Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya mchepuko kwa kiwango cha lami kutoka Mpemba kupitia Chapwa Mwakakati katika Mji wa Tunduma kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninashukuru kwa majibu mazuri lakini kuna changamoto ambayo ipo.

Mheshimiwa Spika, hii barabara tunayoiongelea hapa ni barabara ambayo ni ahadi ya Hayati Mheshimiwa Rais Magufuli na pia kumekuwa na barabara nyingine ya Chapwa, Chindi, Msangano ambayo hii ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja Songwe tarehe 06 Julai, 2020. Ninataka kufahamu kwa nini ahadi za Viongozi hazitekelezeki kwa wakati?

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto nyingine ambayo ipo ya ujenzi hafifu wa barabara za lami kwa TARURA. Ninataka kufahamu ni kwa nini barabara zao haziwi na ubora, mfano mzuri uko katika Jiji lako la Mbeya utaona barabara ya Kabwe – Isanga, barabara ya Mafiati - Airport, barabara ile ya kutoka njiapanda ya Ilonda kwenda Isyesye ni barabara zinazoharibika kabla ya muda.

Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu ni kwa nini barabara zao zinakuwa hazina ubora? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa ya Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi zote za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ni kipaumbele katika utekelezaji wake na Serikali imekuwa ikitekeleza ahadi za viongozi kwa awamu kwa sababu ziko nyingi, kwa hiyo kadri ya fedha zinavyopatikana ahadi zile zinatekelezwa. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba ahadi hii ya Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kipaumbele na Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji. Ndiyo maana katika bajeti ijayo itatenga Bilioni Moja na Milioni Mia Tano kwa ajili ya kuanza utekelezaji huo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara za lami za TARURA barabara zetu za lami za kipindi cha nyuma kabla ya 2022 zilikuwa zinajengwa kwa maana ya kubeba uzito wa chini ya tani 10 hadi 15, baada ya kuona siyo rahisi ku-control magari yenye uzito mkubwa Serikali kupitia TARURA tumeborsha sasa tunakwenda tani 30 na kuendelea. Kwa hiyo sababu ya kuonekana barabara zile zilikuwa ni dhaifu ni kwa sababu zilikuwa zinajengwa kwa kiwango cha tani 10 lakini magari mazito zaidi yaliweza kupita, tunaamini sasa hatutakuwa na changamoto hiyo kwa sababu tumeboresha mfumo huo. Ahsante. (Makofi)

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya mchepuko kwa kiwango cha lami kutoka Mpemba kupitia Chapwa Mwakakati katika Mji wa Tunduma kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 2

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya kutoka Jimboni kwako Mheshimiwa Waziri Wanging’ombe kuelekea Lupira, kwa maana Kipengere - Lupila na barabara ya Esaprano. Barabara hizi ni za kiuchumi lakini zimekuwa zikisumbua kwa muda mrefu.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Richard Sanga Mbunge wa Jimbo la Makete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mbunge jirani yangu amekumbusha suala la msingi na tayari nimhakikishie kwamba kwenye bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI suala hilo ni kipaumbele kujenga barabara kutoka kipengere kuelekea kule Lupila na itatekelezwa, ahsante. (Makofi)