Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Primary Question

MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi wa Kijiji cha Kintanula Kata ya Mwamagembe katika Jimbo la Manyoni Magharibi mawasiliano ya uhakika ya simu?

Supplementary Question 1

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi wa Kintanula ni walinzi shirikishi wa hifadhi kubwa kabisa ya Rungo Mhesi Kizigo ambayo ipo pale na wanasaidia kupambana na majangili kwa njia ya mawasiliano. Sasa kupitia mnara huu, wananchi hawana mawasiliano sasa. Ili kuepusha ajali nyingi ambazo zinatokea za watu kuanguka juu ya miti na kuvunjika mgongo na wakati mwingine viuno; je, Serikali inasemaje? Ni lini itakwenda kukamilisha mradi huu ili wananchi hao pia wanufaike na mradi huu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna mnara ambao unajengwa pale katika Kijiji cha Mhanga, ulisimama Kitongoji cha Jirimli, ulikuwa unajengwa na Halotel. Sasa Serikali ipo tayari kuzungumza na Halotel ambao walisimamisha ujenzi wa mnara huu ili waendelee? (Makofi)

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, Kijiji hiki kitaingizwa katika utaratibu wa kufanyiwa tathmini ili tujiridhishe ukubwa wa tatizo na kujua kama tunahitaji kwenda kuweka mnara au tunaenda kuongeza tu nguvu ya mnara uliopo ili uweze kuhudumia wananchi wa pale.

Mheshimiwa Spika, pia lengo la Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ni kufikisha mawasiliano kwa wananchi wote. Kwa hiyo, hilo ni jukumu la Serikali, nasi Serikali tumejipanga kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vijiji ambavyo vinahitaji mawasiliano kikiwemo na Kijiji ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja, kitakuwepo ndani ya mkakati wa Kiserikali wa kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, pia kuhusu masuala ya Halotel; katika ujenzi wa minara, wakandarasi wengi ambao wanapewa tender za ujenzi wa minara hii ni kwamba wamekumbana na changamoto nyingi katika kipindi hiki ambacho tulikuwa tuna Covid 19, lakini pia katika baadhi ya vibali ambavyo walikuwa wanaomba, vingine vilichelewa kwa sababu ambazo zilikuwa nje ya uwezo wao. Sasa Serikali imejipanga kwamba katika vipengele ambavyo vinahusisha na vibali ambavyo Serikali moja kwa moja inahusika, tunaenda kuhakikisha kwamba tunashirikiana na wenzetu ambao wanatoa vibali ili vibali vile vinatoka kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)