuulizwa kwa siku za Alhamisi tarehe 7 Novemba, na 14 Novemba, 2019.


3.0 MISWADA YA SERIKALI

Bunge pia litarajia kujadili na kupitisha Muswada ya Sheria ya marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 7) ya mwaka 2019 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 7) Bill, 2019] ambao utasomwa kwa hatua zote Tatu.


Aidha, Miswada miwili itawasilishwa na serikali kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya Kwanza katika mkutano huo. Miswada hiyo ni:-


a) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mbalimbali (Na.8) Mwaka 2019 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 8) Bill, 2019].


b) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kilimo na Mazao wa Mwaka 2019 (The Agricultural and Crop Laws Miscellaneous Amendment Bill, 2019).


4.0 MAAZIMIO

Katika Mkutano wa Kumi na Saba wa Bunge, jumla ya Maazimio Saba (7) yanatarajiwa kuwasilishwa na Serikali Bungeni:-


1.Azimio la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama (Agreement on Port Measures to Prevent, Deter and Eliminate Illegal, Uneported and Unregulated Fishing-PSMA);


2. Azimio la Kuridhia Kuanzishwa kwa ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (Framework Agreement on the Establishment of the International Solar Alliance-ISA);


3. Azimio la Kuridhia Marekebisho ya Kigali kuhusu kupunguza Uzalishaji na Matumizi ya Kemikali Jamii ya Hydrofluocarbons (HFCS) chini ya Itifaki ya Montreal inayohusu Kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni (Kigali Amendment on Phasing Down Hydrofluocarbons (HFCs to the Montreal Protocol on Ozone Depleting Subsatnces);


4. Azimio la kuridhia Itifaki ya SADC kuhusu Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo Endelevu (The Southern African Development Community Protocol on Environmental Management for Sustainable Development);


5. Azimio la Kuridhia Itifaki ya Kinga na Maslahi ya Kidiplomasia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) (Protocol on Privileges and Immunities of East African Community);


6. Azimio la Kuridhia Itifaki ya Afrika Mashariki ya Mitandao ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (EAC Protocol on ICT Networks);


7. Azimio la Kuridhia Itifaki ya Marekebisho ya Mkataba wa Marrakesh ulioanzisha Shirika la Biashara la Dunia (Protocol Amending the Marrakesh Agreement Establishing the World Trade Organazation-WTO).


Bofya hapa kupata ratiba yote ya Mkutano huu

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's