Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maida Hamad Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:- Vipo baadhi ya Vijiji vilivyoorodheshwa kwa ajili ya kufikiwa na miradi ya TASAF III Awamu ya Kwanza upande wa Zanzibar lakini bado havijafikiwa na mradi unaelekea mwisho:- Je, Serikali inasemaje juu ya maeneo ambayo hayajafikiwa na Mradi?

Supplementary Question 1

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa utekelezaji wa TASAF III, Awamu ya Kwanza wapo wafaidika 1,000 na zaidi wanaotoka katika Shehia 78 za Pemba ambao walikuwa katika utaratibu wa malipo na majina yao yaliachwa. Je, Serikali inasema nini kuhusu kulipwa fedha zao wafaidika hawa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa wananchi hawa maskini waliingia katika mikopo mbalimbali kwa kutegemea kwamba fedha wanazoendelea kuzipata zinawasaidia katika kujikimu kimaisha. Je, Serikali inaweza kututhibitishia kwamba ni bajeti ipi itawalipa fedha hizi kwa sababu mradi wa TASAF III, Awamu ya Kwanza umeisha?

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maida, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mwaka jana mwezi Juni ulifanyika uhakiki wa kaya zote ambazo zinapokea fedha za TASAF. Kaya zile ambazo hazikutokea kwenye uhakiki ziliondolewa kwenye mpango mpaka pale watakapokuja tena kuhakikiwa ili malipo yao yaweze kuendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa kesi hii ya Pemba kwenye Shehia 78 kuna walengwa 1,200 ambao hawakujitokeza kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki na malipo yao yalisitishwa. Hata hivyo, ilipofika uhakiki wa awamu ya pili uliofanyika mwezi Desemba, 2020 walengwa 300 walijitokeza na walengwa 900 bado hawajajitokeza kufanyiwa uhakiki.

Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pale tu walengwa hawa watakapojitokeza kufanyiwa uhakiki basi malipo yao yatarejeshwa na wataendelea kupokea fedha hizi za TASAF.

Mheshimiwa Spika, swali lake la nyongeza la pili ameuliza ni nini Serikali inafanya, kama nilivyojibu kwenye swali lake la nyongeza la kwanza ni pale tu hawa 900 watajitokeza kufanywa uhakiki basi malipo yao yatarejeshwa na wataendelea kuwepo kwenye mpango.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.