Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa maboma ya Shule za Sekondari Bombo na Ndungu ili Kidato cha Tano kianze baada ya mabweni ya wasichana kukamilika?

Supplementary Question 1

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, shule hizi ziliahidiwa tangu 2019/2020 kwamba zingeanza high school; na madarasa yalishakamilika Shule ya Bombo na bweni lilikuwa ni moja tu ambalo lilikuwa lijengwe ili wavulana nao wapate nafasi. Cha kusikitisha ni kwamba sasa yamepelekwa tena mpaka Septemba 2022. Swali langu ni kwamba: Kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kuona kwamba high school ni muhimu sana katika shule zetu ili wanafunzi wetu waweze kuendelea na masomo ambayo yatawapa ujuzi zaidi katika maisha yao? (Makofi)

Swali la pili ni kwamba, kwa kuwa somo la Stadi za Kazi mashuleni linafanywa zaidi kinadharia: Je, Serikali ina mpango gani kuongeza nguvu katika kufanya masomo ya vitendo kusudi wanafunzi wanapomaliza shule wakaweze kujiajiri kwa kuzingatia kwamba Serikali haiwezi kuajiri wanafunzi wote wanaomaliza shule? Ahsante. (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Naghenjwa amejaribu kuainisha, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kufungua shule hizo kama ambavyo ilikuwa imeahidi katika mwaka wa fedha 2019/2020? Nimweleze tu kabisa kwamba Serikali inafahamu umuhimu wa kuanzisha Kidato cha Tano na Sita katika shule hizo na ndiyo maana tumekuwa tukipeleka fedha kila mwaka ili kuhakikisha kwamba shule hizo zinakidhi vigezo vyote vinavyotakiwa. Kwa sasa kuna upungufu wa miundombinu ya msingi; madarasa bado hayajajitosheleza, hakuna maabara na hakuna maktaba katika maeneo hayo. Kwa hiyo, tunataka tukamilishe ili tuweze kuzifungua shule hizo zikiwa na vigezo vyote vilivyokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kuhusu stadi za kazi mashuleni kwamba wanafunzi kwa sasa wanasoma nadharia, nieleze tu kwamba Sera ya Serikali ni kuhakikisha kwamba stadi zote za kazi mashuleni wanafunzi wanafanya kwa vitendo. Ndiyo maana unaona katika mwaka uliopita 2020 kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, watoto waliomaliza Kidato cha Nne kwa mfano kwenye masomo ya sayansi hawakufanya ile alternative to practical, walifanya ile real practical kwenye mitihani yao.

Mheshimwia Naibu Spika, kwa hiyo, hii inaonesha tu kwamba nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaondoa hii dhana ya nadharia na ndiyo maana katika bajeti zetu unaona tumejenga maabara karibu katika shule zote nchini na tutahakikisha tutazikamilisha kwa wakati ikiwemo kuzipelekea vifaa. Ahsante.