Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kasuku Samson Bilago

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Buyungu

Primary Question

MHE. KASUKU S. BILAGO aliuliza:- Kifungu cha 3 cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, na Kifungu cha 1(26) cha Kanuni za Kudumu za mwaka 2009 vinatoa tafsiri ya neno mwajiri kuwa ni mtu au taasisi ambayo mtumishi wa umma anaingia naye mkataba wa ajira na kumlipa mshahara. Je, kwa kuzingatia tafsiri hiyo, mwalimu ambaye ni mtumishi wa umma, mwajiri wake ni nani?

Supplementary Question 1

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, asante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa Waziri mwenyewe amekiri katika majibu yake ya swali la msingi kwamba ajira ya walimu imekasimiwa kwenye mamlaka zingine, na mamlaka zilizokasimiwa ajira za walimu ndizo zimesababisha matatizo makubwa ya walimu, walimu kutopanda madaraja kwa wakati, walimu kutolipwa mishahara mizuri na walimu kutolipwa madai yao kwa muda mrefu sana.
Je, Waziri yuko tayari hii Tume iliyoundwa namba 25 ya mwaka 2015 iwe na mamlaka kamili ya kuwaajiri na kulipa mishahara bila kukasimiwa kwenye mlolongo wa vyombo vingine?
Swali la pili, kwa kuwa matatizo yaliyosababishwa ya walimu nchini yametokana na mfumo kwa kukasimu mamlaka ya ajira ya walimu kwa vyombo vingine vingi kuanzia Katibu Kata, Mratibu, TSD, Utumishi, Hazina na kadhalika, vyote vinavyoleta usumbufu kwa ajira ya mwalimu na maslahi yake kupotea.
Je, Serikali iko tayari kuwahudumia walimu kwa dharura kabisa kulipa madai yao yanazidi shilingi bilioni 20 kwa dharura ya haraka ili walimu hao waweze kufanyakazi kwa moyo? Asante

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwalimu Bilago ametaka kujua kama Serikali iko tayari kuipa Tume ya Utumishi ya Ualimu mamlaka kamili ya kulipa mishahara. Niseme tu kwamba ukiangalia katika kifungu cha 5 kinachoanzisha Tume hii ya Utumishi wa Walimu, Mamlaka kwa Tume hii ni Mamlaka ya ajira. Bado suala zima la kulipa mishahara kama ilivyo Kanuni ya Utumishi wa Umma na kama wanavyolipwa watumishi wote wa umma itabaki katika Serikali. Lakini ukiangalia kama Mamlaka ya Usimamizi kwenye Serikali za Mitaa, ambao ndio wanaendesha na wenye shule uko chini, wao wanachokifanya ni kulipa tu mishahara kwa kuwa wao ndiyo mamlaka ya usimamizi, kwa hiyo tutaendelea hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba pamekuwa na changanmoto ambazo tunazitambua kwa kuanzisha Tume hii tunaamini sasa kwa kuwa ni Tume ambayo inajitegemea, maana ukiaangalia huko awali Idara ya Walimu ilikuwa chini ya Utumishi wa Umma, lakini Tume hii mpya ambayo tunayoianzisha itakuwa ni Tume inayojitegemea na tunaamini sisi kama Serikali kwa kuwa tumejipanga kuiwezesha kwa rasilimali fedha, kuiwezesha kwa rasilimali watu na vitendeakazi mbalimbali tunaamini changamoto mbalimbali ambazo zilijitokeza basi zitaweza kutatuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge aweze kuwa na imani, tuweze kuanza Tume hii halafu tuone mambo yatakavyojitokeza lakini sisi kama Serikali tuko tayari kuiwezesha Tume hii kwa hali na mali. Ukiangalia katika mahitaji ya kibajeti yaliyobainishwa ni takribani shilingi bilioni 75, wakati ukiangalia ni ilipokuwa ni Idara ya Utumishi wa Walimu walikuwa wanategemea bajeti yao kutoka katika Tume ya Utumishi wa Walimu, ndiyo maana changamoto mbalimbali za kupandishiwa mishahara, changamoto za kupandishwa madaraja na mambo mengine yalikuwa zinajitokeza. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aiamini Serikali, tuipe nafasi Tume iweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili kuhusiana na madeni ya walimu, kama nilivyoeleza jana. Ni kweli madeni ya walimu yako katika kiwango cha juu, takribani shilingi bilioni 42, lakini hivi sasa tunachokifanya ni kuhakiki madeni haya. Nilitoa angalizo, yako madeni au madai yanayowasilishwa ambayo unajikuta yana mapugufu fulani, yako ambayo unajikuta hayana nyaraka mbalimbali za kiutumishi. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali tutajitahidi kuhakikisha kwamba tunalipa madeni haya haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa kupitia Bunge lako Tukufu, kwa kuwa mfumo wetu wa Human Capital Management System uko katika Halmashauri mbalimbali, niwaombe Waheshimiwa Wabunge ambao nao ni Madiwani katika Halmashauri husika waweze kufuatilia madeni haya, yako kiasi gani kwa mwezi husika, mwezi unaofuata unatarajiwa kulipa kiasi gani, lakini vilevile endapo kuna madai ambayo yamerudishwa changamoto ni nini, waweze kutusaidia.

