Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Primary Question

MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara ya Mianzini, Sambasha, Ngaramtoni hadi Hospitali ya Selari kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri ambayo yanaonesha kwamba kwa kweli Serikali inafanya kazi nzuri sana, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza, je, fedha ambazo kiasi kilichotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo shilingi bilioni 2.5 zinatosha kukamilisha barabara hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Jimbo la Arumeru Magharibi mazingira yake kwa maana ya miundombinu sio mizuri kabisa. Naomba kujua je, tuna barabara mbili, barabara ya Malalua – Nduruma – Bwawani inayounganisha Simanjiro na Arumeru Magharibi na barabara ya TPRA – Likamba inayounganisha na Monduli.

Je, haioni sasa ni busara kwa ajili ya mazingira ya Jimbo hilo magumu barabara hizo mbili kupandishwa hadhi kupelekwa TANROADS? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba fedha iliyotengwa haiwezi ikakamilisha kilometa 18, lakini hii ni fedha ya awali kwa ajili ya kuanza mradi na wakati huo Serikali itaendelea kutafuta fedha ili kukamilisha mradi huu. Mradi huu utaenda kwa awamu, fedha iliyopatikana tutaanza na kazi na kazi itakavyozidi kupatikana basi tutakamilisha huu mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili nimshauri Mheshimiwa Noah Lemburis, Mbunge wa Arumeru Magharibi kwamba hizo barabara ambazo amezitaja kuna utaratibu maalum ambao kama barabara inatakiwa ipandishwe hadhi zipo taratibu, ziko kanuni ambazo zinapitia kwenye vyombo kuanzia Halmashauri kwenda kwenye DCC, kwenda Mfuko wa Barabara wa Mkoa hadi RCC ambao wanaleta hayo maombi kwenye Wizara yetu na sisi tunafanya tathmini na kuona inakidhi vigezo vya kupandishwa daraja ili barabara hizo ziweze kuhudumiwa na Wakala wa Barabara TANROADS. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Noah uende ukafanya mchakato huo nasi tutafanya tathmini na kama zitakidhi vigezo barabara hizo zitasimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Ahsante.

Name

Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Primary Question

MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara ya Mianzini, Sambasha, Ngaramtoni hadi Hospitali ya Selari kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 2

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Kwa kuwa Mkoa wa Morogoro ni Mkoa pekee nchini ambao haujaunganishwa kwa kiwango cha lami na mikoa mitatu; Mkoa wa Lindi, Mkoa wa Ruvuma, na Mkoa wa Njombe.

Sasa swali langu dogo la nyongeza ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye kilometa 223 kutoka Ifakara – Mlimba mpaka Madeke -Lupembe – Njombe? Ahsante. (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Godwin Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kunambi kwa kufuatilia hiyo barabara. Mikoa aliyoitaja ni kweli barabara hazijaunganishwa kwa kiwango cha lami, lakini barabara zipo japo zinapitika kwa shida sana.

Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kunambi kwamba katika bajeti tunayoanza kuitekeleza atakubaliana nami kwamba Serikali imetenga fedha kuanza ujenzi wa barabara hiyo ya kuanzia Ifakara – Mlimba – Madeke mpaka Kibena Junction kwa kiwango cha lami.

Kwa hiyo, kwenye bajeti tunayoanza kuitekeleza naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kunambi na wapiga kura wa Jimbo la Mlimba kwamba Serikali imejipanga utekelezaji kwa kiwango cha lami wa barabara hiyo utaanza. Ahsante. (Makofi)

Name

George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Primary Question

MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara ya Mianzini, Sambasha, Ngaramtoni hadi Hospitali ya Selari kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 3

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa daraj ala Godegode linalounganisha majimbo mawili yaliyoko katika Wilaya ya Mpwapwa lilichukuliwa na maji msimu wa mvua wa mwaka 2020 na kusema ukweli uchumi wa wananchi wa Majimbo haya mawili, Jimbo la Kibakwe na Jimbo la Mpwapwa yanategemea sana uwezo wa daraja hili, lakini pia tukizingatia kwamba daraja hili ujenzi wake uko kwenye Ilani ya Uchaguzi 2020/2025.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa daraja hili? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Malima Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimuombe Mheshimiwa Malima baada ya session hii tuweze kuonana ili kama daraja limeondoka, kujenga daraja inaweza ikachukua muda, lakini tuna madaraja ya chuma ambayo yanaweza yakatumika kwa muda wakati Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kujenga hilo daraja kwa muda mrefu. Lakini kwa maana inaunganisha Halmashauri au Wilaya mbili nadhani itakuwa ni busara tuonane nae ili tuone na wataalam kupitia Bunge hili Mkoa huu wa Dodoma basi waende wakafanye tathmini ili tuweze kuona kama tunaweza tukajenga daraja la muda wakati tunatafuta fedha ya kujenga daraja la kudumu ili shughuli za uchumi na usafirishaji na usafiri wa wananchi ziweze kufanyika katika kipindi cha muda mfupi. Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Primary Question

MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara ya Mianzini, Sambasha, Ngaramtoni hadi Hospitali ya Selari kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 4

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona na naomba nitumie fursa hii pia kukupongeza kwa Kiti hicho ulichokikalia, kwa kweli umekitendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu dogo la nyongeza linahusu ahadi ya muda mrefu sana ya barabara ya lami ambayo iliahidiwa itoke Longido mpaka Siha kuunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Kilimanjaro kutokea Longido ambayo iko kwenye Ilani ya mwaka 2015 mpaka sasa sijajua hatua ya Serikali katika kutekeleza ahadi hiyo imefikia wapi?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema kwenye majibu mengine barabara aliyoitaja iko kwenye Ilani na imeahidiwa na viongozi wa Kitaifa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kiruswa kwamba ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami utategemea na upatikanaji wa fedha na kadri Serikali tunavyoendelea kupata fedha nataka kukuhakikishia kwamba ni azma ya Serikali kuijenga hiyo barabara ikiwa ni pamoja na kutimizia ahadi za viongozi kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, tuvute tu subira, cha msingi tuendelee kufanya makusanyo ya fedha. Basi tutakapopata, hizo barabara zitajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante sana. (Makofi)