Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Primary Question

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: - Je, Serikali haioni kuwa ipo haja ya kuwajumuisha Wenyeviti wa Halmashauri na Wabunge kwenye Kamati za kujadili na kupitisha maombi ya wavunaji wa mali za misitu kwenye Wilaya zetu nchini?

Supplementary Question 1

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru Serikali kwa majibu mazuri, na nimpongeze Naibu Waziri kwamba naye ameshafika Liwale kwa hiyo ninachokizungumza anakifahamu. Lakini hii sehemu ya pili anayosema kwamba Madiwani na Wabunge wanahusika, kwamba wanapata hizi taarifa, mimi nimekaa Liwale miaka sita, sijawahi kupata hii taarifa zikiletwa kwenye Baraza letu la Madiwani. Kwa hiyo jambo hili labda leo aagize hili jambo lifanyike lakini hili jambo halifanyiki kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili, kwamba Kamati hii ya Uvunaji anayeingia mwanakijiji ni Mwenyekiti wa Kijiji peke yake, sasa wanaovuna hesabu zinakuja pale wanaambiwa cubic meters yule mwanakijiji cubic meters hajui, magogo mangapi yanaondoka hajui, matokeo yake kuna magogo yale makubwa ambayo yana mashimoshimo wanayaacha, kwa hiyo uharibifu ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kufahamu, ni lini Serikali italeta fedha za upandaji miti kwenye vile vijiji ambavyo vina uvunaji huo ambao mimi nausema kwamba ni uvunaji wa holela?

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kuchauka Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Kamati hii ni Kamati ambayo inaundwa katika level ya Wilaya, lakini washiriki wa Kamati hii ni pamoja na Wenyeviti wa Vijiji na Watendaji wa Vijiji, pia inajumuisha Meneja wa Misitu ambaye anatoka Makao Makuu TFS lakini yuko pale Wilayani, kuna Afisa Misitu ambaye anakuwa ni mjumbe, vilevile kuna Afisa Tawala wa Wilaya ni mjumbe pia kuna Afisa Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaitamka hii Kamati ili afahamu Wajumbe wanaoingia mule ambao sasa ndiyo wanapeleka taarifa kwenye Baraza la Madiwani kama taarifa ya wale wote tu waliopitishwa kwenye orodha ya uvunaji wa mazao ya misitu na anayekuwa Mwenyekiti wa Kamati hii ni Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na Katibu ni Meneja wa Misitu anayetoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hii inapokuwa imekamilika inapelekwa kwenye Baraza la Madiwani. Baraza la Madiwani Wabunge ni Madiwani, wanashiriki pia Mwenyekiti wa Halmashauri ni Diwani na hawa Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji wanapopeleka maombi yao kwenye hii Kamati ya Wilaya tayari wanaonekana ni wajumbe ambao watapeleka tena kwenye WDC kama taarifa. Kwa hiyo taarifa hizi kuanzia level ya kijiji kwenda WDC na mpaka kufika kwenye Halmashauri, Mbunge na Mwenyekiti anakuwa ameipata kupitia Mabaraza yanayofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi niwaombe tu, kwa kuwa huyu Mjumbe ambaye ni Afisa Ardhi wa Wilaya anaingia kwenye hii Kamati na kama hafanyi hivyo basi anafanya makosa ni kwamba hii taarifa baada ya kukamilika inatakiwa ikasomwe kwenye Baraza la Madiwani ili Waheshimiwa Wabunge wafahamu lakini pia na Mwenyekiti wa Halmashauri afahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana ya Mwenyekiti wa Halmashauri ama Mbunge, wale ni wasimamizi, hawawezi kuingia kwenye mchakato kama ilivyo maelekezo na miongozo ya uvunaji wa misitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ameongelea kuhusu fedha, ni kweli kulikuwa kuna changamoto ya fedha, tukipeleka kwenye Halmashauri, halmahsauri zilikuwa hazifikishi kwenye maeneo husika ambayo kunatakiwa kuanzishwa vitalu na kupandwa hii miti ili kuziba yale maeneo ambayo yamekwisha vunwa. Kwa sasa tutapeleka hizo fedha lakini tutaleta mwongozo mahsusi wa kuhakikisha fedha hizi zinawafikia wale tu ambao wanahusika na fedha hizi na siyo Halmashauri kuelekeza kwenye matumizi mengine.Naomba kuwasilisha.