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. KASUKU S. BILAGO aliuliza:- Kifungu cha 3 cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, na Kifungu cha 1(26) cha Kanuni za Kudumu za mwaka 2009 vinatoa tafsiri ya neno mwajiri kuwa ni mtu au taasisi ambayo mtumishi wa umma anaingia naye mkataba wa ajira na kumlipa mshahara. Je, kwa kuzingatia tafsiri hiyo, mwalimu ambaye ni mtumishi wa umma, mwajiri wake ni nani?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Pamoja na matatizo makubwa ambayo wanayo Walimu na nia ya Serikali kuyatatua ipo kada nyingine ambayo ni kama inasahaulika na hii ni kada ya Wakaguzi wa Elimu. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba kada hii nayo inatazamwa ili kwa pamoja na kwa kushirikiana na walimu waweze kusaidiana katika kuboresha elimu ya watoto wetu katika nchi yetu?

Name

Prof. Joyce Lazaro Ndalichako

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Answer

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali tayari imeshaanza mkakati wa kuboresha ukaguzi wa shule na sasa hivi hata kuna muundo mpya wa wakaguzi, ambapo hata jina la ukaguzi limebadilishwa, wanaitwa Wathibiti wa Ubora wa Elimu, na yote hii ni katika lengo la kuhakikisha kwamba tunaimarisha zaidi ukaguzi wa shule kwa kuangalia wakaguzi wanavyoweza kufanya kazi zao kwa kufanisi zaidi. Ukaguzi umeimarishwa mpaka katika ngazi za Wilaya, na huu muundo unaendana pia na maslahi bora kwa wakaguzi. (Makofi)

Name

Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. KASUKU S. BILAGO aliuliza:- Kifungu cha 3 cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, na Kifungu cha 1(26) cha Kanuni za Kudumu za mwaka 2009 vinatoa tafsiri ya neno mwajiri kuwa ni mtu au taasisi ambayo mtumishi wa umma anaingia naye mkataba wa ajira na kumlipa mshahara. Je, kwa kuzingatia tafsiri hiyo, mwalimu ambaye ni mtumishi wa umma, mwajiri wake ni nani?

Supplementary Question 3

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Kwa kuwa walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi walisimamia mtihani wa kidato cha Nne mwaka jana 2015 hawajalipwa fedha zao. Je, Serikali haioni ni mwendelezo wa kuwanyanyasa walimu na kuwaonea?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika asante. Mheshimiwa Pascal juzi wakati anajadili hapa nadhani alizungumzia suala la Mbozi, na ofisi yetu inalifanyia kazi kushirikiana na Hazina na katika mchakato tunaoondoka nao walimu wote ambao malipo yao yalikuwa bado hayajakamilika basi yataweza kusawazishwa na jambo hili likaweza kukaa vizuri, Serikali inafanyia kazi jambo hilo.