Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. FESTO R. SANGA aliuliza: - Je, nini mkakati wa Serikali kuondoa changamoto ya Lumbesa kwa wakulima wa zao la viazi nchini?

Supplementary Question 1

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kutokana na majibu ya Serikali, kwa kuwa suala la kutoa elimu kwa wananchi limekuwa likifanyika mara kwa mara, lakini halijawa na tija ya kutibu tatizo la lumbesa. Ni upi mkakati wa Serikali kusimamia Sheria ya Vipimo, Sura 340, kuhakikisha kwamba suala la lumbesa linaisha kabisa nchini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali haioni ni wakati muafaka kati ya Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara kuanzisha selling point ili kuwekwe mizani katika maeneo hayo ili kudhibiti suala la lumbesa nchini kwenye mazao ya viazi, vitunguu na mazao mengine ambayo yamekuwa msiba kwa muda mrefu kwa mkulima ambaye amekuwa akinyonywa kwenye Taifa letu?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Festo Sanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli moja ya changamoto tuliyonayo ni usimamizi wa kutekeleza hii Sheria na mkakati uliopo ni kupitia wenzetu Serikali za Mitaa kwa maana TAMISEMI, kuhakikisha wanasaidia kwanza maeneo yale ambayo kuna mauzo kuwe na mizani ambayo itatumika kuhakikisha wale wote wanaonunua wanapima au wananunua kwa uzito.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ambalo nalo linaendana na hili ni kwamba, hiyo ndiyo mikakati ya Serikali ambayo tunataka sasa tuhamasishe wananchi kujiunga katika vyama vya msingi au kuimarisha ushirika katika maeneo ya mashambani ili waweze kuwa na uwezo au nguvu ya ku-bargain. Moja, ili wapate bei nzuri na pili, ili sheria hii iweze kutumika ni lazima wawe na maeneo ya kuuzia.

Kwa hiyo, mpango uliopo kupitia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara vile vile Kilimo na wenzetu wa TAMISEMI ni kuona tunawa-organize sasa wakulima wale wawe na maeneo mahususi ya kuuzia mazao yao ili tuwapatie uwezeshaji wa kuwa na vipimo, kwa maana ya mizani lakini pia wawe na nguvu ya kudai bei stahiki ya mazao yao. Nakushukuru.

Name

Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FESTO R. SANGA aliuliza: - Je, nini mkakati wa Serikali kuondoa changamoto ya Lumbesa kwa wakulima wa zao la viazi nchini?

Supplementary Question 2

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Pamoja na uwepo wa hiyo sheria Mheshimiwa Waziri aliyotuambia, lakini ni dhahiri kwamba watumishi tulionao hawatoshi, lakini pili miundombinu siyo rafiki. Huko vijijini ambako ndiko wakulima waliko, wakulima wetu wa mazao mbalimbali nchini wamekuwa wakiuza kwa lumbesa kwa sababu tu kwanza mtu anayeratibu ni wafanyabiashara kwa maana ya madalali, ndio wanaopanga wakulima wetu wauzaje na kwa uzito upi. Je, Serikali haioni sasa muda umefika kwa wafanyabiashara wa mazao kutoa maelekezo wanapokwenda vijijini kununua mazao, waende na mizani na wananchi wetu wapewe maelekezo pia na elimu kwamba wasiuze kwa mfumo wa lumbesa?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti Majala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna changamoto ya watumishi katika maeneo yote ikiwemo hili la Wakala wa Vipimo kwa maana ya wanaosimamia mambo ya vipimo. Kwa kweli kazi kubwa inafanyika kwa kushirikiana na halmashauri kuhakikisha tuna washirikisha Maafisa Biashara ambao ndio wanaowasadia na pia Maafisa Ugani ambao wako katika maeneo hayo ili kuhakikisha tunawalinda wakulima katika maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, sio katika lumbesa tu, kwa sababu lumbesa kama alivyouliza muuliza swali la msingi kwenye viazi, lakini pia hata katika maeneo mengine ambako wanatumia vitu kama ndonya, kangomba, bakuli na vitu kama hivyo. Kwa hiyo tunajitahidi kuhakikisha Maafisa Biashara na Maafisa Ugani hawa wanawasaidia wakulima ili kuhakikisha kwamba wanakuwa na maeneo ya kuuzia ambako watawasaidia.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwaelekeza Maafisa Biashara ambao tumekwishawapa nafasi ya kuwa wafanyakazi pia katika Idara za Uwekezaji, Viwanda na Biashara, wasaidie na wasimamie hili suala ili tuondokane na unyonyaji huu unaotumika wa kunyonya wakulima kwa kununua katika vifungashio au bila kutumia vipimo katika maeneo ya mashambani ili tuondokane na masuala haya ya lumbesa.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.