Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Primary Question

MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: - Je, ni nini kinachosababisha kesi 1,097 za kodi za muda mrefu zenye thamani ya shilingi trilioni 360 na dola za Marekani milioni 181.4 kutoamuliwa hadi sasa?

Supplementary Question 1

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, kwanza nasikitika kwamba swali limeuliza shilingi trilioni 360 lakini limejibiwa shilingi trilioni 4.21. Hata hivyo, ninayo maswali mawili ya nyongeza: -

La kwanza, kwa nini Serikali iliamua kukubali kupokea shilingi bilioni 700 kutoka katika kesi za malimbikizo ya makampuni ya madini maarufu “makinikia” badala ya shilingi trilioni 360 ambayo ni madai halali katika nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nini kilichowafanya TRA washindwe kukusanya malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi ya shilingi trilioni 7.54 na kusababisha ongezeko hili la malimbikizo ya kodi kufikia asilimia 94.6 lakini wakati huo huo uwezo wa TRA wa kukusanya malimbikizo hayo umekuwa ukishuka kila wakati na kufikia asilimia 10 tu na wakati huo TRA ikijivuna kwamba inaongeza makusanyo ya kodi?

SPIKA: Mheshimiwa Mpina kwanza nipate ufafanuzi; swali linazungumzia kesi 1,097; shilingi trilioni 360 na hizo Dola za Kimarekani milioni 181.4.

Mheshimiwa Naibu Waziri jibu linazungumzia mashauri kuwa 854 ambayo thamani yake ni shilingi trilioni 4.21 na dola za Kimarekani milioni 3.48. Haya ndiyo mashauri yaliyopo ambayo Serikali inayajua ambayo ni tofauti na ya Mbunge au mmechagua kati ya yale ambayo yapo, mmeamua kuyajibia haya ambayo mmeleta majibu? Nataka kuelewa kwanza hapa. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hayo ni mashauri ambayo yapo na Serikali tunayatambua.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, naona umesimama. Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, ufafanuzi wa hiyo sehemu ya kwanza, halafu nimpe fursa ya kujibu yale maswali mawili.

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwenye suala la msingi lile la shilingi trilioni 360; moja, Serikali haijakubali tu kimya kimya, haijakubali kupokea fedha hizo kwa maana ya kuacha shilingi trilioni 360, isipokuwa kilichofanyika, utakumbuka Serikali ilipeleka complain against makampuni hayo ya madini na baada ya complains zile kupelekwa…

SPIKA: Ngoja Mheshimiwa, twende kwa mtiririko mzuri. Ninachotaka kuelewa, swali la Mheshimiwa Mpina linazungumzia kesi 1,097; jibu linazungumzia kesi 854 na thamani ambayo Mheshimiwa Mpina anazungumzia ni shilingi trilioni 360, serikali inasema ni shilingi trilioni 4.21. Mimi nataka kuelewa ili nitoe mwongozo vizuri wa majibu hapa, namna Serikali ijibu. Haya majibu ambayo Serikali mmetoa, ni kwamba ndiyo kesi zilizopo ama idadi ni hii aliyotaja Mheshimiwa Mpina na kiasi cha fedha ni hiki alichotaja Mheshimiwa Mpina?

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, pana utofauti. Ile kesi kubwa aliyoiongelea ya Shilingi trilioni 360 ni ya upande wa makinikia. Hii ya mashauri ambayo yanaenda kwenye shilingi trilioni nne, ni ya mashauri ya kesi nyingine ambazo ziko TRAB na TRAT ambazo ndiyo Serikali inaendelea kuyafanyia kazi moja baada ya nyingine.

Kwa hiyo, pana mambo ya aina mbili na lingine limeongezeka ya yale yasiyo ya kesi na lile linakuwa la tatu. Kwa hiyo yameunganishwa pamoja.