Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: - Je, ni lini utekelezaji wa Mkataba wa kibiashara kati ya Serikali na Kampuni ya Dubai World utaanza?

Supplementary Question 1

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri na bora kabisa ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa sisi tayari tunalo eneo letu la kibiashara: Je, ni kwa kiasi gani Serikali imejiridhisha juu ya uwezo wa ufanisi na uwezo wa mtaji wa Kampuni ya DP World ili kuja kuongeza soko katika bandari zetu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kwa kiasi gani Serikali imejiridhisha uwezo wa kuweza kuongeza ushindani kwa kuwa tayari tunazo Bandari za Beira (Msumbiji), Mombasa (Kenya), na Durban (South Africa) ambazo tunashindana nazo? Mmepima uwezo wa DP World kuja kuongeza ushindani katika eneo hili la ukanda wa SADC na ukanda wa Afrika Mashariki?

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali pasi na shaka imejiridhisha kwamba DP World Port ina uwezo wa kuendesha bandari zetu nchini hususan Bandari yetu ya Dar es Salaam. Tumejiridhisha kwa maana ya kwamba, kwanza, inafanya kazi katika mataifa yasiyopungua 69 duniani, na pia wataalamu wetu wametembelea mataifa hayo ikiwemo Uingereza, Canada, India, Dubai kwenyewe na mataifa mengine.

Mheshimiwa Spika, vile vile Bandari hii ya Dar es Salaam hivi sasa inapata wateja wake kwa njia ya mfanyabiashara kuleta meli yake, lakini kupitia DP World, wao wana connection, au mtandao mpana wa kibiashara huko duniani, kwa hiyo, watatutafutia masoko. Zaidi ya yote, wamejenga bandari kavu katika nchi ambazo tunahudumia kama Taifa hususan kule Congo pamoja na Rwanda.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge anataka kujiridhisha kuhusu ushindani na uwekezaji ambao atafanya DP World. Ni kweli kwamba ushindani katika bandari zetu ni mkubwa hususan katika ukanda wetu wa Bahari ya Hindi. Tuna Mombasa, ni washindani wetu; tuna Beira (Msumbiji), pamoja na Durban (Afrika Kusini). Kupitia DP World, Bandari ya Dar es Salaam, itaongeza ufanisi kwa ushindani kwa sababu kwanza ataleta vifaa na vyombo vya kisasa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mifumo ambayo tumekuwa tukizungumza miaka mingi katika Bandari yetu ya Dar es Salaam ili taasisi zionane kupitia mifumo ya electronic single window system, pia itawekezwa na itakuwa automated ili kuongeza ufanisi. Sasa hivi ukienda bandarini utakuta meli ni nyingi lakini muda wa kupakua na kushusha mizigo ni mrefu. Hili ndilo tunataka sasa tuongeze ufanisi kwa kupunguza huo muda ili Bandari yetu ya Dar es Salaam iendane na ushindani wa bandari hizi nyingine ambazo nimezitamka.

Mheshimiwa Spika, tunakushukuru. (Makofi)