Parliament of Tanzania

MHE. SPIKA AWAAPISHA WABUNGE WAWILI WATEULE WA MHE. RAIS, ATOA ONYO KWA WANAOKEJELI SHUGHULI ZA KIBUNGE

SPIKA wa Bunge Mhe. Job Ndugai amewaapisha Waheshimiwa Wabunge wawili wateule, Humprey Polepole na Riziki Said Lulida ambao wameteuliwa hivi karibuni na Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli katika tukio lililofanyika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha Wabunge hao, Mhe. Spika alitoa onyo kwa baadhi ya wanasiasa wanaokejeli shughuli za Bunge.

Alieleza utaratibu wa Kikanuni unaowezesha wabunge wapya kuapishwa katika kipindi ambacho hakuna Mkutano wa Bunge jambo ambalo linawawezesha waaanze kutekeleza majukumu yao ya kibunge mapema.

Alisema kwa utaratibu wa zamani wabunge hao hawakutakiwa kufanya kazi za kibunge hadi wakati wa Mkutano wa Bunge wa Februari mwakani wakati watakapoapishwa.

Alisema utaratibu huu mpya uliotokana na maboresho ya Kanuni za Kudumu za Bunge siyo wa kwanza kwa Bunge la Tanzania na kwamba baadhi ya mabunge ya nchi nyingine yamekuwa yakifanya hivyo ikiwemo baadhi ya Nchi za Jumuiya ya Madola.

“Kufikiri kwamba Bunge ni Ukumbi wa Bunge pekee ni fikra finyu sana, kauli zinazotolewa na upinzani zisiwayumbishe Watanzania, ndiyo maana hata mahakama inaweza kwenda kusikiliza kesi na kutoa hukumu sehemu yoyote hata chini ya miti,” alisema.

Aidha, Mhe. Spika alisisitiza kwamba waheshimiwa wabunge wote 20 wa Chadema wakiwemo wa Viti Maalum 19 na wa Jimbo mmoja walioapishwa wanatambulika kuwa ni wabunge halali na kutaka wasisumbuliwe.

Aliwaonya pia viongozi wa baadhi ya vyama vya upinzani wanaowanyanyasa wanawake hususani wabunge 19 wa Viti Maalum wa Chadema na kuwataka Watanzania wote kupiga vita ukandamizaji dhidi ya wanawake hao katika jamii kwa kisingizio chochote kile.

Mheshimiwa Spika aliahidi pia kuwapanga Waheshimiwa Wabunge katika Kamati za Kudumu za Bunge hivi karibuni.

Akizungumza mara baada ya kuapishwa, Mheshimiwa Polepole alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua na kuahidi kuwa mwaminifu na mtiifu pamoja na kuweka maslahi mapana ya Taifa mbele.

Kwa upande wake Mheshimiwa Riziki alimshukuru Dkt. Magufuli kwa imani aliyoonyesha kwake huku akiahidi kufanya kazi kwa moyo wake wote ili kuhakikisha anarudisha fadhila kwa watanzania.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament