Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stella Simon Fiyao

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa Hati kwa maeneo yote ya Umma katika Halmashauri za Mkoa wa Songwe?

Supplementary Question 1

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niwe na maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Swali langu la kwanza, Taasisi nyingi za Umma zimejikita katika kutoa huduma na hazifanyi biashara: Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka kuondoa kodi ya ardhi ili kuziwezesha taasisi nyingi kuweza kupata hati? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, nataka kujua: Ni lini Serikali itakamilisha kutoa hati katika maeneo 787 yaliyosalia katika Halmashauri za Mkoa wa Songwe ili yaweze kupatiwa hati na kuepusha migogoro ya ardhi isiyokuwa na ulazima baina ya wananchi na Serikali? Nakushukuru sana. (Makofi)

Name

Geophrey Mizengo Pinda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu hizi Taasisi za Umma kuziondolea kodi, hili tumelichukua na tutakwenda kulichakata na kuona namna nzuri ya kufanya. Mara nyingi sana taasisi zinazoomba kumilikishwa maeneo haya zinakuwa na makusudio maalum pamoja na miradi maalum. Kwa hiyo, kwao inakuwa ni rahisi sana kutumia vyanzo vyao vidogo kwa ajili ya kumilikishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la lini maeneo yaliyobaki katika Mkoa wa Songwe yatakwenda kukamilishiwa umilikishwaji wake? Niwaombe hizo taasisi kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, waanze mchakato wa kuomba namna ya umilikishwaji. Hatua zote ziko wazi na taasisi hizo zote zinaelewa utaratibu ambao tumejiwekea katika uratibumzima wa kumilikisha ardhi hapa nchini.

Name

Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Primary Question

MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa Hati kwa maeneo yote ya Umma katika Halmashauri za Mkoa wa Songwe?

Supplementary Question 2

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Je, ni lini Wizara ya Ardhi itaingilia kati kutusaidia kutatua migogoro iliyopo ndani Kata ya Kapele kwa kuwafuatilia watu wote ambao wamehodhi na kupora maeneo ya wananchi kinyume na utaratibu bila kuwa hati na wengine kuwa na hati za uwongo kwa kigezo na kusingizia wametumwa na wakubwa huko juu? Ni lini Wizara ya Ardhi mtatusaidia kutatua jambo hili?

Name

Jerry William Silaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukonga

Answer

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Nina nyongeza ndogo kwenye majibu hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa kuzungumza, naomba dakika moja kutoa shukrani. Kwanza, namshukuru sana Mwenyezi Mungu ambae amenipa kibali kuhudumu kwenye Wizara hii ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniteua kuhudumu na kumsaidia kama Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Ninachoweza kumuahidi ni utumishi uliotukuka wa uadilifu. Nitatumikia kwa nguvu zangu na akili zangu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaliomba Bunge lako tukufu ushirikiano na wakati wote nitakuwa tayari kwa ajili ya kufanya kazi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa nyongeza ndogo ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Serikali imejipanga na lipo suala la migogoro ya ardhi. Serikali kupitia Kamati ya Mawaziri Nane ilishafanya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwenye vijiji 975.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutumia fursa hii kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa 26 yote ya nchi nzima, kuendelea na utekelezaji wa maagizo ya Baraza la Mawaziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwaahidi Waheshimiwa Wabunge ambao wengi tumekutana na wameelezea kero zao akiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Momba, Mheshimiwa Condester. Baada tu ya Bunge hili kuna mkutano wa Kimataifa Arusha na unaisha Alhamisi, tutajipanga kuanza ziara nchi nzima kutekeleza maagizo ya Baraza la Mawaziri kwenye vijiji 975. Vilevile, kutatua migogoro yote ambayo inajitokeza kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ushirikiano. Ahsante sana. (Makofi)