Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TUNZA I. MALAPO K.n.y. MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza: - Serikali ilikuwa na mpango mzuri juu ya uwepo wa nishati ya gesi asilia nchini, lakini mpaka sasa kumekuwa na sintofahamu juu ya mwendelezo wa uwekezaji wa miradi hiyo ikiwemo gesi ya Mkoa wa Mtwara. Je, nini kauli ya Serikali juu ya mwendelezo wa miradi hii nchini?

Supplementary Question 1

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; miongoni mwa ahadi za uendelezaji wa nishati ya gesi ni pamoja na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea. Naomba nipate ufafanuzi wa Serikali ni lini kiwanda hicho kitajengwa katika mkoa wa Mtwara?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; sisi watu wa Mtwara kila siku tunauliza gesi kwa sababu hatuoni ile michakato ambayo tulikuwa tunaiona pale nyuma. Sasa hivi Mtwara habari ya gesi ni kama haipo, kama imelala. Hata Ripoti ya CAG ukiisoma inaeleza kwamba matumizi ya gesi bado yako chini.

Sasa nataka tu kujua kauli ya Serikali; ni nini hasa inafanya ili sisi watu wa Mtwara turidhike kwamba ile gesi iliyogundulika Mtwara inafanya lile ambalo limekusudiwa na kuinua uchumi wa watu wa Mtwara na Taifa kwa ujumla? Nakushukuru. (Makofi)

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Tunza Malapo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali ilianza majadiliano na wawekezaji wa viwanda vya kutengeneza mbolea kwa kutumia gesi almaarufu kama petrochemicals. Hiyo gesi ndiyo malighafi kubwa katika utengenezaji wa hizo mbolea na vitu vya namna hiyo. Sasa kilichotokea ni kwamba biashara ile ilionekana haikuwa ya kutusaidia na kutufaa kwa kipindi hicho kwa sababu wakati duniani wanataka kununua kwa dola tatu sisi wa kwetu walikuwa ana bei ya chini kabisa ambayo ilionekana haitakuwa faida kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa sasa tumefungua upya milango ya majadiliano na wawekezaji mbalimbali wanaotaka kuwekeza katika viwanda kama hivyo akiwemo mwekezaji mkubwa wa Dangote naye ameonesha nia na bado tunaendelea kupokea maombi na majadiliano mbalimbali yanafanyika kuhakikisha kwamba sasa tunaweza kutumia gesi kutengeneza viwanda vya malighafi mbalimbali kama hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunakoelekea ni kuzuri na viwanda vya petrochemicals na vingine vitakuja. Gesi tutaitoa huko iliko na kuitumia kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili; ni kweli kwamba kwa muda mrefu kidogo pameonekana kama pamelala kwamba hakuna kilichokuwa kinaendelea. Kimsingi kilichokuwa kinaendelea ni kikubwa kuzidi kilichokuwa kinaonekana. Tunayo mikataba inayoitwa Production Sharing Agreement (PSA) ni mikataba ambayo inaingiwa kati ya Serikali na wale wawekezaji wanaokuja kuwekeza katika maeneo yetu ya gesi. Tukikubaliana tutazalishaje, tutagawana vipi na tutatumia vipi.

Mheshimiwa Spika, sasa majadiliano hayo yamechukua muda mrefu na marekebisho na mapitio ya mikataba hiyo imechukua muda mrefu, lakini sasa yamekamilika na tayari Serikali imetoa maelekezo na sasa kinachofanyika ile Kamati ya Serikali ya ku-negotiate mikataba imerudi tena kazini na tunatarajia mwezi wa 10 itakuwa imekamilisha kazi yake ya ku-negotiate sasa mikataba ya matumizi na unufaikaji wa gesi na tunatarajia kuanzia mwezi wa 11 basi mambo yataanza kuwa vizuri. Gesi hii tunayoitoa na kuitumia sasa itaongezeka zaidi kwa ajili ya manufaa ya nchi kwa ujumla. (Makofi)

Name

Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Primary Question

MHE. TUNZA I. MALAPO K.n.y. MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza: - Serikali ilikuwa na mpango mzuri juu ya uwepo wa nishati ya gesi asilia nchini, lakini mpaka sasa kumekuwa na sintofahamu juu ya mwendelezo wa uwekezaji wa miradi hiyo ikiwemo gesi ya Mkoa wa Mtwara. Je, nini kauli ya Serikali juu ya mwendelezo wa miradi hii nchini?

Supplementary Question 2

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nataka kuulizia kwamba mradi wa LNG wa Lindi mazungumzo yake yamechukua muda mrefu sana; ni zaidi ya miaka saba na hata wawekezaji wengine ambao wanataka kuwekeza kwenye shughuli za petrochemicals wameshakata tamaa. Ni nini sasa kauli ya Serikali kwamba mazungumzo hayo yanatarajiwa kukamilika?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Chikota kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema majadiliano yalisimama ili kupisha mapitio ya mikataba ya uzalishaji wa gesi na sasa majadiliano yameanza tena kuanzia mwezi wa nne na tunatarajia mwezi wa 10 majadiliano hayo yatakuwa yamekamilika na mwekezaji anaweza akaanza kuwekeza muda wowote baada ya hapo.

Mheshimiwa Spika, LNG ikitolewa kule tunakwenda mbele zaidi na kuisambaza katika maeneo mengine. Tutajenga vituo vitano vya ku-compress gesi na kuweza kuiuza kwa wananchi Dodoma ikiwa ni mojawapo.

Kwa hiyo, tutaweza kupata gesi asilia tukiwa hapa hapa Dodoma baada ya kukamilisha majadiliano na kuanza kujenga vituo vingine ambapo katika bajeti ya wenzetu wa TPDC imetengwa takribani shilingi bilioni 28 kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo vitano katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwishoni mwa mwaka huu wataanza kufurahia matumizi ya gesi kwa sehemu kubwa ya nchi yetu.