Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:- Je, kwa nini wazazi wanachangishwa michango ya kuchangia elimu wakati Serikali inasema Elimu kwa Shule ya Msingi na Sekondari ni bure?

Supplementary Question 1

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu ya Serikali, hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa mapokeo ya wananchi kupitia matamko mbalimbali ya Serikali na kwenye swali langu nimeuliza elimubure kama ilivyotamkwa mara ya kwanza tofauti na waraka. Mapokeo ya wananchi kulingana na kwamba ni elimubure wamekuwa na uitikio hafifu wa kuchangia michango wakiamini elimu ni bure kama ilivyotamkwa. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kulieleza Bunge lako na wananchi wakajua sasa kwamba kilichobadilika ni elimu bila ada na utaratibu wa michango umebadilishwa tu kwa kwenda kuomba kibali wanapaswa kuchangia maendeleo ya shule?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa nia ya Serikali ilikuwa ni kuwapunguzia wazazi mizigo au changamoto ambazo wanazipata na shida ya huko sio ada peke yake, Serikali kwa nia hiyo hiyo njema hawaoni sasa ni muda muafaka wa kurudi kufanya tathmini kwa kuwashirikisha kikamilifu wadau wa elimu wakawaambia changamoto kubwa iliyopo badala ya ada peke yake? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida Joseph Khenan, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ametaka Serikali tueleze kwamba, hii sio elimubure ni elimu bila ada. Niseme tu kabisa kwamba Waraka wa Elimu Na.5 wa mwaka 2015 ulishazungumza, kwamba tulichokisema elimumsingi ni elimu bila ada wala sio bila kitu kingine chochote, elimu bila ada, lakini, Serikali ilitoa tena Waraka mwingine Na.3 wa mwaka 2016, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba, katika ule waraka tumeainisha wajibu; kuna wajibu wa Serikali na vilevile wa mwananchi. Wajibu wa mwananchi ni pamoja na kushiriki katika miradi ya maendeleo ya Kiserikali ikiwemo kujenga miundombinu kama madarasa, vyoo na vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumeainisha pale, lakini sasa tuliweka option ya kwamba wale wananchi wasilazimishwe, wachangie kwa hiari yao kwa kushikirikishana na Bodi za Shule. Huo ndio msimamo wa Serikali mpaka sasa hivi kwamba, elimu bila ada bado inaendelea kwa sababu lengo letu ni kuwasaidia watoto wale wa chini ili watoto wote waweze kupata elimu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Serikali tufanye tathmini upya; tunaendelea kufanya tathmini kila wakati na tunaendelea kuangalia au kuboresha kadri muda unavyokwenda. Kwa hiyo, tumepokea kwa sababu ndio wajibu wa Serikali kuhakikisha kama kuna mahali kuna upungufu, basi tunarekebisha. Hili katika jibu la msingi ni kwamba, nchi nzima sasa hivi tuna watoto wa sekondari zaidi ya milioni 14. Kwa hiyo, ni lazima Serikali tufanye upya tathmini ili kuangalia namna gani tunasaidia Sera ya Elimu na elimu kwa ujumla nchini. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Kama alivyoeleza Waraka Na.3 wa mwaka 2016, umeainisha bayana wajibu wa wazazi katika kushiriki kwenye kuchangia maendeleo ya shule. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wazazi kuendelea kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali kwa sababu mazingira ya shule yanapokuwa mazuri na watoto wao wanakuwa na uhakika wa kupata elimu iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa tunasisitiza kwamba mwanafunzi asifukuzwe shule kwa sababu ya michango. Hilo ndio jambo ambalo lazima katika kutekeleza Waraka huo, wazingatie kwamba ni marufuku kumfukuza mwanafunzi yeyote shuleni kwa sababu ya michango. Ahsante sana. (Makofi)