United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
SPIKA wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai amewaapisha Waheshimiwa Wabunge wawili walioteuliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli Desemba 5 mwaka huu.
Wabunge hao walioapishwa katika Viwanja vya Bunge Jijini
Dodoma ni Dkt.Dorothy Gwajima na Mhandisi Leonard Chamuriho.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha wabunge hao,
aliwapongeza kwa uteuzi na kuahidi kuwapa ushirikiano huku akiwataka Wabunge
wote waliapishwa kuendelea na shughuli zao popote walipo.
Aidha, alimpongeza Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar,
Mheshimiwa Maalim Seif Sharrif Hamad kwa kuapishwa kutumikia nafasi hiyo huku
akisema uapisho huo unadhihirisha yale yaliyoelezwa na Rais Magufuli kuwa
uchaguzi umekwisha.
Mheshimiwa Spika pia alizungumzia maneno yanayozungumzwa na
baadhi ya watu kwamba amefanya kosa kuwaapisha Wabunge wa Viti Maalum 19 kutoka
Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema).
Alisema yeye kazi yake ni kuapisha Wabunge wote ambao
analetewa majina yao kutoka Tume ya Uchaguzi (NEC) na ameshafanya hivyo na
kwamba kama kuna walakini Mahakama ndiyo inaweza kumuambia hatua za kuchukua na
si vinginevyo.
Awali akimkaribisha Mheshimiwa Spika, Naibu Spika,
Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson aliahidi kuwa Bunge litawapa ushirikiano Wabunge
Wateule ili waweze kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika pia alimpongeza Mheshimiwa Ndugai kwa
kazi kubwa anayoifanya ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya sheria ambazo zimekuwa
zinawanufaisha Watanzania.
Naye Dkt. Gwajima alisema amepokea uteuzi alioufanya Rais kwa uaminifu na kwamba
anatambua kazi iliyo mbele yake ni kubwa, ni kazi inayotaka uzalendo, ujasiri,
umakini na ushirikiano.
Kwa upande wake Dkt. Chamuriho alisema anatambua majukumu
aliyopewa ni makubwa na mazito hivyo anaomba ushirikiano ili aweze kuyatekeleza
kama inavyotarajia kwa uaminifu, uadilifu na kwa kuwaajibika.