Parliament of Tanzania

Azimio la Bunge la Kumpongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

AZIMIO LA BUNGE LA KUMPONGEZA MHE. SAMIA SULUHU HASSAN KUWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

(Kanuni ya 61 (1) ya Kanuni za Bunge Toleo la Juni, 2020) _______________________

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 61 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Juni, 2020, naomba kuwasilisha Hoja kwamba, Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Azimio la Kumpongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue nafasi hii kukushukuru wewe binafsi kwa kunipatia fursa hii adhimu ya kuwasilisha Hoja ya Azimio hili;

Mheshimiwa Spika, naomba pia kutumia nafasi hii kumpa pole Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kifo cha Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi, 2021 Jijini Dar es Salaam. Hakika huu ni msiba mkubwa kwetu sote Watanzania, ila kwake yeye ni msiba mzito zaidi;

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ibara ya 47 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Makamu wa Rais ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Jamhuri ya Muungano kwa jumla. Ni wazi kwamba mafanikio ya Serikali chini ya uongozi wa Rais yeyote yanatokana na ushirikiano wa Rais huyo na Makamu wake. Kwa mantiki hii, mafanikio ya uongozi wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli yana mkono wa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa walifanya kazi bega kwa bega.

Mheshimiwa Spika, kuapishwa kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kunawezesha muendelezo wa mafanikio yaliyopatikana. Aidha, uzoefu wake katika nafasi za uongozi, Utumishi wa Umma na Taasisi za Kimataifa unatoa matumaini kwamba Tanzania itaendelea kufanikiwa zaidi;

Mheshimiwa Spika, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameitumikia nchi hii katika nafasi mbalimbali za uongozi, miongoni mwa nafasi hizo ni pamoja na zifuatazo:-

 Mwaka 2015 – 2021 alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;  Mwaka 2014 alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;  Mwaka 2010 – 2015 alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;  Mwaka 2010 – 2015 alikuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jimbo la Makunduchi;  Mwaka 2000 – 2005 alikuwa Waziri wa Vijana, Ajira, Maendeleo ya Wanawake na Watoto na baadaye Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;  Mwaka 2000 – 2005 alikuwa Mwakilishi wa Viti Maalum katika Baraza la Wawakilishi; na  Mwaka 2011 mpaka sasa amekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, ukiondoa nafasi hizi alizowahi kushika Kitaifa na Kimataifa, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kipindi chote alichohudumu kama Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa akimuwakilisha Rais katika Mikutano na Matukio mbalimbali katika Taasisi za Kimataifa na nchi za nje.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo haya ni dhahiri kwamba Mhe. Samia Suluhu Hassan ana uzoefu wa kutosha, weledi na uwezo wa kuendeleza kazi nzuri za Rais wa Tano Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa niwasilishe Azimio la Kumpongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ifuatavyo:-

KWA KUWA, Mhe. Samia Suluhu Hassan sasa ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

KWA KUWA, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshika nafasi mbalimbali za uongozi katika nyanja tofauti nchini hivyo kuwa na uzoefu, uhodari, uthubutu na uwezo wa kuendeleza kazi nzuri za Rais wa Tano Dkt. John Pombe Joseph Magufuli;

KWA HIYO BASI, Bunge hili katika Mkutano wake wa Tatu, Kikao cha Kwanza, tarehe 30 Machi, 2021, linaazimia kwa dhati na kauli moja:

(a) Kumpongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na

(b) Kumuunga mkono katika majukumu yake ya kazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumuombea afya njema, baraka na ulinzi wa Mwenyezi Mungu katika kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Joseph Kizito Mhagama, Mb. MBUNGE WA MADABA

30 Machi, 2021

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament