United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeahirishwa hadi tarehe 28 Januari, 2020.
Bunge limeahirishwa baada ya kumalizika kwa Mkutano wake wa Kumi na Saba uliofanyika tarehe 05 hadi 15
Novemba, 2019 Jijini Dodoma.
Mkutano
Kumi na Saba wa Bunge ulishuhudia mabadiliko makubwa ya matumizi ya Mtandao
katika kuendesha shughuli za Bunge hii ikiwa ni baada ya Waheshimiwa Wabunge
kupewa tablets kabla ya kuanza kwa mkutano huo.
Pamoja na shughuli nyingine za
Kibunge, Mkutano wa Kumi na Saba Bunge ulikuwa mahususi kwa Bunge kukaa kama
Kamati ya Mipango kwa siku takribani Tano (5) kujadili na kuishauri Serikali kuhusu
mapendekezo ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa
kutekelezwa na Serikali wa Mwaka 2020/2021.
Aidha, katika mkutano
wa Kumi na Saba, Bunge pia lilijadili
na kupitisha Muswada ya Sheria ya marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 7) ya
mwaka 2019 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 7) Bill, 2019]
mara baada ya kusomwa kwa hatua zote Tatu.
Mbali na hayo, Bunge pia katika Mkutano wake wa Kumi
na Saba wa Bunge, lilijadili na kuridhia Maazimio saba ya Kimataifa pamoja na
Azimio la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli kwa utendaji uliotukuka kwa kipindi cha miaka minne ya
Uongozi wake na pia Azimio la kumpongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mheshimiwa Job Y. Ndugai, kwa uamuzi wake wa kulifanya Bunge
kutekeleza kwa vitendo dhana ya Bunge Mtandao (e-Parliament).
Akitoa Hotuba ya
Kuahirisha Bunge, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alisema Mpango wa Maendeleo
wa Taifa wa 2020/2021 umelenga kutekeleza
maeneo ya kipaumbele ikiwa ni pamoja na kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu kwa kuweka mkazo
katika upatikanaji wa huduma bora za jamii ikiwemo elimu, maji, afya, umeme na
barabara.
Mhe. Majaliwa
aliongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli itaendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta zinazogusa wananchi
moja kwa moja na kuhakikisha
kuwa matunda ya kukua kwa uchumi yanawafikia wananchi.
Aidha, amewaasa Watanzania kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, katika kipindi hiki ambacho amekuwa akichukua hatua za makusudi kuhakikisha anajenga uchumi imara, kuboresha kipato na hali ya maisha ya wananchi.